Nembo na kauli mbiu ya ziara ya Kitume ya Papa Francisko nchini Hungaria
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Jumatano tarehe Mosi Machi 2023, imewakilishwa Nembo na mada ya ziara ya Kitume ya Papa Francisko nchini Hungaria kwa waandishi wa habari. Kipengele kikuu cha nembo hiyo ni Mkufu wa Daraja la Budapest, daraja la kizamani zaidi la Hungaria linalovuka mto Danube. Alama ya mji mkuu na wa nchi, hapo awali ilijengwa kuunganisha miji ya Buda na Pest. Hiyo inataka kuibua mawazo, ambayo yametajwa mara kwa mara na Baba Mtakatifu, kuhusu umuhimu wa kujenga madaraja kati ya wanadamu.
Rangi za Vatican (njano na nyeupe) na zile za kitaifa za Hungaria (nyekundu, nyeupe na kijani) zinakutana kwenye nguzo mbili za daraja. Nembo hiyo imetengwa na mduara unaoashiria Ekaristi, lakini pia ulimwengu uliokombolewa na Kristo. Upande wa kushoto wa duara, msalaba unakumbuka hotuba iliyotolewa na Papa Francisko mnamo tarehe 12 Septemba 2021 huko Budapest, ambapo matumaini yake yalikuwa msalaba ungekuwa daraja kati ya siku zilizopita na zijazo. Upande wa kulia wa duara kuna kauli mbiu isimayo: Kristo ndiye maisha yetu ya usoni na Papa Francisko huko Hungaria 28-30 Aprili 2023.
Ikumbukwe Kwa mujibu wa Msemaji wa Vyombo vya Habari Vatican, Dk. Bruni Jumatatu 27 Februari, 2023 alisema kuwa “kwa kupokea mwaliko wa Mamlaka ya Rais na Kikanisa, Baba Mtakatifu atatimiza ziara yake ya Kitume nchini Hungaria kuanzia tarehe 28-30 Aprili 2023, kwa kutembelea mji mkuu Budapest”. Na ratiba ya siku hizo za ziara ilitololewa.