Tafuta

Mtakatifu Faustina Kowalska  na  Picha ya Yesu na Huruma ya Mungu. Mtakatifu Faustina Kowalska na Picha ya Yesu na Huruma ya Mungu. 

Historia ya Ibada ya Huruma ya Mungu:Yesu ninakutumainia

Sr.Faustina anaandika kuwa“Jioni,nikiwa nimesimama kwenye chumba changu, nilimwona Bwana akiwa amevaa vazi jeupe.Baada ya papo hapo Yesu aliniambia: “Chora picha kulingana na mfano unaouona,kwa maandishi hapa chini”:“Yesu ninakutumaini Wewe!Ninataka picha hii iheshimiwe kwanza katika kanisa lako,na ulimwenguni kote.

Na Angella Rwezaula,-Vatican.

Ninapenda kuanza na kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ananiwezesha kuandika kwa ufupi historia ya ibada ya Huruma ya Mungu. Ninaweza kusema kuwa ni neema ya mwaka huu 2023 katika fursa ya Siku Kuu ya Huruma ya Mungu, iliyopita ambapo kupitia makala tulizoandikwa, walitokea baadhi ya vijana ambao walitaka kujua zaidi kuhusu siku hii, kwa sababu ya kuchanganya kati ya Ibada ya Roho Mtakatifu, au Mama Maria Mwenye huruma na mengine. Katika muktadha huu ninakuandikia wewe ili kujua asili ya ibada hiyo ya huruma, kinyume na mawazo uliyo kuwa nayo, kwa matumaini ya kukukidhi haja ya kiu yako. Katika Ibada hii ya Huruma ya Mungu yote yalianzia mnamo tarehe 12 Februari 1931 katika nyumba ya watawa ya Plock huko Poland, ambapo Sista Faustina (mtawa ambaye baadaye alikuja kuwa mtakatifu, na mtume aliyechaguliwa na Bwana kutangaza ibada ya Huruma ya Kimungu), alipomwona Bwana ndani ya chumba chake.

Sanamu ya Mtakatifu Faustina Kowalska
Sanamu ya Mtakatifu Faustina Kowalska

Sr. Faustina anaandika kuwa “Jioni, nikiwa nimesimama kwenye chumba changu, nilimwona Bwana akiwa amevaa vazi jeupe. Baada ya papo hapo Yesu aliniambia: “Chora picha kulingana na mfano unaouona, kwa maandishi hapa chini”: “Yesu ninakutumaini Wewe! Ninataka picha hii iheshimiwe kwanza katika kanisa lako, na kisha ulimwenguni kote. Ninaahidi kwamba nafsi ambayo itaheshimu picha hii haitaangamia. Pia ninaahidi tayari kwenye dunia hii, lakini hasa saa ya kifo, ushindi juu ya maadui. Mimi mwenyewe nitailinda kama utukufu wangu mwenyewe.” (47).

Baba Mtakatifu akiwa anasali kwenye madhabau ya huruma ya Mungu
Baba Mtakatifu akiwa anasali kwenye madhabau ya huruma ya Mungu

Muungamishi, ambaye mtawa huyo alimweleza jambo hilo la kuvutia, kwa wazi alionesha kutoridhishwa kwake kwa kufasiri maneno haya katika maana ya picha  itakayotiwa chapa kwenye nafsi. Lakini wakati Sr. Faustina alipoondoka kwenye maungamo sauti ya Yesu ilirudi na kwa hakika ikaanza kupendekeza ibada kuwa: “Picha  yangu tayari ipo ndani ya nafsi yako. Ninataka kuwe na Sikukuu ya  Huruma. Ninataka picha unayochora kwa brashi ibarikiwe sana Dominika ya pili ya Pasaka; Dominika hii lazima iwe Sikukuu ya Huruma. Ninataka makuhani watangaze Huruma yangu kuu kwa roho za wenye dhambi. Mwenye dhambi asiogope kunikaribia.” Miali ya Huruma yanila; Ninataka kuzimimina juu ya nafsi za watu” (49-50).

Katika mwaka wa 1934 Yesu alirudi na kusema: “Ninapenda picha hii ionekane wazi kwa umma Dominika ya kwanza baada ya Pasaka. Dominika hii ni Sikukuu ya Huruma ” (88) "Ninatamani Picha hii ibarikiwe Dominika  ya kwanza baada ya Pasaka na ipate ibada ya hadhara" (341). Wakati huo huo, mchoraji Eugenio Kazimirowski mnamo 1934, baada ya juhudi nyingi, aliweza kuchora picha ya kwanza ya Yesu wa Huruma. Sr. Faustina  hata hivyo alikatishwa tamaa sana na kazi ya mchoraji huyo na akajiachia akilia ipasavyo na kumwambia Bwana: “Ni nani awezaye kukuchora uzuri  kama wewe?” Lakini Yesu akamwambia: “Ukuu wa Sura hii haupo katika uzuri wa rangi au picha, bali ni katika Neema Yangu” (313).

