Tafuta

Furaha ya Maaskofu inadumu ikiwa kama watanzania wanasoma na kufaulu vizuri; itadumu zaidi ikiwa kama watarejea nyumbani na furaha hii itakuwa ni endelevu na timilifu ikiwa kama wataweka katika matendo hayo waliyojifunza. Furaha ya Maaskofu inadumu ikiwa kama watanzania wanasoma na kufaulu vizuri; itadumu zaidi ikiwa kama watarejea nyumbani na furaha hii itakuwa ni endelevu na timilifu ikiwa kama wataweka katika matendo hayo waliyojifunza. 

Rai Kwa Wanafunzi Wakatoliki Tanzania Wanaosoma Nchini Italia: Rudini Nyumbani

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga alikuwa na ujumbe maalum kwa wanafunzi wakatoliki wanaosoma nchini Italia. Furaha ya Maaskofu inadumu ikiwa kama watanzania wanasoma na kufaulu vizuri; itadumu zaidi ikiwa kama watarejea nyumbani na furaha hii itakuwa ni endelevu na timilifu ikiwa kama wataweka katika matendo hayo waliyojifunza. Pongezi kwa Mama Evaline M. Ntenga kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Wanawake Wakatoliki Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia Dominika 14 Mei hadi tarehe 21 Mei 2023 limekuwa likifanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina” inayofanyika kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican. Hija hii imekamilika hapo tarehe 21 Mei 2023 kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kukutana na Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki wanaoishi nchini Italia na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo, mjini Roma, na ambayo ilitangazwa mbashara na Radio Maria. Nia za Misa hii zilikuwa ni pamoja na kumshukuru Mungu kwa wanafunzi wanaohitimu masomo yao kwa mwaka 2022-2023, kumpongeza Askofu mkuu Protase Rugambwa kwa kumaliza muda wake na hatimaye kuteuliwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora. Ibada ya Sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni iliongozwa na Askofu Flavian Matindi Kassala Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania aliyezungumza umuhimu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu hadi miisho ya dunia, kwa kujitahidi kusoma alama za nyakati, ili kuinjilisha ulimwengu mamboleo kwa tunu msingi za Kikristo. Katika dominika hii pia Kanisa limeadhimisha kwa ngazi ya kiulimwengu, siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika siku hii umenogeshwa na kauli mbiu isemayo “Kuongea kutoka moyoni, ‘kadiri ya ukweli na upendo’” (Efe. 4:15). Ndani ya ujumbe wake huu, Baba Mtakatifu anasisitiza kuzingatia upendo wa kindugu na umuhimu wa kukuza msamiati wa amani katika tasnia ya habari na mawasiliano kati yetu. Upendo wa kindugu ndio msingi wa kutoa Habari Njema zinazojenga na msamiati wa amani, anaongeza Baba Mtakatifu, hukuzwa pale ambapo tutaondoa fikra za malumbano na ugomvi ndani mwetu.

Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni tarehe 21 Mei 2023
Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni tarehe 21 Mei 2023

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limewazawadia watanzania wakatoliki wanaoishi Italia Misale ya Kirumi kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa. Kanisa la Tanzania limegawanyika katika Kanda kuu saba zinazoundwa na Majimbo makuu ya: Dar es Salaam, Tabora, Songea, Arusha, Dodoma, Mwanza na Mbeya. Kanisa la Tanzania limebarikiwa kutoa Kardinali wa kwanza Mwafrika naye ni kwa nafsi ya Kardinali Laurean Rugambwa (12- Julai 1912 – 8 Desemba 1997) na Askofu mkuu wa kwanza Barani Afrika katika nafsi ya Askofu Marko Mihayo wa Jimbo kuu la Tabora aliteuliwa tarehe 21 Juni 1960. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili 1922, Kijijini Butiama, mkoani Mara. Kumbe, watu wa Mungu nchini Tanzania mwaka 2023 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 101 tangu alipozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu J.K. Nyerere, aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999, miaka 24 iliyopita, akiwa na umri wa miaka 77, huko kwenye Hospitali ya St. Thomas, Jijini London, nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu ya Saratani ya Damu. Urithi mkubwa aliowaachia watanzania ni: amani, umoja, upendo na mshikamano wa Kitaifa. Mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa ni Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu unaendelea. Huyu ni mwana siasa mahiri Barani Afrika. Hii ni fursa kwa watu wa Mungu nchini Tanzania kutafakari tena maisha, wito na utume wake kama mwanasiasa, na Baba mwenye harufu ya utakatifu wa maisha, aliyekita maisha yake katika Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kuwa kama dira na mwongozo wa maisha na utume wake kama mwanasiasa ndani na nje ya Tanzania na mwamini mlei kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Kama binadamu, Mwalimu Nyerere alikuwa na mapungufu yake na daima alikimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu.

