Kard.Semeraro:Mtakatifu Rita alipata shahada ya upendo
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mwanamke, mtakatifu, aliyejulikana kwa mateso lakini ambaye bado leo hii, baada ya karne nyingi ni kielelezo cha furaha kwa waamini wote. Ndivyo Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatiu alisema katika kukumbukuka Mtakatifu Rita wa Cascia, anayejulikana duniani kote, anayependwa na ambaye kumbukumbu yake ya kiliturujia inaadhimishwa kila ifikapo tarehe 22 Mei ya kila mwaka. Kardinali Semeraro aliongoza Misa Takatifu katika Madhabahu ikafuatia sala na baraka ya mawaridi.
Katika mahubiri yake, Kardinali Semeraro alieleza alivyojitayarisha kwa ajili ya maadhimisho hayo kwa kuchukua maandishi kutoka Jalada la Kumbukumbu ya maisha ya Mtakatifu huyo (Positio super virtutibus) yaliyochapishwa mnamo mwaka 1897 kwa ajili ya kumtangaza Rita kuwa mtakatifuna ambao ni muhtasari wa historia yake kwa kuanzia na wito kwa nyuki, tangu mwanzo waliopo katika mila ya Rita. “Nyuki, wakiviviringisha vinywani mwao wanatabiri kwamba maneno yake yangekuwa matamu kama asali. Mara baada ya hapo, wimbo unakumbuka jinsi alivyoingia, kwa namna ya kielelezo, hali mbalimbali za maisha ya Kikristo: uchumba, ujane na maisha ya kuwekwa wakfu. Baadaye kuna kumbukumbu ya muujiza wa donda ambao hasa Msalaba uliojibu maombi yake kwa kumpa moja ya miiba ya taji lake, alisema Kardinali Semerao na kwamba Shahidi, mmoja alisema kuwa Rita alipata hamu ya kweli ya kuwa sehemu ya maumivu yale ambayo Yesu alitaka kuteseka kwa ajili ya upendo wetu.
Kadinali Semeraro vile vile alikumbuka maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliyoandika wakati wa kuadhimisha karne ya sita ya kuzaliwa kwa Mtakatifu huyo kwamba “Ishara ya mwiba, zaidi ya mateso ya kimwili ambayo ilimsababishia, ilikuwa katika Mtakatifu Rita kama muhuri wa maumivu yake ya ndani; hata zaidi, hata hivyo, ulikuwa uthibitisho wa kushiriki kwake moja kwa moja katika Mateso ya Kristo”. Na tena aliandik: “Donda linalong’aa kwenye paji la uso wake ni uthibitisho wa ukomavu wake wa Kikristo. Msalabani pamoja na Yesu, kwa namna fulani alihitimu katika upendo huo, ambao tayari alikuwa ameujua na kuuonesha kwa njia ya kishujaa ndani ya kuta za nyumba yake na kushiriki katika matukio ya jiji lake”.