Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Vatican na Tanzania: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia Dominika 14 Mei hadi tarehe 21 Mei 2023 linafanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina” inayofanyika kila baada ya miaka mitano, tayari wamekwisha kusali na kutembelea Mabaraza mbalimbali ya Kipapa kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Jumatano tarehe 17 Mei 2023 Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilipata bahati ya kutembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Ilikuwa ni fursa ya kukutana na kusalimiana na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, kusikiliza historia ya mahusiano kati ya Vatican na Tanzania hasa katika mchakato wa kutafuta na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tukio hili adhimu limehudhuriwa pia Jumaa H. Aweso (Mb), Waziri wa Maji ambaye amewaomba viongozi wa dini kushirikiana na kushikamana na Serikali katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuwapatia watanzania maji safi na salama, sanjari na kukazia malezi, makuzi na maadili mema; haki, amani na mshikamano wa Kitaifa. Anawaalika viongozi kuwa ni wachaji wa Mungu. Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Venance Mabeyo, kama mwakilishi wa waamini walei nchini Tanzania yuko pia kwenye hija ya kitume ya Maaskofu Katoliki Tanzania. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia amewakaribisha Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuonesha nia, dhamira na ombi la kutaka kutembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Italia wakati wa hija yao ya kitume mjini Vatican. Huu ni ubalozi wa watanzania wote na ujio wao ubalozini hapo ni neema na baraka tele. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina dini lakini watanzania wana dini na imani zao, kumbe, Maaskofu ni sehemu kubwa ya uwakilishi wa sehemu kubwa ya nchi na watanzania katika ujumla wao.
Hii ni hija ya kihistoria inayofanyika kila baada ya miaka mitano, kumbe, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameandika historia ya kuwapokea Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha Mwaka 2023. Huu ni mwendelezo wa historia iliyoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Thabit Kombo Jecha walipotembelea mjini Vatican baada ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, na hivyo kutunukiwa Nishani ya Amani na Mtakatifu Yohane wa XXII. Baba Mtakatifu Yohane wa XXII alitambua juhudi kubwa zilizofanyika za kuunganisha Tanganyika iliyokuwa nchi huru na Zanzibar iliyokuwa imejikwamua kutoka kwa kwenye makucha ya wakoloni kwa Mapinduzi matukufu. Mtakatifu Yohane XXIII ameandika historia kubwa ya mahusiano na Tanzania. Ndiye aliyetunga Sala ya Kuiombea Tanzania. Rej. Misale ya Waamini Ukurasa 1510. Kumbe, kuna historia ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican na jinsi ambavyo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyokuwa akitenda shughuli zake kwa ajili ya kutafuta haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye makao yake makuu mjini Roma, ilianzishwa rasmi tarehe 7 Februari 1968 kwa kujikita katika Sala, Maskini na Amani duniani; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Jumuiya hii pia ina historia ndefu ya mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia katika kutafuta na kukoleza haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kumbe, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Serikali ya Italia na Vatican wana mahusiano ya pekee sana na Tanzania katika kuleta haki, amani, utu na ubinadamu anasema Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Naye Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa niaba ya Maaskofu Katoliki Tanzania amesema, Maaskofu wamefurahia kuwepo Ubalozini hapo na kwamba, hija yao ya kitume ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni msingi za wajibu wao kama Maaskofu. Wamefurahishwa sana kwa ukarimu na mapokezi makubwa. Lengo likiwa ni kufahamiana na kumpongeza Balozi kwa kazi kubwa anayotekeleza kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Tanzania. Amemshukuru kwa kuwapitisha Maaskofu kwenye historia kuhusu mchango wa Sheikh Thabit Kombo Jecha, mtu maarufu sana katika harakati za ukombozi wa Zanzibar. Leo hii kazi hii inaendelezwa na Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Mtoto wa Sheikh Thabit Kombo Jecha, katika mchakato wa ujenzi wa Taifa la Tanzania. Maaskofu wamemwahidi kumweka katika sala na maombi yao, ili aendelee kutekeleza kazi yake vizuri zaidi, ili hatimaye, kumrahishishia Rais kazi zake, ili ziwe nyepesi zaidi na apate hata muda wa mapumziko na kuendelea kuchapa kazi kwa furaha, kumbe, Maaskofu pia wanamtakia Rais Samia Suluhu Hassan heri na baraka tele katika majukumu yake ya kuwaongoza watanzania. Ni furaha kubwa kwa Maaskofu kuona nchi inaendelea, watu wanafurahi na maendeleo yanapatikana na Tanzania kama nchi inazidi kulinda, heshima na tunu zake. Haya ndiyo matamanio halali ya Maaskofu Katoliki Tanzania, ndiyo maana wafanyakazi Serikalini wanajituma bila ya kujibakiza ili watanzania wapate furaha, amani na maendeleo. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga amemwombea Balozi nguvu, ari na moyo wa kutenda yote hayo na kwamba, Maaskofu Katoliki Tanzania wako bega kwa bega kuiendeleza Tanzania.
Askofu Mkuu Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora baada ya sala kwa ajili ya kuombea Ubalozi wa Tanzania nchini Italia amemshukuru na kumpongeza Balozi Mahmoud Thabit Kombo kwa kjitihada zake za kuwaunganisha watanzania wa diaspora, ili waweze kuwa wamoja sanjari na kubadili mtazamo na mwelekeo wa ubalozi, ambao leo hii umekuwa na mvuto kwa watanzania wengi. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ni kiongozi ambaye amejipambanua katika majadiliano ya kidini, kwa kushirikiana na watanzania wenzake kwa hali na mali.