Mama Borjana Krišto, Waziri Mkuu wa Bosnia na Herzegovina Akutana na Papa Francisko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 3 Aprili 2023 amekutana na kuzungumza na Wazi mkuu wa Bosnia na Herzegovina na baadaye, alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo yake na Mama Borjana Krišto, Waziri mkuu wa Bosnia na Herzegovina, kwa pamoja wameridhishwa na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo pamoja na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Viongozi hawa wamegusia pia masuala tete kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Bosnia na Herzegovina. Baadaye wamejielekeza na kuzama zaidi kuhusiana na masuala ya ndani, kwa kukazia haki na usawa katika vyombo vya haki na katika maisha ya kijamii katika ujumla wake mintarafu Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi, ili kila mwananchi aweze kupata fursa ya kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wake. Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake wamekazia umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwishoni, wamejadiliana kuhusu uwezekano wa Bosnia na Herzegovina kujiunga na Umoja wa Ulaya, EU na Baba Mtakatifu Francisko ameonesha kuridhishwa kwake na hali ya sasa ya Bosnia na Herzegovina.