Jubilei ya Miaka 140 ya Uinjilishaji na Maendeleo Nchini Congo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 140 ya Uinjilishaji nchini Congo. Kilele cha Maadhimisho haya ni tarehe 4 Juni 2023. Hizi zilikuwa ni juhudi za uinjilishaji zilizotekelezwa na Papa Leo XIII. Kumbe, hili ni tukio la kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuliwezesha Kanisa kutangaza amani na kuendelea kuinjilisha. Katika miaka hii 140 kumekuwepo na wainjilishaji wengi waliosimama kidete kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake kwa bidii, juhudi, maarifa, kwa upendo na bila woga. Kardinali Michael Czerny, kama sehemu ya maadhimisho haya, Jumamosi tarehe 3 Juni 2023 katika hotuba yake amekazia kuhusu: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; dhamana ya uinjilishaji sanjari na mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na changamoto za Kanisa nchini Congo: Umaskini, Afya, Mazingira, Elimu na Uinjilishaji. Kardinali Michael Czerny anasema anapenda kuungana na watu wa Mungu nchini Congo kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 140 ya Uinjilishaji na kwamba, hotuba yake inajikita katika mchakato wa uinjilishaji na maendeleo fungamani ya binadamu, mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walikazia mchakato wa uinjilishaji unaopata chimbuko lake katika taalimungu yenye kumtazama mwanadamu mintarafu Maandiko Matakatifu sanjari na mahusiano yake na jirani zake, jumuiya na Injili katika ujumla wake.
Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia: Haki, Amani na Mshikamano na kwamba, umaskini katika ulimwengu mamboleo unajionesha kwa njia ya ukosefu wa mambo msingi katika maisha kama vile: makazi bora, chakula na ajira mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika ulimwengu wa utandawazi, kanuni auni inapaswa kushika mkondo wake. Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa anatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu kama ushuhuda wa imani tendaji. Kardinali Michael Czerny amebainisha changamoto zinazolikabili Kanisa nchini Congo kwa kutambua kwamba, uinjilishaji nchini Congo ulikwenda sanjari na ukoloni, kumbe, kuna vivuli vya giza katika mchakato wa uinjilishaji nchini humo. Kati ya changamoto mamboleo zinazolikabili Kanisa nchini Congo ni umaskini unaojionesha kwa ukosefu wa ajira kwa vijana wengi wa kizazi kipya. Kanisa limechangia kwa kiasi kikubwa maboresho ya huduma ya afya ya jamii nchini Congo, lakini huduma hii, bado ni changamoto kubwa kama sehemu ya mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu: Ikumbukwe kwamba, huduma bora ya afya na mazingira bora ni sawa na chanda na pete, ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Ili kukabiliana na changamoto hii, kuna haja ya kukuza na kudumisha utawala bora unaozingaria sheria, kanuni na taratibu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kuondokana na kishawishi cha uchu wa mali, madaraka na utajiri wa chapuchapu!
Uchafuzi wa mazingira ni chanzo kikuu cha kuenea kwa umaskini na kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni ukweli usiopingika kwamba Kanisa limekuwa kati ya wadau wakubwa wa maendeleo katika sekta ya elimu kabla na baada ya uhuru nchini Congo. Mchango wa Kanisa Katoliki katika utoaji wa huduma ya elimu umekuwa ni kuanzia shule za chekechea, awali, msingi, sekondari, vyuo vya ufundi stadi hadi elimu ya juu. Kanisa Katoliki linatambua kwamba kila binadamu ana haki ya msingi ya kupata elimu makini bila kujali itikadi za kisiasa, kidini, kijinsia, kabila au taifa. Lengo kuu la elimu Katoliki ni kumfunda mtu mzima; kiakili, kimwili, kiroho, kijamii na kimaadili, kwa kufanya hivyo, shule za Kanisa zinawaanda vijana wa kike na kiume kwa kesho iliyo bora zaidi. Kipaumbele kiwe ni elimu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea: amani utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mchakato wa Uinjilishaji Barani Afrika unapania pamoja na mambo mengine kumletea mwanadamu ukombozi halisi kutoka katika umaskini, magonjwa na ujinga.
Waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni mchakato ambao umeliwezesha Kanisa kupyaisha maisha na utume wake, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nyakati hizi, kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa kwa kukazia utamaduni wa kusikiliza, ushiriki mkamilifu wa watu wateule wa Mungu kwa kumsikiliza kikamilifu Roho Mtakatifu, ili kusoma alama za nyakati. Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, ana matumaini kwamba, mchakato wa uinjilishaji na maendeleo nchini Congo unapaswa kusimikwa katika hali ya kujiamini, ujasiri, matumaini na furaha ya kweli.