Askofu mkuu Miguel Maury Buendía Balozi mpya wa Vatican nchini Uingereza
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 13 Aprili 2023 amemteuwa Askofu mkuu Miguel Maury Buendía kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Uingereza. Kabla ya uteuzi huu Askofu mkuu Miguel Maury Buendía alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Romania na Moldova. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Miguel Maury Buendía, alizaliwa tarehe 19 Novemba 1955 Jimbo kuu la Madrid, Hispania. Baada ya masomo na majiundo ya Kipadre, tarehe 26 Juni 1980 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Madrid, nchini Hispania. Kunako mwezi Julai 1987 alianza utume wake wa kidplomasia na kupangiwa huko: Rwanda, Uganda, Morocco, Nicaragua, Misri, Slovenia na Ireland.
Ilikuwa ni tarehe 19 Mei 2008 Baba Mtakatifu Benedikto VXI akamteua kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu tarehe 12 Juni 2008 na Kardinali Tarcisio Pietro Evasio Bertone, S.D.B. Siku hiyo, hiyo Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa ni Balozi mpya wa Vatican nchini Kyrgystan na Tadjikistan. Tarehe 5 Desemba 2015 akateuliwa na Papa Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Romania na tarehe 25 Januari 2016 akamtewa kuwa Balozi wa Vatican nchini Moldova. Na hatimaye, tarehe 13 Aprili 2023 akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Uingereza na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu mkuu Claudio Gugerotti ambaye tarehe 21 November 2022 aliteuliwa kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki.