Siku ya 60 ya Kuombea Miito: Ushuhuda wa Shemasi Renovatus Edward Mugisha
Na Frt. Renovatus Edward Mugisha, - Vatican.
Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu daima wakijitahidi kumfuata Kristo Yesu, Mchungaji mwema! Maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: “Wito: Neema na Utume.” Huu ni mwaliko wa kutafakari kwamba, watu wameumbwa, kwa upendo, kwa ajili ya upendo na kwa upendo. Mimi ni utume katika dunia hii, hiyo ndiyo sababu ya kuwepo kwangu mimi katika ulimwengu, kuwa pamoja na wengine na kwa ajili ya wengine. Tunaitwa kuwa wamoja ili kuunda jumuiya ya wamisionari mitume kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia upendo kwa ajili ya wengine kwa kutambua kwamba, neema na utume ni zawadi na dhamana. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2023, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwakilishi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 29 Aprili 2023 anatoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Mashemasi 28 kutoka sehemu mbalimbali za dunia, Kati yao kuna Frt. Renovatus Edward Mugisha anayesimulia kwa ufupi historia ya maisha yake, changamoto katika maisha na wito wake na hatimaye, shukrani kwa wale wote waliomwezesha kwa hali na mali kufikia hatua hii kama sehemu ya wito wake!
Ninaitwa Frt. Renovatus Edward Mugisha, ni mseminari kutoka Jimbo Katoliki la Kayanga, Parokia ya Bugene, kwa sasa naendelea na masomo ya Sheria za Kanisa (Shahada ya uzamili) katika Chuo Kikuu cha Kipapa (Urbaniana) mjini Roma-Italia na natarajia kupewa Daraja Takatifu ya Ushemasi tarehe 29.04.2023 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa mkesha wa Dominika ya Kristo Mchungaji mwema sanjari na Siku ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2023. Mimi ni mtoto wa tano na wa mwisho wa Ta Edward Kalemba Bernard na Ma. Petronilla Kagemuro. Nilizaliwa tarehe 13 Januari 1991 huko Karagwe, Kagera-Tanzania. Nilipokuwa mdogo nilitamani sana kuwa daktari, hivyo nilipoanza sekondari nilipendelea sana masomo ya sayansi. Kwa kuwa nilisoma shule ya serikali (kidato cha kwanza hadi cha nne), baada ya kuhitimu nilitamani kwenda kujiunga na shule binafsi hasa seminari ili niyafaidi malezi na maarifa yanatolewa na shule za Kanisa. Wazazi walinisadia kuongea na aliyekuwa Mkurugenzi wa miito wa Jimbo la Kayanga Padre Fortunatus Bijura ili anisaidie kunitafutia seminari inayofundisha masomo ya sayansi. Nilifanikiwa kupata nafasi katika Seminari ndogo ya Bikira Maria, Nyegezi Jimbo kuu la Mwanza, japo ilibidi nibalidi mchepuo badala ya kuchukua PCB niliamua kuhamia PCM kwa sababu Bioyolojia ilikuwa haifundishwi pale Nyegezi. Nikiwa naendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, kuna mambo yalianza kunivutia, moja ya jambo lililonigusa sana ni huruma na upendo wa Mapadre walezi kwetu hasa pale mseminari alipokuwa anapitia kipindi kigumu na changamoto za maisha kama: magonjwa, kufiwa nk. Kitu kingine kilichonivutia zaidi ni mavazi yanayovaliwa na Mapadre wakati wa adhimisho la Misa Takatifu, kipindi kile nilikuwa sijazoea kuwaona Mapadre mara kwa mara au kila siku halafu wakiwa zaidi ya mmoja, hivyo kwangu ilikuwa ni furaha kuwaona kila siku asubuhi wakati wa adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, wakiwa wameizunguka Altare ya Bwana kwa Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, kielelezo cha umoja na ushirika wa watu wa Mungu.
Pole pole nilianza kujiuliza mwenyewe kama na mimi nastahili kuwa mmoja wa wale Mababa. Hapo ndipo nilipoanza kufuatilia na kutaka kujua zaidi ni vigezo gani anavyopaswa kuwa navyo kijana anayetaka kuwa kama wao. Hii ilinisukuma nianze kwenda kwa aliyekuwa Baba mlezi wa maisha ya kiroho wa Seminari na kumuuliza sifa kuu za Padre. Katika majibu niliyoyapata, mawili nayakumbuka hadi leo. Kwanza, alinambia Upadre hautafutwi wala kusomewa ila ni wito na zawadi tu na Mungu anampatia yule aliyemchagua na jibu la pili alisema ni kwa njia ya sala na kwa mazungumzo ya mara kwa mara na baba wa maisha ya kiroho ndiyo pole pole mtu anatambua kuwa ameitwa. Baada ya kuhitimu kidato cha sita nilienda kuongea na wazazi, nikawajulisha kuwa natamani kuwa Padre, ingawa sikuwa na uhakika kama kweli ni sauti ya Mungu au ni mimi nilikuwa ninajiita tu! Walinitia moyo, nikaenda nao kuongea na Paroko wangu na badae Mkurugenzi wa miito na baada ya kufuata taratibu zote nikaenda kuungana na wenzangu waliokuwa tayari wamekwenda nyumba ya malezi ya jimbo. Mwaka 2014 nilichaguliwa kujiunga na masomo ya falsafa katika seminari kuu ya Bikira Maria Malkia wa Mitume Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Mwaka 2017, nilihitimu masomo ya falsafa na mwaka 2018 nilitumwa kuja kuanza masomo ya Taalimungu na Askofu wangu Mhashamu Almachius Vincent Rweyongeza) baada ya kupewa ufadhili na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu (Propaganda Fide) katika chuo cha Papa Urbano wa VIII. Mwaka 2021, nilihitimu masomo ya Taalimungu na nikapewa nafasi nyingine ya kuendelea na shahada ya uzamili katika Sheria za Kanisa.
Changamoto katika wito: Changamoto kubwa iliyonisumbua ilikuwa ni kifo cha ghafla cha Mama mzazi Ma. Petronilla Kagemuro kilichotokea tarehe 04.08.2016 kwa ajali ya gari barabarani. Nilikuwa mwaka wa pili wa falsafa, ni tukio ambalo sikulitegemea wala sikuwaza kama lingetokea kabla ya mimi kuwa Padre. Lilinipa msongo wa mawazo ila lilinisaidia pia kuiona thamani na nguvu ya sala na imani. Changamoto ya pili ni kipindi nilipofika nchini Italia 2018 kuanza masomo ya Taalimungu. Ile hali ya kuanza kijifunza lugha mpya kuanzia majina ya herufi, namna ya kuhesabu nk kama watoto wa shule za awali ilininyenyekesha sana, lakini pia ilibidi niwe mvumilivu kuanza kuzoa vyakula, hali ya hewa na kujifunza kuishi na watu wenye tamaduni tofauti na wa kwangu. Changamoto nyingine ni ile hali ya kibinadamu ya kuwa na wasi wasi kama kweli huu ni wito wangu. Lakini kwa njia ya sala, imani na matumaini makubwa, changamoto zote hizi, hatua kwa hatua zilipita na hivyo kuniongezea ukomavu na imani. Shukrani: Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote anayonitendea katika maisha yangu hasa kwa zawadi na wito huu mtakatifu. Napenda kuwashukuru wazazi wangu kwa kuendelea kunisindikiza kwa sala na kwa kuendelea kuwa Makatekista wangu wakuu. Shukrani zangu za dhati zimwendee Askofu wangu Mhashamu Alamchius Vincent Rweyongeza, kwa upendo wake wa kibaba kwangu, kwa kuendeleza kunitegemeza na zaidi ya yote kwa kuniamini na kunituma kusoma huku ughaibuni. Shukrani zangu za pekee kwa uongozi wote uliopita na wa sasa wa Baraza la kipapa la Uinjilishaji wa watu kwa ufadhili wao na kwa nafasi waliyonipatia kuwa mmoja wa wanafamilia kubwa ya chuo cha Papa Urbano VIII. Napenda kuwashukuru Mapadre wa Jimbo la Kayanga, Mapadre walionifundisha seminari ndogo na kubwa, watawa na walezi ambao nimepita katika mikono yao kwa mchango wao kwangu. Napenda kuwashukuru sana waamini wa Parokia yangu ya Bugene na waamini wote wa Jimbo la Kayanga kwa kuendelea kuhifadhili miito kwa njia ya sala na michango yao. Kwa namna ya pekee nawapenda kuishukuru jumuiya ya watanzania wanaoishi Italia na hasa watanzania wanaoishi hapa Roma, mnanifanya niione Tanzania ndani ya Ulaya. Mwisho, natambua na kuthamini mchango wa kila aliyekuwa sehemu ya wote walionisaidia kuifikia siku ya leo, siwezi kuwataja kwa majina ila nawakumbuka katika sala. Naomba muuendele kuniombea ili hicho ambacho Mwenyezi Mungu amepanda ndani mwangu kiendelee kukua na kukomaa.