Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi Balozi mpya wa Vatican Nchini Jamhuri ya Watu wa Dominican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi, kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Watu wa Dominican na Mwakilishi wa Kitume nchini Porto Ricco na kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Piergiorgio Bertoldi alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Msumbiji na amewahi pia kuwa Balozi wa Vatican nchini Burkina Faso na Niger. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Bertoldi alizaliwa huko Varese, Jimbo kuu la Milano, hapo tarehe 26 Julai 1963. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikuhani, akapewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 11 Juni 1988. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 24 Aprili 2015 akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Burkina Faso na Niger na kuwekwa wakfu tarehe 2 Juni 2015 na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.
Tarehe 19 Machi 2019 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Msumbiji! Na tarehe 18 Mei 2023 Papa Francisko akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican kwenye Jamhuri ya Watu wa Dominican na Mwalikishi wa Kitume nchini Porto Ricco. Historia ya maisha yake inaonesha kwamba, baada ya Daraja Takatifu ya Upadre, alijiendeleza na hatimaye akapata Shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Tarehe Mosi, Julai 1995 akaanza utume wa kidiplomasia na amewahi kutekeleza dhamana hii kwa mara ya kwanza kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Uganda, Jamhuri ya Congo, Colombia, Yugoslavia ya zamani, Romania, Iran na Brazil.