Tafuta

Mama Evaline Malisa Ntenga hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika. Mama Evaline Malisa Ntenga hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika. 

Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais Wanawake Wakatoliki Afrika

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania katika makala hii anapembua kwa kina na mapana juu ya: Siku ya Wanawake Wakatoliki Duniani, Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA, Mkutano na wanawake wa Mashariki ya Kati, Mkutano mkuu wa mwaka 2023 uliofanyika mjini Assisi, Uchaguzi wa Bodi mpya, Uchaguzi mkuu na hitimisho lake.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - WUCWO, Assisi, Italia.

Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania katika makala hii anapembua kwa kina na mapana juu ya: Siku ya Wanawake Wakatoliki Duniani, Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA, Tanzania, Mkutano wa kihistoria na wanawake wa Mashariki ya Kati, Mkutano mkuu wa mwaka 2023 uliofanyika mjini Assisi; Ufunguzi, Semina, Uchaguzi wa Bodi mpya, uchaguzi mkuu na hitimisho lake. UTANGULIZI: Tunapenda kumshukuru Mungu aliyetujalia afya na huruma yake kuweza kuetekeleza yale machache tuliyofanikiwa kutekeleza. Kwa namna ya pekee napenda kumshukuru Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padre Florence Rutaihwa, Kamati tendaji ya WAWATA, Viongozi wote wa majimbo na Wakurugenzi wa majimbo kwa utumishi wenu katika kuwezesha shughuli za Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, “Unión Mundial de las Organizaciones Femeninas Católicas, UMOFC” kufanyika katika kipindi hiki cha taarifa. Kwa kipindi cha 2022/23, shughuli za WUCWO ziliimarika zaidi ukilinganisha na kipindi cha 2021/22. Ni baada ya kudhibitiwa kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 hivyo kuruhusu kuendelea kwa utekelezaji wa vipaumbele vya WUCWO kwa kipindi cha Mwaka 2018/2019 – 2022/23. Pamoja na mikutano ya kawaida, kulikuwa na matukio muhimu kama ifuatavyo:

1.      Mkutano/Warsh ya WWO – World Women Observatory Mei 2022

2.      Jubilei ya WAWATA Septemba 2022

3.      Mkutano wa Bodi Oktoba 2022

4.      Mkutano Mkuu – General Assembly (GA) Mei 2023.

Mkutano mkuu wa wanawake wakatoliki duniani Assisi 2023
Mkutano mkuu wa wanawake wakatoliki duniani Assisi 2023

MKUTANO/WARSHA YA (World Union Observatory) WWO NA SIKU YA WUCWO DUNIANI: Kanda ya Afrika ilifanya warsha ya WWO - Afrika kujiandaa na utafiti wa changamoto ama kilio cha mwanamke wa Afrika kama shughuli kuu kwa mwaka 2022. Maandalizi yalichukua sehemu ya robo ya mwaka 2022 kwa vikao vya mfululizo na mikutano ya zoom hasa kati ya Rais wa WUCWO, Makamu wa Rais wa WUCWO Afrika na mwakilishi wa WUCWO kutoka Kenya kwa kuwa Kenya ndiyo ilikuwa wenyeji. Tanzania ilishiriki warsha hiyo ikiwakilishwa na Mwenyekiti wa WAWATA Taifa Mama Evaline Malisa Ntenga ambae pia ni mjumbe wa Bodi ya WUCWO na Mtunza Hazina WAWATA Mama Gertrude Mtiga. Baada ya Warsha wajumbe wote waliandaa mpango kazi wa kufanya utafiti kwenye nchi zao kwa njia ya DODOSO maalum. Utafiti uliendelea kuanzia mwezi Septemba 2022 hadi mwezi Aprili 2023. Pamoja na kusuasua, lengo la kuwasikiliza wanawake 10,000 na takriban wataalam wabobezi 210 wa masuala ya nyanyaso lilifanikiwa. Tulipata pia fursa ya kusherehekea siku ya WUCWO duniani tarehe 14 Mei 2022 iliyofanyika sambamba na warsha ya WWO katika Kanisa kuu la Ngong Parokia ya Yosefu Mfanyakazi. Tukio hili kubwa la Kimataifa lilikuwa na wawakilishi kutoka Bara la Afrika wakiongozwa na Rais wa WUCWO Bi Maria Lia Zervino Servidora, huku Kenya ikiwa na wawakilishi kutoka majimbo yake yote. WUCWO WASHIRIKI JUBILEI YA MIAKA 50 YA WAWATA: Mnamo mwezi Septemba 2022, Bi Winnie Muthinga ambae ni mjumbe wa Bodi ya WUCWO akiwakilisha Kenya akiambatana na Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kenya (CWA) Bi Anastacia Musyimi, walimwakilisha Rais wa WUCWO pamoja na makamu wa Rais kwa Bara la Afrika kwenye kilele cha Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA, Tanzania. WAWATA kwa furaha walipokea salamu za upendo kutoka kwa Rais wa WUCWO Bi Maria Lia na Makamu wake kwa Bara la Afrika Bi Monique Faye kwa pamoja wakiiwapongeza WAWATA kwa Jubilei na kuwasihi kuendeleza ushirikiano uliopo na zaidi kusimamia malezi ya familia kama kanisa dogo la nyumbani.

Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA, Tanzania
Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA, Tanzania

WUCWO WAFANYA MKUTANO WA KIHISTORIA NA WANAWAKE WA MASHARIKI YA KATI SAMBAMBA NA MKUTANO WA BODI HUKO UGIRIKI 5 HADI 7 OKTOBA, 2022. Mnamo Mwezi Oktoba 2022, wajumbe wa Bodi ya WUCWO pamoja na Wanawake wa Bara la Asia walishiriki kikao cha Bodi ya WUCWO ana kwa ana na kukutana na wanawake wa Mashariki ya Kati na Mediteranea huko Athens nchini Ugiriki. Hiki ni kikao cha pili cha ana kwa ana tangu bodi ianze kazi mwaka 2018. Wajumbe wa bodi walishirikishana uzoefu walioupata kwa kuwepo kwenye bodi na jinsi uanachama wa WUCWO ulivyowasaidia wao na mashirika yao. Ni Dhahiri kwamba kila mjumbe alipata fursa ya kujifunza kutoka kwa nchi nyingine na zaidi ukuaji wa kiroho kwa kushirki sala, tafakari ya neno kupitia makundi sogozi na salamu za kila mwezi kutoka kwa mlezi Pd Marcelo Gidi. Ripoti zilizowasilishwa ni Pamoja na;

1.      Ripoti ya Kazi za vikundi

2.      Ripoti ya Kamati Uchumi

3.      Ripoti za Mabara

4.      Marekebisho ya Katiba

5.      Mandalizi ya Mkutano mkuu wa WUCWO GA 2023

6.      Mapendekezo ya Majina ya Rais wa WUCWO.

Mkutano mkuu wa wanawake wakatoliki duniani Assisi 2023
Mkutano mkuu wa wanawake wakatoliki duniani Assisi 2023

MKUTANO MKUU – GA ASSISI 2023: Mkutano mkuu ulianza kwa hadhira na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Mei 2023 ambayo pia ni siku ya WUCWO duniani ikiwa ni siku kuu ya Bikira Maria wa Fatima ambae ni somo wa WUCWO. Rais wa WUCWO Bi Maria Lia alimkaribisha Baba Mtakatifu akimshukuru kwa namna anavyoshirkiana na WUCWO na kwa namna ya pekee kutenga muda kuwahutubia wanawake Wakatoliki kote ulimwenguni. Zaidi ya waamini 1500 walishiriki. Bi Maria Lia alimweleza Baba Mtakatifu Francisko miradi mbalimbali inayotekelezwa na WUCWO, mradi mkubwa ukiwa ni WWO unaoendelea Afrika. WWO inatarajia kufanya mkutano nchini Tanzania kuanzia tarehe 02/07/2023 hadi 07/07/2023. Mkutano huu utafanyikia Kurasini, kwenye Makao makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC na maandalizi yameanza. Baba Mtakatifu Francisko aliwakaribisha waamini waliokuwepo katika ukumbi wa Mtakatifu Paulo VI na wale ambao walikuwa wanafuatialia moja kwa moja kwa njia ya mtandao na ambao ni sehemu ya umoja huo kutoka sehemu mbalimbali za dunia na familia zao akiwasihi kujikita katika roho ya kikanisa na kuwataka warudi na shauku kubwa ya kuendelea kumtumikia Kristo Yesu katika sehemu wanakotokea. Baba Mtakatifu aliwataka wanawake wote kuelekeza macho mjini Fatima kwa mtangulizi wao Bikira Maria na kuendelea kufanya kazi ya Eva mpya ya kuwahudumia maskini na wale waliosukumizwa pembezoni. Aliwapongeza WUCWO kwa kazi kubwa ya kupaza sauti za wasio na sauti na kuwaleta kwenye nuru wale wanaoteseka bila kupatiwa msaada – ‘Make the invisible woman and man visible’ kupitia Mradi wa WWO.

UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU: Mkutano ulifunguliwa rasmi kwa Misa iliyoongozwa na Monsinyo Lucio A Ruiz, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano Dominika tarehe 14 Mei 2023 katika Basilica la Bikira Maria ikifuatiwa na hafla ya ufunguzi katika hoteli ya Domus Pacis mjini Assisi ambapo Serikali iliwakilishwa na Meya wa Assisi Bi Stefania Profetti huku Kanisa likiwakilishwa na Askofu Domenico Sorrentino wa Jimbo Katoliki la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino. Bi Stefania aliwakaribisha wajumbe wa mkutano na kuwapongeza kwa kazi kubwa ya kutumikia wengine – familia, kanisa, jamii na siasa. Aliwakumbusha wajumbe kuwa wanyenyekevu akinukuu ujumbe wa Mama Theresa wa Calcuta ‘Sisi ni penseli mkononi mwa Mungu, yeye anafikiri, anachora na kuandika, anafanya kila kitu na wakati mwingine sio rahisi kwani penseli hii huvunjika kila mara na ili aendelee lazima aichonge kwanza.” Askofu Domenico Sorrentino kwa upande wake alisema, kwa miaka 17 sasa hajashuhudia mkutano wenye wajumbe wengi kiasi kile. Aliwakabidhi wajumbe wote ufunguo wa Assisi, yaani “Wimbo wa Mtakatifu Francisko, ‘Nifanye chombo cha amani’ kwa kuimba wimbo huo kwa lugha zote za WUCWO -Kiingereza, Kihispania na Kifaransa. Askofu Domico alisoma pia Salamu za Kadinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambae kwa bahati mbaya hakuweza kuhudhuria. Katika salamu za Kadinali Farrel alisema, “Mmechagua Maisha ya Wafransikani kwa kufika Assis, mmechagua Maisha ya UPATANISHO, UDUGU na AMANI sawa na kauli mbiu ya mkutano wenu. Ninawaombea ili muweze kuitikia wito wa Kristo wa kutangaza Injili ambao ni kufanywa upya katika maisha ya kila mmoja, mashirika yenu na kujenga mahusiano kama njia ya kustawisha Kanisa.”

Kardinali Tagle amekazia ushuhuda na umisionari wa wanawake wakatoliki
Kardinali Tagle amekazia ushuhuda na umisionari wa wanawake wakatoliki