Watawa wa Mashirika mbalimbali wakiwa pamoja na Maaskofu
Watawa wa Mashirika mbalimbali wakiwa pamoja na Maaskofu

Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, “Unión Mundial de las Organizaciones Femeninas Católicas, UMOFC, ulioanzishwa kunako mwaka 1910, kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 20 Mei 2023 umeadhimisha Mkutano mkuu wa uchaguzi ulionogeshwa na kauli mbiu Wanawake Wakatoliki Wajenzi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu kwa amani ya Ulimwengu. Mkutano ulifunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu Dominika tarehe 14 Mei 2023 huko mjini Assisi, nchini Italia. Kwa kipindi chote hiki wanawake wakatoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wamejadili kuhusu: “Wanawake ndani ya Kanisa.” Huu umekuwa ni muda muafaka wa kupokea taarifa, kuchambua baadhi ya vipengele vya Katiba, ili kuvifanyia marekebisho; Miradi mipya, maazimio, vipaumbele vya kufanyiwa kazi, uchaguzi na hatimaye, hija ya kiroho mjini Assisi. Mkutano huu ni muda wa sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kusikilizana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, kwa namna ya pekee, Jumamosi tarehe 13 Mei 2023 umepata nafasi ya kusherehekea Sikukuu ya Mama Bikira Maria wa Fatima kwa kupata fursa ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika
Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika

Tanzania ambayo imeshiriki mkutano huo imewakilishwa na Padri Florence Rutaihwa, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya kichungaji TEC, Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa na Bi Happiness Mbepera aliewakilisha WAWATA chipukizi. Mama Evaline Malisa Ntenga amechaguliwa kuwa Rais wa Wanawake Wakatoliki Barani Afrika na Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, uongozi huu utakuwepo madarakani kwa muda wa miaka minne, yaani kuanzia mwaka 2023 hadi 2027. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limempongeza Mama Evaline Malisa Ntenga kwa kuliheshimisha Kanisa la Tanzania. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linampongeza na kumshukuru Askofu mkuu Protase Rugambwa kwa utume uliotukuka, kwa weledi na uchapakazi na kwa hakika amekuwa ni kiungo muhimu kati ya Maaskofu na wanafunzi wakatoliki wanaosoma na kuishi nchini Italia. Maaskofu wanamwombea baraka tele na kumkaribisha tena nchini Tanzania kuendeleza utume wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.  

Rai: Wanafunzi someni, malizeni masomo na rudini nyumbani.
Rai: Wanafunzi someni, malizeni masomo na rudini nyumbani.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga alikuwa na ujumbe maalum kwa wanafunzi wakatoliki wanaosoma nchini Italia. Furaha ya Maaskofu inadumu ikiwa kama watanzania wanasoma na kufaulu vizuri; itadumu zaidi ikiwa kama watarejea nyumbani na furaha hii itakuwa ni endelevu na timilifu ikiwa kama wataweka katika matendo hayo waliyojifunza. Kuna wanafunzi wanaosoma, lakini hawamalizi; wanaomaliza masomo yao, lakini hawarudi nyumbani na kuna wale wanaomaliza masomo na kurejea nyumbani Tanzania, lakini wanakuwa ni mzigo mkubwa kwa Kanisa. Maaskofu wanawataka watanzania kusoma kwa juhudi, bidii na maarifa wakitambua dhamana kubwa iliyoko mbele yao, kwani wametumwa na Kanisa na Taifa ili kukidhi mahitaji ya wataalam katika nyanja mbalimbali. Huu ndio uzalendo kwa Kanisa la Taifa ili kujitosheleza kwa wataalam.

Maaskofu Tanzania
22 May 2023, 15:50