Tafuta

Kila tarehe 28 Mei ni Siku ya Kutokomeza Njaa Duniani. Kila tarehe 28 Mei ni Siku ya Kutokomeza Njaa Duniani.  (ANSA)

Caritas Internationalis:wadau wa kisiasa saidia kutokomeza njaa duniani

Caritas Intenationalis inaalika wadau wa kisiasa kutokomeza utumiaji hovyo wa chakula na kutekeleza suluhisho endelevu la kukomesha njaa duniani.Ni katika Muktadha wa Siku ya Kutokomeza Njaa duniani ifanyikayo kila tarehe 28 Mei ya kila mwaka.“Haikubaliki kwamba katika mjadala wa hadhara ni wenye nguvu tu na wanasayansi wana sauti lakini bila matendo ya dhati.”

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Katika fursa ya Siku ya kutokomeza njaa duniani kwa mwaka 2023 ambayo uadhimishwa kila ifikapo tarehe 28 Mei ya kila mwaka, Caritas Internationalis ina mshikamano na Jumuiya ya kimataifa kusaidia watu ambao wanakabiliana kipindi cha umaskini na njaa isiyo isha. Kwa hiyo Caritas Internationalisi inabanisha kuwa ili kumaliza njaa kwa njia endelevu, tunahitaji kukuza kilimo endelevu na uzalishaji wa chakula, kupunguza upotevu wa chakula, na kusaidia mifumo ya chakula nchini. Hatua hizi sio tu zitasaidia kupambana na njaa lakini pia zitasaidia kuhifadhi sayari kwa ajili ya vizazi vijavyo. Mamilioni ya watu hawawezi kupata chakula cha kutosha kutokana na migogoro, athari za janga la COVID-19 na kupanda kwa gharama ya maisha. Upotevu wa chakula mara nyingi ni matokeo ya uzalishaji usio endelevu wa chakula na uwekezaji mdogo katika kilimo. Kwa hiyo katika muktadha huo Caritas Intenationalis inaalika wadau wa kisiasa kutokomeza utumiaji hovyo wa chakula na kutekeleza suluhisho endelevu la kukomesha njaa duniani.

Barani Afrika sehemu kadhaa zinasumbuliwa na hali mbaya aya tabianchi

Papa Francisko, katika waraka wa Fratelli tutti, yaani Wote ni Ndugu anathibitisha: “Haikubaliki kwamba katika mjadala wa hadhara ni wenye nguvu tu na wanasayansi wana sauti, lakini bila matendo ya kweli”. Kwa hiyo katika kuitikia wito huu, Caritas imefanya kazi pamoja na jumuiya mahalia  kutekeleza mbinu endelevu za kilimo, kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuunga mkono viongozi wa dunia na watoa maamuzi kushughulikia na kurekebisha sera zinazozidisha njaa duniani. Barani Afrika na katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali mbaya ya hewa au hali mbaya ya  tabianchi, kama vile ukame na mafuriko, Caritas imehamasisha jamii mahalia kuhamasisha umma kuhusu njaa na usalama wa chakula na kukabiliana na majanga ya kibinadamu na dharura. Nchini Kenya, Caritas (kupitia mtandao wake wa majimboi) inaendelea kufanya kazi pamoja na jamii zilizo hatarini za Marsabit, kutoa mgao wa dharura wa chakula na maji safi ya kunywa.

Harakati za Caritas katika nchi mbali mbali

Tangu mwaka wa 2018, Caritas Pakistan imekuwa ikikuza mbinu endelevu za kilimo na kutekeleza programu zinazozingatia ustahimilivu wa familia ndogo za wakulima na kuboresha uwezo wao wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na majanga, kudumisha mfumo wa ikolojia na afya ya udongo. Caritas pia iko katika mshikamano na wanawake na watoto ambao wako katika hatari kubwa na njaa. Caritas Somalia inatoa ufadhili kwa ajili ya mipango mbalimbali, kusaidia kazi ya kukabiliana na ukame nchini Somalia, ambayo pia inajumuisha shughuli za elimu kwa wasichana na koo za Kisomali zilizotengwa. Wakati wa Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Bonn (Juni 5-15), Caritas itashiriki zaidi mitazamo juu ya vipengele vinavyohitajika ili kusaidia kukabiliana na njaa duniani wakati wa tukio la kando ya Mkutano huo  litakalofanyika tarehe 8 Juni 2023 lenye kuongozwa na mada “Mitazamo ya watendaji wa kidini na wa ndani juu ya kazi mpya ya pamoja ya kilimo na mifumo ya chakula, ambayo itajumuisha maoni kutoka katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Mfuko wa Hali ya Hewa ya Kijani (GCF), wapatanishi kutoka Kundi la Afrika na Umoja wa Ulaya (EU).

Siku ya kutokomeza njaa duniani 28 Mei ya kila mwaka
29 May 2023, 10:41