MAFUNZO / SEMINA: Kabla ya kuanza kwa mikutano ya kikatiba, wajumbe walipata semina zenye mada zifuatazo: Njia mpya juu ya swala la ushiriki wa Wanawake katika kanisa – Prof. Anne Marie Pelletier. Changamoto za wanawake katika kanisa la kisinodi linalohimiza upatanisho, haki na amani – Sr Anne-Beatrice Faye. Huduma ya wanawake na vijana katika kanisa la kisinodi – Laura Moreno Marroco. Kuongea na kusikiliza kutoka moyoni ili kukuza lugha ya amani – Cristiane Murray. Ingekuwaje kama kanisa lingekuwa kweli mama? – Sr Linda Pocher. UCHAGUZI WA BODI MPYA: Majina ya wagombea wa nafasi ya kuingia kwenye bodi ya WUCWO 2023-2027 yaliwasilishwa na baada ya kura wajumbe wafuatao walichaguliwa: Marie Salome Ngo Bibout Espe Biogngla – Cameroon. 2 Doris Makhubu – Eswatini. 3. Cecilia Asobayire – Ghana. 4. Lucy Joceylin Vokhiwa – Malawi. 5. Theresa Arama Somboro – Mali. 6. Mary Asibi Gonsum – Nigeria 7. Veronica Patricia Elicia Malan Lebona – Afrika ya Kusini. 8. Evaline Malisa Ntenga – Tanzania. 9. Florence Namata Mawejje – Uganda 10. Julieth Rumamurthy – India. 11. Justina Rostiawati – Indonesia. 12. Isabella Eunyong Park – Korea. 13.    Barbala Csehne Vadnai – Hungaria. 14. Susana Fernandez Guisasola – Hispania.15. Maureen Meatcher – Uingereza. 16. Mercedes Padron Prada – Cuba. 17. Maria de Lourdes Espinoza Rosas – Mexico. 18. Maria Gracia de Fleury – Venezuela. 19. Esohe Maria Semota – Marekani. 20. Karen de Souza – Australia. 21. Clarita Adalem – Philipines. 22. Barbara Dowding- Canada 23. Maria Isabel Gimenez Diaz Argentina   24. Titi Kamano – Guinea. 25. Beatrice Tavarez De Souza – Senegal. KAMATI KUU: Monica Santamarina Noriega, Rais kutoka nchini Mexico. Issabela Eunyong Park, Makamu wa Rais kutoka nchini Korea. Lavinia Carrera Roche, Katibu Mku kutoka Hispania/Italia. Maria Gratia, Mtunza Fedha kutoka Hispania. Evaline Malisa Ntenga, Makamu wa Rais – Afrika kutoka, Tanzania Julieth Rumamurthy Makamu wa Rais – Asia kutoka nchini India. Barbala Csehne Vadnai Makam wa Rais – Bara la Ulaya kutoka Hungaria. Maria de Lourdes Espinoz. Makamu wa Rais Amerika kusini Na anatoka   Amerika ya kusini. Barbara Dowding Makamu wa Rais – Amerika kaskazini anatoka nchini Canada.

Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika
Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika

VIPAUMBELE 2023-2027: WUCWO itaendelea kupanua na kuimarisha kazi ya utafiti kuhusu nyanyaso kwa wanawake na watoto na wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii kupitia mradi wa World Women Obsevatory WWO. WUCWO na washirika wake watasimamia yafuatayo: Kuwaleta kwenye mwanga wale wanaopitia kwenye nyanyaso mbalimbali na kupaza sauti kwa niaba yao. Kuwajengea uwezo utakaosaidia kubadilisha Maisha yao. Kushiriki kuandaa sera za kuwajali wanyonge. WUCWO itatetea uhuru wa kidini: Msingi wa njia ya kujenga udugu na kuleta amani sawa na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” namba 279 kama msingi wa haki za binadamu kama sehemu ya utamaduni na heshima ya kila mtu. Hivyo WUCWO itahimiza yafuatayo: Kukuza ufahamu wa baraka zitokananzo na utajiri wa kukaribishana bila kujali tofauti na kuwathamini wengine kama ndugu na dada, watoto wa Mungu mmoja; kukuza ulinzi wa haki pana ya uhuru wa kidini; kufanyia kazi mipango thabiti ya kutobaguana; kukemea ukiukwaji wa uhuru wa kidini au mateso, na; kuhimiza shughuli za kidini na za madhehebu kwa njia za mazungumzo kwa utulivu, kwa utaratibu, na kuishi pamoja kwa amani, kuwekeza kwenye mafungamano ya udugu wa ulimwengu wote. Baa la njaa Ulimwenguni: Wito wa kujali mazingira yetu, nyumba ya wote. Wito wa wa toba na wongofu wa kiikolojia. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” WUCWO itashirikiana na serikali za ulimwengu katka kutafuta suluhisho la baa la njaa na kupigania usawa wa ugawaji wa rasilimali kuhusiana na wanawake na Watoto, kuhimiza uwajibikaji katika matumizi ya vyakula kupunguza upotevu. WUCWO itafanya kazi na serikali pamoja na wahisani kupata uwekezaji kwenye uzalishaji na upatikanaji wa chakula. WUCWO itashiiriki katika kuitikia wito wa Baba Mtakatifu wa wongofu wa mazingira.

