Tafuta

Maadhimisho ya Sinodi katika ngazi ya Mabara kimekuwa ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa umoja na mafungamano ya kijamii na kikanisa. Maadhimisho ya Sinodi katika ngazi ya Mabara kimekuwa ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa umoja na mafungamano ya kijamii na kikanisa. 

Mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi Kimabara: Umoja, Ushiriki na Mafungamano ya Kikanisa

Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inasema, kipindi chote cha maadhimisho ya Sinodi katika ngazi ya Mabara kimekuwa ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa umoja na mafungamano ya kijamii na kikanisa; kwa kusikilizana, kujadiliana, tayari kufanya mang’amuzi ya pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Maadhimisho haya ni sehemu muhimu ya utengenezaji wa Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu kuanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2024. Awamu ya kwanza ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki yalianza kutimua vumbi tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi 15 Agosti 2022. Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi yalianza Mwezi Septemba 2022 hadi tarehe 31Machi 2023. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wote wa Mungu kujizatiti kikamilifu ili waweze kuwa ni wajenzi wa sanaa ya watu kukutana. Huu ni muda muafaka wa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu. Ni wakati wa kukoleza utamaduni wa Sala, Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa kwa nyakati hizi. Baba Mtakatifu anasema, huu ni wakati wa kukutana na kutajirishana kutokana na karama, miito na utume ambao watoto wa Kanisa wamekirimiwa kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni makutano yanayohitaji ukweli na uwazi, ujasiri na uwepo ili kukutana na wengine. Huu ni mwelekeo mpya unaowataka waamini kutoka katika: uchoyo, ubinafsi na mazoea yao, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu ambaye yuko na anatembea pamoja nao katika ukweli na uwazi!

Maadhimisho ya Sinodi, ujenzi wa umoja, ushiriki na utume
Maadhimisho ya Sinodi, ujenzi wa umoja, ushiriki na utume

Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inasema, kipindi chote hiki kimekuwa ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa umoja na mafungamano ya kijamii na kikanisa; kwa kusikilizana, kujadiliana, tayari kufanya mang’amuzi ya pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Majadiliano haya ni msingi wa maandalizi ya Hati ya Kutendea Kazi, maarufu kama “Hati ya Kutendea Kazi”: “Instrumentum laboris, tayari kuendelea kutembea kwa pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Katika Awamu ya Pili, Ngazi ya Kimabara, imesimikwa katika kanuni ya auni, kwa kufanya rejea kwa mambo msingi yaliyobainishwa; kwa kuonesha kinzani pamoja na vipaumbele vya Makanisa mahalia kadiri ya hali na mazingira yao, ili hatimaye, kuandaa “Hati ya Kutendea Kazi”: “Instrumentum laboris, itakayotumika wakati wa Kikao cha Sinodi kuanzia tarehe 4-29 Oktoba 2023.

Sinodi ya Maaskofu 2023-Oktoba 2024
Sinodi ya Maaskofu 2023-Oktoba 2024

Hati hii kwa sasa inafanyiwa kazi na Kamati ya Maandalizi ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika Awamu ya Pili Kimabara, imekuwa ni kipindi cha neema na baraka kwa Mama Kanisa, sehemu muhimu sana ya ujenzi wa umoja, ushiriki na utume wa Kanisa. Licha ya changamoto, magumu na mapungufu yaliyojitokeza, lakini imekuwa ni fursa ya ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana, kujadiliana na kufanya mang’amuzi ya pamoja kama Kanisa. Majadiliano ya maisha ya kiroho kimekuwa ni chombo adhimu katika ujenzi wa mazingira ya kusikilizana na kufanya mang’amuzi ya pamoja kwa ajili ya Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Awamu ya Pili Kimabara yamebainisha umuhimu kwa watu wa Mungu kufanya kazi katika umoja, ushiriki na utume tayari kuimarisha mchakato wa majadiliano kati ya Makanisa mahalia na Kanisa la kiulimwengu. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inasema, mchakato wa majadiliano ndani ya Kanisa unaendelea kwa kasi nzuri, tayari kumwilisha vipaumbele vilivyobainishwa na Makanisa mahalia mintarafu hali halisi ya maisha na utume wao, kwa kuzingatia pia mang’amuzi ya Kanisa la kiulimwengu na Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium.”

Mchakato wa Sinodi

 

18 April 2023, 16:14