Padre Michele Sopocko, mkurugenzi wa kiroho wa Sr. Faustina, aliposikia shauku ya Yesu, aliomba na kupata kibali kutoka mamlaka ya kikanisa ili kuonesha kwa dhati picha  hiyo. Ilikuwa mnamo tarehe 28 Aprili 1935, katika  Domenica in  Albis, yaani Dominika ya Pili baada ya Pasaka  aambayo leo hii  tunaweza kusema kwamba ndiyo ilikuwa  sikukuu ya kwanza ya Huruma  iliyopoadhimishwa kwa dhati.  Na ikumbukwe kwamba Jubilei ya Ukombozi pia ilikuwa inahitimishwa siku hiyo. Bila kutarajia Sr.  Faustina alisikia sauti ikisema:“Sikukuu hii imetoka katika matumbo ya Huruma  yangu na imethibitishwa katika kina cha  neema zangu. Kila nafsi inayoamini na kutegemea huruma yangu itaipata”(420).

Ndugu Msomaji wa makala hii, ikumbukwe kwamba, ibada ya Huruma ya Mungu inafungamana kwa karibu sana na Ekaristi, katika adhimisho la kiliturujia na katika udhihirisho wa Sakramenti Takatifu. Tunapaswa kukumbuka kwamba Sr Faustina anaitwa ‘wa Sakramenti Takatifu’ na kwamba mara nyingi alikuwa na uzoefu wa ajabu wa kina wakati wa Kuabudu. Hata baadhi ya mazoea ya ibada yamethibitishwa kwa ajili ya kumbukumbu na muungano wa sadaka ya Ekaristi (kwa mfano  rosari). Mbele zaidi ya hayo Yesu anarejeea ibada hiyo kuwa: “Binti yangu, ikiwa ninataka kutoka kwa watu kwa ajili yako ibada ya Huruma  yangu, lazima uwe wa kwanza kujipambanua kwa imani yako katika huruma yangu”… (742).

Katika mchakato wa safari ya kielimu inayokua, Yesu alipendekeza ibada ambayo sala, neno na vitendo vinaunganishwa bila usawa, na kwa hivyo ibada inayohama kutoka katika sherehe hadi uzima na kutoka katika maisha na kurudi kwenye maadhimisho: kuomba na kufanya kazi ya upendo katika umoja wa kina ni amri kuu ya Upendo, kwa Mungu na kwa jirani. Yesu aliendelea kusema: “Kwa mtindo huu roho hutukuza na kuabudu huruma yangu. Ndiyo, Dominika ya kwanza baada ya Pasaka ni Sikukuu ya Huruma, lakini lazima pia kuwe na matendo na ninadai ibada ya Huruma yangu pamoja na sherehe kuu ya Sikukuu hii na kwa ibada ya Picha ambayo imechorwa. Kupitia picha hii nitatoa neema nyingi kwa roho, lazima ikumbuke matakwa ya Huruma yangu, kwasababu hata imani yenye nguvu ni bure bila matendo’ (742).

Leo, hii harakati ya   kitume ya Huruma ya Mungu inawaleta pamoja mamilioni ya watu kutoka duniani kote katika kanisa: Mashirika ya kitawa, taasisi za kiulimwengu, mapadre, washirika wa udugu, vyama, jumuiya mbalimbali za mitume wa Huruma ya Mungu na watu binafsi wanaofanya kazi ambazo Bwana kupitia kwa Sista Maria Faustina aliwatuma. Utume wa Sr. Maria Faustina ulielezwa katika Shajara lake ambalo aliandika kufuatia na shauku ya Yesu na mapendekezo ya mapadre waungamishaji akizingatia kwa uaminifu maneno yote ya Yesu na kufunua yaliyomo ndani ya nafsi yake pamoja Naye. Katika maandishi yake, Bwana alimwambia Faustina kuwa: "Katibu wa huduma yangu ya kina kabisa ... kazi yako kubwa ni kuandika kila kitu ninachokujulisha kuhusu Huruma yangu, kwa manufaa ya nafsi ambazo, kwa kusoma maandiko haya, zitapata faraja ya ndani na itakuwa ni kichocheo cha kuhimizwa kunikaribia” (1693).