Washiriki wa mkutano mkuu wa WUCWO Assisi, 2023
Washiriki wa mkutano mkuu wa WUCWO Assisi, 2023

Tuitikie kwa Imani na kwa upya, safari ya furaha ya upendo ndaniya familia – Umama na Ubaba. Katika kuitikia wito wa Baba Mtakatifu wa kuanza kwa ari mpya safari ya maisha ya upendo ndani ya familia – kauli mbiu ya mkutano wa kumi wa familia ‘Upendo wa familia’ wito na njia ya Maisha ya utakatifu, WUCWO itaandaa na kuwekeza kwenye mikakati itakayosaidia kuwaandaa vijana kutambua wito na furaha ya maisha ya ndoa na ya kuwa mama / baba kama kifungo cha Maisha – kuwasindikiza wanandoa wapya katika hatua mbalimbali za maandalizi ya maisha ya ndoa na kuziimarisha familia kuwa mfano wa maisha ya udugu na kimbilio katika shida na mahangaiko. Kujenga Mustakabali na wahamiaji na wakimbizi: Kuitikia wito wa Baba Mtakatifu Francisko, anaetualika kushiriki ‘kujenga mustakabali wa wahamiaji na wakimbizi’. kupitia ukaribu thabiti unaoonyesha mtazamo wa Mungu juu yao. WUCWO, mashirika yake, wanachama na wawakilishi wao wa kimataifa watashiriki: Kuhimiza vitendo kwa Kanisa: kukaribisha, kulinda, kusindikiza, kukuza na kuunganisha wahamiaji na wakimbizi. Kukuza kujitolea kwa ajili ya wakimbizi, wanaotafuta hifadhi na wahamiaji walio katika mazingira magumu zaidi. Kuweka wazi vifo vinavyotokea wakati wa uhamiaji usio wa kawaida na biashara haramu ya binadamu. Tafuta kutetea na kutafuta njia mbadala kwa sheria zinazohusu kundi la wakimbizi Kuwezesha kila mmoja kushiriki wajibu muhimu wa Kanisa: (Papa Francisko): Kanisa la Kisinodi. Uundaji na ushirikishwaji wa Wanawake. WUCWO na Mashirika yake yatakuza: Malezi na mafunzo ya wanawake ili, kupitia uongofu wa "kiroho, kiakili na kichungaji", kusikiliza, utambuzi, mazungumzo na vitendo, waweze kuchukua nafasi yao katika ujenzi wa kanisa, ili wanaume na wanawake, makuhani na walei, "watembee" pamoja ili kufanya Sinodi na ushiriki wao katika vyombo mbalimbali vya maamuzi katika Kanisa iwezekanavyo. Malezi na ushiriki wa wanawake kuchukua nafasi za uongozi na majukumu, kuanzia ujana wao, katika kutafuta manufaa ya wote, katika nyanja za kijamii, kisiasa na kidini, kuwa wahamasishaji wa utamaduni wa maisha na utunzaji unaokuza amani na udugu wa wote, kufanya kazi, sambamba na wanaume, kubadilisha mawazo ya utamaduni uliopo na kuwa mashahidi wa utakatifu.

Wanawake wakatoliki wajenzi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu
Wanawake wakatoliki wajenzi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu

KUFUNGA MKUTANO: Mkutano ulihitimishwa kwa Misa iliyoongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, katika Kanisa kuu la Bikira Maria mjini Assisi. Katika mahubiri yake, Kardinali Antonio aliwakumbusha waamini kuhusu nafasi ya mwanamke katika kutafuta amani na ujenzi wa dunia ambayo inajali zaidi mapatano, utu, ubinadamu, mshikamano na hivyo kuna umuhimu wa pekee kuwa mkutano huu umefanyikia Assisi. Mtakatifu Francisko wa Assisi ambae anajulikana kwa mafanikio yake ya kiroho katika kufungamana na viumbe wengine aliuishi mshikamano ambao matunda yake ni Amani. Tunaishi katika Ulimwengu ambao vita ni biashara kubwa. Watoto na wanawake wanalia kwa sababu hakuna amani. Yesu aliwahakikishia wanafunzi wake kuwa watateseka sasa, lakini hatawaacha wala kuwapungukia. Ndivyo anavyotuambia hata leo kuwa atakuwa nasi katika utume wetu na mwisho kuna thawabu ya uzima wa milele. Aliwaasa waumini kuepuka kujijengea hofu kwani matokeo yake ni huzuni. Furaha ya kweli iwe ni Yesu pamoja nasi na sio mafanikio tuliyoyapata. Tunapoondoka Assisi maisha yetu yaakisi umisionari wa kweli wa kutafuta upatanisho na amani na kila mtu.

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika.

Wanawake Wakatoliki
24 May 2023, 14:45