Tafuta

Kanisa la Zambia na Malawi wamepata Balozi mpya wa Vatican. Kanisa la Zambia na Malawi wamepata Balozi mpya wa Vatican. 

Mons.Luca Perici ni Balozi Mpya wa Vatican nchini Malawi na Zambia

Alikuwa ni Mshauri wa Ubalozi wa Vatican aliyeteuliwa na Papa kuwa Balozi wa Vatican.Wakati huo huo Papa amemteua Askofu mpya wa jimbo katoliki la Zomba,Malawi Mhs.Padre Alfred Chaima,aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la maaskofu;Papa pia ameteua Askofu Mkuu wa Antannarivo,Madagascar.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baba Mtakatifu amemteua Balozi mpya wa Vatican nchini Zambia na Malawi, Monsinyo Gian Luca Perici, aliyekuwa Mshauri wa Ubalozi kwa kumwinua wakati huo huo kuwa na makao ya Bolsena na hadhi ya Uaskofu Mkuu.

Wasifu wake

Monsinyo Gian Luca Perici alizaliwa huko Bassano ya Grappa (Vicenza), Italia tarehe 17 Septemba 1964. Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 21 Septemba 1991 kwa ajili ya Jimbo la Velletri-Segni. Katika majiundo yake amepata shahada ya Sheria za Kanoni. Aliingia kuwa sehemu ya shughuli za huduma ya kidiplomasia Vatican mnamo tarehe Mosi 2001, na kutoa huduma yake katika balozi za Vatican nchini Mexico, Haiti, Malta, Angola, Brazili, Sweden, Hispania na Ureno. Anaufahamu wa lugha ya kifaransa, kiingireza, kireno na kihispania.

Malawi: Askofu wa Jimbo la Zomba

Baba Mtakatifu Francisko  wakati huo huo tarehe 5 Juni amemteua Askofu wa Jimbo katoliki la Zomba (Malawi) Mweshimiwa Alfred Chaima, kuhani wa Blantyre, ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu katoliki nchini Malawi.

Curriculum vitae/ wasifu wake

Mheshimiwa Padre  Alfred Chaima alizaliwa tarehe 14 Julai 1970 huko Nambera, Jimbo kuu la Blantyre. Majiundo yake ni seminari ndogo ya Mtakatifu Pius XII, mafunzo ya falsafa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Anthony huko Kachebere na taalimungu katika Seminari Kuu ta Mtakatifu Petro huko Zomba, kwa kupata diploma ya Taalimungu katika Chuo Kikuu cha Malawi. Alipewa daraja la upadre mnamo tarehe 4 Julai 1984 kwa ajili ya jimbo kuu la Blantyre.

Amefunika nyadhifa ikiwemo  mafunzo zaidi:

mwalimu katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Patrick na Paroko wa parokia ya Mzedi (1998-2000); paroko wa parokia ya Njuli (2000-2001); Gambera na mwalimu katika Seminari ya Mtakatifu Pius XII (2000-2004); shahada ya elimu ya Taalimungu, leseni ya taalimungu ya kichungaji na udaktari katika falsafa ya Taalimungu  katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, jijini Nairobi (2004-2010); profesa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (2006-2010 na 2016-2022). Ameawahi kuwa  katibu wa askofu mkuu wa Jimbo Kuu katoliki  Blantyre na Kansela wa jimbo kuu (2010-2012); Paroko msaidizi wa Kanisa kuu na mratibu wa kituo cha kichungaji jimbo kuu, Limbe (2010-2014); mkurugenzi wa Kituo cha Kichungaji cha Nantipwili, Jimbo Kuu la Blantyre (2014-2022); profesa katika Chuo Kikuu cha Malawi (2015-2022); hadi uteuzi huo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu la Malawi

Madagascar: Askofu  Raoelison ni Askofu Mkuu wa Antannarivo

Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 5 Juni 2023 amepokea barua ya kung'atuka katika shughuli za kichungaji kwa Askofu Mkuu wa Antannarivo nchini Madagascar iliyowakilishwa na Askofu Mkuu Odon Marie Arsène Razanakolona na wakati huo huo Papa akamteuai Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu hilo hilo, Askofu Jean de Dieu Raoelison, ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Askofu wa Jimbo katoliki la  Ambatondrazaka, Madagascar.

05 June 2023, 15:20