Kwa hiyo mdogu msomaji  Mama Kanisa, kila Dominika ya Pili ya Kipindi cha Pasaka ainaadhimisha Sherehe ya Huruma ya Mungu, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992. Kulingana na asii hiyo maadhimisho hayo yamekuwa na umuhimu wa kipekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa sababu daima  ni wazi kuonesha uhusiano wa karibu kati ya Fumbo la Ukombozi na Sherehe ya Huruma ya Mungu ambayo imetokana wazi na Fumbo la Msalaba, kifo na ufufuko wake. Tumshukuru Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye kwa njia ya ushuhuda wa utume na maisha yake, aliwezesha  kuwafunulia watu, huruma na upendo wa Mungu, kama Kristo Yesu alivyomfunulia Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma, na ambaye baadaye alimtangaza kuwa  Mtakatifu mnamo tarehe 30 Aprili 2000 katika Jubilei.

Baba Mtakatifu Francisko mnamo tarehe 8 Desemba 2015 alichapisha Waraka kwa ajili ya maadhimisho ya mwaka wa Huruma ya Mungu, ujulikanao kwa lugha ya Kilatini Misericordiae vultus, yaani Uso wa Huruma au Sura ya Huruma. Katika Waraka huo Baba Mtakatifu anaendele anatoa mwaliko kwa wote kutafakari daima huruma ya Mungu. Ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani. “Wokovu wetu unategemea huruma ya Mungu kwani huruma ni neno linalodhihirisha fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma ni tendo la mwisho na la juu kabisa ambalo kwalo Mungu anakuja kukutana nasi. Huruma ni sheria-msingi iliyomo katika moyo wa kila mtu anayewatazama kwa wema binadamu wenzake anaokutana nao katika mapito ya maisha. Huruma: ni daraja inayomuunganisha Mungu na mwanadamu na inaelekeza mioyo yetu kwenye tumaini la kupendwa daima licha ya udhambi wetu”.

Papa anabainisha kuwa tunaalikwa kuitazama huruma kwa umakini zaidi, ili tuweze kuwa alama wazi za matendo ya Mungu katika maisha yetu. Ni kwa sababu hii, Papa alisema  aliamua kutangaza Jubilei ya pekee ya Huruma, kama nafasi ya pekee kwa Kanisa; wakati ambamo ushuhuda wa waamini unaweza kukua na kuimarika zaidi. Baba Mtakatifu katika waraka huo   wa Huruma ya Mungu, anasisitiza kutamkabidhi Kristo Yesu maisha ya Kanisa, wanadamu wote na ulimwengu mzima kwa ujumla. Alikuwa akitoa mwaliko wa kuomba  Kristo atumiminie wingi wa huruma yake kama umande wa asubuhi ili sote kwa pamoja tujenge kesho iliyo angavu zaidi”.  Tamanio lake Papa lilikuwa kwamba mwaka huo uweze kuzamishwa katika huruma ili tuweze kutoka kuwaendea binadamu wote na kuwapelekea habari njema na upendo wa Mungu. Mwangwi wa huruma umfikie kila mmoja; wote wanaoamini na wale walio mbali, kama alama ya kwamba Ufalme wa Mungu upo tayari kati yetu.

Na hiyo ni kwa sababu Mungu alijidhihirisha ukuu wake kwa njia ya huruma yake, kama anavyotufundisha Mtakatifu Tomaso wa Akwino, kwa kusema kwamba huruma sio alama ya udhaifu, bali ni alama ya ujasiri na ukuu.  Tukielekeza macho yetu kwa Yesu na tazama yake ya huruma, tunaona upendo wa utatu Mtakatifu. Utume wa Yesu  alioupokea kutoka kwa Baba, ulikuwa ni kulidhihirisha fumbo la upendo huu  katika ukamilifu wote. Baba Mtakatifu alisitiza kwamba Mungu ni upendo ambao umedhihirishwa  kwa wazi zaidi na unagusa katika maisha mazima ya Yesu. Nafsi yake ni Upendo unaofafanuliwa katika huruma yake kuu. Ishara anazotenda, kwa namna ya pekee kwa wadhambi, masikini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wagonjwa, wanaoteseka, katika hayo yote alilenga kutufundisha huruma. Kila kitu ndani mwake kinaongelea huruma. Baba Mtakatifu alisema Jubilei ya Huruma ya Mungu iwe ya kutafakarisha kuanzia “ sisi wenyewe kila mmoja wetu jinsi alivyoweza kupokea huruma ya Mungu katika maisha. Hata kama umesahau, ipo siku uliguswa na huruma ya Mungu na ikakuinua na kukufariji sana. Tunaendelea kuishi na kufanya kazi, sio kwa sababu ya mastahili yetu, bali kwa sababu tu ya Huruma ya Mungu.

