Tafuta

Kardinali Cantalamessa katika mahubiri yake ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa amejikita zaidi katika “Fumbo la Imani Mintarafu Liturujia” Kardinali Cantalamessa katika mahubiri yake ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa amejikita zaidi katika “Fumbo la Imani Mintarafu Liturujia”  (Vatican Media)

Kardinali Cantalamessa: Mahubiri ya Kwaresima 2023: Ekaristi Takatifu Ni Fumbo la Imani

Kardinali Cantalamessa katika tafakari yake, Ijumaa tarehe 24 Machi 2023 kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, amejikita zaidi katika “Fumbo la Imani Mintarafu Liturujia”: “Mysterium Fidei” On the Liturgy.” Karamu ya Bwana! Fumbo la Ekaristi Takatifu ni jumla na muhtasari wa imani ya Kanisa. Ekaristi ni ishala na chemchemi ya upendo, umoja na mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia umeliwezesha Kanisa kufahamu kwa kina zaidi Liturujia katika mwanga wa Ufunuo mintarafu utume wa Yesu Kristo kuhani mkuu, unaoendelezwa na Fumbo la mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kristo Yesu ndiye mhusika mkuu wa kila adhimisho linalofanywa na Mama Kanisa kwa kushirikiana na Kanisa ambalo ni mchumba wake ili kumpatia Mwenyezi Mungu sifa na utukufu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu yenye mvuto kwa viumbe vyote. Liturujia ni tendo kubwa ambalo kwa njia yake Mwenyezi Mungu hutukuzwa kikamilifu na wanadamu wanatakatifuzwa, Kristo daima hulishirikisha Kanisa; naye Kanisa Bibiarusi wake mpendwa anamwomba na kumwabudu. Katika Liturujia, kwa ishara zinazonekana, huoneshwa na kutendeka kutakatifuzwa kwake binadamu, kila ishara ikiwa na maana ya pekee. Katika Liturujia Ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa Fumbo wa Kristo Yesu, yaanina kichwa na viungo vyake. Kimsingi, Liturujia ni tendo la Kristo Yesu Kuhani na Mwili wake, ndilo Kanisa, ni tendo takatifu kupita yote na hakuna tendo jingine la Kanisa linalofanana nalo kwa mafao kwa kiwango na kwa daraja lilelile. Liturujia ni kilele ambapo kazi ya Kanisa inaelekea, na papo hapo ni chemchemi zinamotoka nguvu zake zote. Rej. Sancrosanctum concilium 1- 17. Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwa mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia Makanisa.” Uf. 2:7. Tangu mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2023, Kardinali Cantalamessa amekwisha kuchambua na kutafakari kuhusu mchakato wa uinjilishaji na taalimungu na kwamba, Liturujia ya Kanisa ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Tafakari ya Fumbo la imani ijenge mshikamano na Kanisa la Kisinodi
Tafakari ya Fumbo la imani ijenge mshikamano na Kanisa la Kisinodi

Kardinali Cantalamessa katika tafakari yake, Ijumaa tarehe 24 Machi 2023 kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, amejikita zaidi katika “Fumbo la Imani Mintarafu Liturujia”: “Mysterium Fidei” On the Liturgy.” Karamu ya Bwana! Fumbo la Ekaristi Takatifu ni jumla na muhtasari wa imani ya Kanisa. Kumbe, namna ya waamini kufikiri hulingana na Fumbo la Ekaristi Takatifu na Ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yao ya kufikiri. Rej. KKK 1324 – 1327. Ekaristi Takatifu ni ishara ya upendo. Ni alama ya upendo wa Mungu kwetu na chemchemi ya upendo wote. Katika Sakramenti hii ya upendo, waamini wanaalikwa kushiriki na kuwashirikisha wengine upendo huu. Yaani kwa kuwa Ekaristi kwa wengine! Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI, aliwahi kusema: “Upendo tunaouadhimisha katika Sakramenti si jambo la kubaki nalo sisi wenyewe. Kwa tabia yake linadai kushirikishwa kwa wote. Kile ambacho ulimwengu unahitaji ni upendo wa Mungu; unahitaji kukutana na Kristo Yesu ili kumwamini. Ekaristi Takatifu ni chemichemi na kilele si tu cha uhai wa Kanisa, bali cha utume wake pia: Kanisa halisi la kiekaristi ni Kanisa la Kimisionari linalojibidiisha katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Watu wa Mungu wanataka kuonja na kupata mang’amuzi ya Utakatifu wa Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu; wanataka kuonja amani na utulivu wa ndani katika maisha na mahangaiko yao ya kila siku. Kanisa linapaswa kuwa ni mahali muafaka pa kuonja uwepo wa Mungu na hivyo kuanza mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu kila mtu kadiri ya wito, dhamana na majukumu yake katika maisha na utume wa Kanisa. Kwanza kabisa, waamini watambue kwamba, Kanisa licha ya kuwa ni jengo lililotabarukiwa kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, ni Jumuiya ya waamini.

