Wanawake Wakatoliki Wajenzi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu!
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - WAWATA, Vatican.
Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, “Unión Mundial de las Organizaciones Femeninas Católicas, UMOFC, ulioanzishwa kunako mwaka 1910, kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 20 Mei 2023 unaadhimisha mkutano mkuu wa uchaguzi unaonogeshwa na kauli mbiu Wanawake Wakatoliki Wajenzi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu kwa amani ya Ulimwengu. Mkutano umefunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu Dominika tarehe 14 Mei 2023 huko mjini Assisi, nchini Italia. Kwa kipindi chote hiki wanawake wakatoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanajadili kuhusu: “Wanawake ndani ya Kanisa.” Huu ni muda muafaka wa kupokea taarifa, kuchambua baadhi ya vipengele vya Katiba, ili kuvifanyia marekebisho; Miradi mipya, maazimio, vipaumbele vya kufanyiwa kazi, uchaguzi na hatimaye, hija ya kiroho mjini Assisi. Mkutano huu ni muda wa sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kusikilizana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, kwa namna ya pekee, Jumamosi tarehe 13 Mei 2023 tumepata nafasi ya kusherehekea Sikukuu ya Mama Bikira Maria wa Fatima kwa kupata fursa ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Mkutano huu na Baba Mtakatifu Francisko ni mwanzo wa Mkutano mkuu wa uchaguzi utakaofanyikia kuanzia tarehe 14 Mei hadi tarehe 19 Mei, 2023 huko Assisi nchini Italia. Tanzania ambayo inashiriki mkutano huo imewakilishwa na Padri Florence Rutaihwa – Mkurugenzi wa Kurugenzi ya kichungaji TEC, Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa na Bi Happiness Mbepera aliewakilisha WAWATA chipukizi. Kabla ya kuzungumza na Baba Mtakatifu, wanawake walipata nafasi kushirishana matokeo ya Mradi wa “WWO” (World Women Observatory) inayoendelea ya kusikiliza kilio cha mwanamke wa Afrika. Mradi huu ulianza kazi kunako mwaka 2021 huko Amerika ya Kusini ilikuwa na lengo la kuwasikiliza wanawake pamoja na watoto na wanaume wanaopitia changamoto au nyanyaso mbalimbali ili kuwasaidia kupaza sauti zao. Baada ya Amerika ya Kusini mradi huo ulianza kufanyiwa kazi Barani la Afrika mwezi Mei, 2022 na mpaka sasa mradi umeweza kuwafikiwa Wanawake 10,000 na kusikiliza wabobezi zaidi ya 210 wa masuala ya nyanyaso za wanawake. Katika filamu halisi iliyorekodiwa Barani Afrika tunapata kusikia sauti ya Mama Agnes alietelekezwa na mume wake baada ya kuzaa mtoto mlemavu. Mama huyu hakukata tamaa, alipambana na kumsomesha binti yake na sasa anamalizia degree ya pili ya masomo ya saikolojia. Hawa ndio wanawake wa shoka ambao wameshika imani na kusimama kidete kuhakikisha familia inasimama.
Akizungumza kwa niaba ya Wanawake wote, Rais wa WUCWO Mama Maria Lia Zervino Sevidora alimkaribisha Baba Mtakatifu akianza kwa kumshukuru kutenga muda wa kukutana na wanawake lakini zaidi kwa namba ambavyo amekuwa akiwapa nafasi kutekeleza wito wetu wa kupaza sauti ya wasio na sauti. Mama Maria Lia alimweleza Baba Mtakatifu kuwa tunapomsherehekea mwanamke hasa yule anaeishi katika mazingira magumu tunaimba wimbo wa “Magnificat” tukijaribu kuwaleta kwenye huruma na upendo wa Mungu, wale wote waliosukumwiza pembezoni mwa vuipaumbele vya jamii; kwa kuwaleta kwenye mwanga kupitia Mashirika yasiyo ya kidini, kanisa na mashirika mengine. Akiwahutubia wanawake tuliokusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko ameanza kwa kuwakaribisha wanawake wote walioweza kufika kwenye uwanjan na hata wale waliokuwa wanafuatilia mkutano huo wa kipekee kwa njia ya mtandao. Aliwashukuru kwa kazi kubwa inayofanywa na wanawake wakatoliki sehemu mbalimbali za dunia. Aliwatia moyo na kuwatia shime kuendelea kusikiliza kilio cha wanawake na wote wanaopitia nyanyaso za aina mbalimbali. Baba Mtakatifu anasema, tunapoelekea Assisi tutasindikizwa kwa sala za mtangulizi wetu na mwombezi wetu Mama Bikira Maria. Baba Mtakatifu anasema kazi ya wanawake ni mfano halisi wa Msamaria mwema. Anaendelea kusema nafasi ya mama ni ya pekee kwa namna tulivyobarikiwa kushiriki kazi ya uumbaji na kutunza uumbaji kama alivyofanya Mama Bikira Maria, Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Anasema mwanaume bila mwanamke ni upweke na utupu na haya tunayasoma hata kwenye Maandiko Matakatifu wakati wa kazi ya uumbaji.
Tumekumbushwa kuelekeza macho na akili zetu Fatima kutazama sura ya huyu Mama Bikira Maria alieshika nafasi yake kutimiza kusudi la Mungu la Ukombozi. Bikira Maria anakuwa shuhuda wa kwanza wa Injili kwa kushirikiana na wanafunzi wa Yesu hata kukabidhiwa mwanafunzi aliempenda zaidi. Tumealikwa kufanya aliyofanya Mama Bikira maria, kuendelea kuwa mashuhuda wa Injili tukiumba na kutetea uhai. Ili tuweze kufanya kazi ya Eva Mpya aliyofanya Mama Bikira Maria ni lazima tuwe na ushirika na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anatualika wanawake wote kuendelea kutembea na Kanisa la kisinodi na anaahidi kutembea pamoja na wanawake wote akitusindikiza kwa sala ili kuendelea na kazi tunazofanya za kusikiliza kilio cha wale waliosukumizwa pembezoni. Baba Mtakatifu hakuishia kuwabariki wanawake, bali anaomba pia sala zetu. Nipende kuwapongeza viongozi wote wa WAWATA majimbo yote Tanzania kwa wanajisadaka bila kujibakisha kwa ushiriki wao katika project ya WWO ambapo Tanzania ilifanikiwa kuwafikia wanawake takriban 400. Kwa namna ya pekee ninawapongeza viongozi wapya wa jimbo kuu la Dar es salaam waliochaguliwa kuongoza WAWATA kwa kipindi cha miaka mitanu ijayo. Hongera sana Mama Stella kahwa – Mkiti, Mama Yolanda Kahunduka Mmkiti, Mama Flora Mugala Katibu mkuu, Mama Hilda Leba Katibu msaidizi na Mama Dora Chikongowe Mtunza hazina. Nipende kuwaalika wanawake wote wanaoteseka na kuachwa peke kulea familia wasikate tamaa, wafuate mfano wa Mama Agnes anaekuwa kielelezo na mfano wa kuigwa. Asanteni sana Wanawake Wakatoliki Tanzania kwa sala zenu na ushiriki wenu katika utume.