Na katika mahubiri yake ya ufunguzi wa Jubileio ya huruma, Baba Mtakatifu alikuwa amesema kwamba Mwaka huu wa maalum pia ni zawadi ya neema. Kuingia kupitia Mlango huo kunamaanisha kugundua undani wa huruma ya Baba ambaye anakaribisha kila mtu na kwenda nje kukutana na kila mtu kibinafsi. Anatutafuta! Yeye ndiye anayekuja kukutana nasi! Utakuwa mwaka wa kukua katika imani ya rehema. Ni makosa kiasi gani yanafanywa kwa Mungu na kwa neema yake wakati mtu anapothibitisha juu ya dhambi zote zinaadhibiwa kwa hukumu yake, bila kuweka mbele badala yake kwamba zimesamehewa kwa rehema yake(Augustine, De praedestinational sanctorum 12, 24)! Ndiyo hiyo ni sahihi. Ni lazima tuweke rehema mbele ya hukumu, na kwa vyovyote vile hukumu ya Mungu itakuwa katika nuru ya rehema yake sikuzote.

Baba Mtakatifu alibainisha kwamba kuvuka Mlango Mtakatifu, kwa hiyo, hutufanya tujisikie sehemu ya fumbo hili la upendo, la huruma. Tunaacha aina zote za hofu na hofu, kwa sababu haifai mpendwa; badala yake, tunaishi furaha ya kukutana na neema ambayo inabadilisha kila kitu. Mkutano uliodhihirishwa na nguvu za Roho ambaye alilisukuma Kanisa lake kuibuka kutoka kwenye kina kirefu ambacho kwa miaka mingi kilikuwa kimejifunga ndani yake, ili kuanza tena safari yake ya umisionari kwa shauku. Ilikuwa ni kuanza tena kwa safari ya kukutana na kila mtu pale anapoishi: katika mji wake, nyumbani kwake, mahali pake pa kazi... popote pale alipo mtu, hapo Kanisa linaitwa kumfikia ili kuleta furaha ya Injili na kuleta rehema na msamaha wa Mungu. Msukumo wa kimishonari, kwa hiyo, kwamba baada ya miongo hii tunachukua tena kwa nguvu ile ile na shauku ileile. Maadhimisho ya Jubilei yanatupa changamoto kwa uwazi huu na inatuwajibisha kutopuuza roho iliyojitokeza kutoka kwa Vatican II, ile ya Msamaria, kama Mwenyeheri Paulo VI alivyokumbuka katika hitimisho la Mtaguso. Kuvuka Mlango Mtakatifu leo ​​kunatufanya tuwe na huruma ya Msamaria Mwema.

Papa akiwa anasali
Papa akiwa anasali

Sala ya Jubilei ya huruma ya Mungu

Bwana Yesu Kristo, umetufundisha kuwa watu wenye huruma kama alivyo Baba wa mbinguni, na umetuambia kwamba mtu yeyote anayekuona wewe amemwona Baba. Tuoneshe uso wako nasi tutaokoka. Jicho lako lililosheheni upendo lilimwokoa Zakayo na Mathayo waliokuwa watumwa wa fedha; lilimwokoa mwanamke mzinzi na Magdalena aliyekita furaha yake kwa kiumbe; ulimfanya Petro aangue kilio baada ya usaliti; ukamhakikishia Paradiso, mwizi aliyetubu. Tuwezeshe kila mmoja wetu kusikiliza lile neno ulilomwambia mwanamke Msamaria: Kama ungetambua zawadi ya Mungu! Wewe ni sura inayoonekana ya Baba asiyeonekana; sura ya Mungu anayejifunua kwa uweza, lakini zaidi kwa njia ya msamaha na huruma: liwezeshe Kanisa lako duniani kuwa sura yako inayoonekana; Bwana wake, Mfufuka anayeishi katika utukufu.

Wewe ulipenda kwamba,hata watumishi wako ambao wamevikwa na udhaifu waweze kuwa na huruma ya haki kwa wale wanaoogelea katika ujinga na makosa: tunakuomba basi, kila mtu anayemkaribia kila mmoja wao ajisikie kukaribishwa, kupendwa na kusamehewa na Mungu. Peleka Roho wako Mtakatifu na utuweke sisi wakfu ili Jubilei ya Huruma ya Mungu iwe ni mwaka wa neema ya Bwana na Kanisa ambalo limepyaishwa kwa ari kuu liweze kuwatangazia maskini Habari Njema, kuwahubiria wafungwa na wanaosetwa uhuru na vipofu kuona tena. Tunakuomba haya kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa huruma, Wewe unayeishi na kutawala pamoja na Baba na Roho Mtakatifu, milele na milele. Amina

Asili ya Ibada ya huruma ya Mungu kwa mujibu wa Mtakatifu Faustina
21 April 2023, 14:40