Ushiriki mkamilifu wa Sadaka takatifu ya Yesu ni muhimu sana
Ushiriki mkamilifu wa Sadaka takatifu ya Yesu ni muhimu sana

Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuwawezesha waamini kuwa na ushiriki mkamilifu sanjari na kutambua utakatifu wa Liturujia ya Kanisa. Kilele cha maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni pale Padre baada ya kumaliza mageuzo anaposema “Hili ni Fumbo la Imani” anapiga magoti na kumwabudu Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Ibada ya Misa Takatifu imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Liturujia ya Neno la Mungu na Liturujia ya Ekaristi. Liturujia ya Neno la Mungu imepangwa kuendana na mpango wa historia ya ukombozi ili liweze kupenya katika nyoyo na maisha ya waamini, mwaliko kwa waamini kuwa wasikivu kwa Neno la Mungu, ili hatimaye waweze kulitafakari na kulimwilisha katika vipaumbele vya maisha na utume wao. Neno la Mungu linaganga, linatibu na kuwainua wale walioteleza na kuanguka. Neno la Mungu ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaganga na kuwaponya wagonjwa, kuwaokoa wadhambi; kuwatafuta na kuwaokoa Kondoo waliopotea; kuwasaidia wale wote waliovunjika na kupondeka moyo; wanaoelemewa na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Kristo Yesu anakaza kusema, huruma na upendo wa Mungu ni kwa ajili ya watu wote. Huu ni ujumbe kwa watu wa nyakati zote na kwamba, Neno la Mungu ni zawadi kwa watu wote na kila mmoja atajipatia zawadi hii kadiri ya Roho Mtakatifu atakavyomuwezesha, hii ni kwa sababu hata wokovu ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wote. Kumbe, changamoto ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu inapaswa kuwa ni kati ya vipaumbele vya Mama Kanisa, ili hatimaye, watu wa Mungu waweze kulipokea, ili hatimaye, hata wao waweze kushiriki katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani
Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani

Neno la Mungu linapaswa kuwa ni kiini na hatima maisha na utume wa Kanisa, ili watu wa Mungu waweze kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Neno la Mungu linamwilishwa katika maisha ya watu, maneno, maendeleo na vipaumbele katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Neno la Mungu ni mwaliko kwa kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kuamsha dhamiri mfu. “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.” Ebr 4: 12. Kardinali Raniero Cantalamessa muhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, Liturujia ya Ekaristi inapaswa kusimikwa katika tafakari na ukimya, kwa kutambua uwepo wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai. Waamini wajenge utamaduni wa kukaa kimya na kusali mara baada ya kupokea na kushiriki Ekaristi Takatifu, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa takatifu; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kushiriki kikamilifu kwa ibada na heshima kuu wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha ya waja wake, Kristo anayeandamana na wafuasi wake, bega kwa bega!

Jengeni utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu
Jengeni utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu

Waamini waoneshe moyo wa upendo kwa kushikamana na Kristo katika safari ya maisha yao, kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kumpokea! Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inogeshwe kwa sala, tafakari na Nyimbo za Ekaristi Takatifu zenye amana na utajiri unaowasaidia waamini kupata utambuzi wa Fumbo la Imani na kwamba, Roho Mtakatifu daima anatenda kazi ndani ya Kanisa. Kwa njia yake, na pamoja naye na ndani yake, wewe Mungu Baba Mwenyezi katika umoja wa Roho Mtakatifu, unapata heshima yote na utukufu milele na milele. Formula hii inaelezea utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wajiandae kikamilifu kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Ekaristi Takatifu
24 March 2023, 16:31