Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025: Maandalizi Yaanza Kutimua Mavumbi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jubilei ya Mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na patashika nguo kuchanika kutokana na vita inayoendelea kupiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote.
Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin tarehe 19 Aprili 2023 ameongoza jopo la viongozi waandamizi kutoka Vatican ili kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Italia, waliokuwa chini ya Waziri mkuu Giorgia Meloni, kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mazungumzo haya yamedumu takribani kwa muda wa saa moja. Viongozi wa pande zote mbili wameridhishwa na mafungamano pamoja ushirikiano ulipo kama nyenzo muhimu katika maandalizi na hatimaye maadhimisho yote. Hili ni tukio ambalo linapania pamoja na mambo mengine kupyaisha maisha ya kiroho, kitamaduni na kiuchumi kwa ajili ya mji wa Roma na Italia katika ujumla wake. Wameonesha nia ya kutaka kukutana ili kubadilishana mawazo, uzoefu na mang’amuzi mbalimbali katika maisha. Kumbe kuna haja ya kuwa na mifumo, sheria, kanuni na taratibu kwa ajili ya mahujaji pamoja na waamini, kama sehemu ya mchakato wa maaadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 tayati kutangaza na kushuhudia imani, matumaini na mapendo.
Ni jukumu la Mama Kanisa kuendelea kujikita katika Mapokeo, sera na mikakati ya shughuli za kiuchungaji. Mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, ili wote wawe na umoja kama Kristo Yesu alivyojisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa ya maandalizi ya Mwaka wa kwanza wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.”