Tafuta

Kanisa nchini Albania linapenda kujielekeza zaidi katika ari na mwamko wa kimisionari tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kanisa nchini Albania linapenda kujielekeza zaidi katika ari na mwamko wa kimisionari tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. 

Kanisa Nchini Albania Linasimikwa Katika Damu ya Mashuhuda wa Imani na Waungama Dini

Kanisa Katoliki nchini Albania linapenda kujielekeza zaidi katika ari na mwamko wa kimisionari tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, sanjari na kuendelea kulisimika Kanisa la Kisinodi sanjari na kupembua fursa, matatizo na changamoto za maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Albania. Vatican na Albania zilianzisha uhusiano wa kidipomasilia rasmi tarehe 7 Septemba 1991 baada ya ukomunisti kubwagwa chini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dhamana ya diplomasia ya Baba Mtakatifu Francisko na Vatican Kimataifa ni: kujitahidi kujenga mazingira ya ushirikiano, mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa, maskini na wahitaji zaidi wakipewa kipaumbele cha kwanza, kama ushuhuda wa unyenyekevu unaoshinda kiburi na tabia ya kutaka kujimwambafai kwa kutumia nguvu za kiuchumi, kisiasa na kivita. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, tarehe 19 Machi 2013 amejikita kuhusu umuhimu wa diplomasia ya Vatican kufumbatwa katika: misingi ya haki jamii na amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote, kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo fungamani! Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu mamboleo. Mataifa yatambue kuwa, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na sababu mbalimbali.

Kanisa Katoliki nchini Albania linasimikwa juu ya damu ya mashuhuda
Kanisa Katoliki nchini Albania linasimikwa juu ya damu ya mashuhuda

Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa anakazia kwa namna ya pekee: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia! Lengo la tatu la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu! Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani na utulivu, kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia unaojikita katika kubainisha mbinu mkakati wa mawasiliano, vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kujitokeza pamoja na kuunda mazingira ya kuaminiana na kuthaminiana, ili kuendeleza majadiliano. Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbalimbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Mashuhuda wa imani ni nguzo imara wa ujenzi wa Kanisa.
Mashuhuda wa imani ni nguzo imara wa ujenzi wa Kanisa.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 20 Machi 2023 anafanya hija ya kichungaji nchini Albania, kwa mwaliko kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini humo. Albania na Vatican, zilianza kuwa na mahusiano ya kidiplomasia kuanzia mwaka 1920, lakini uhusiano huu ulisuasua wakati wa Utawala wa Kikomunisti nchini humo na huo ukawa ni mwanzo wa madhulumu na nyanyaso dhidi ya Kanisa nchini humo. Mahusiano ya kidiplomasia yaliweza kujengwa upya tarehe 7 Septemba 1991 baada ya Utawala wa Kikomunisti kuangushwa chini. Baraza la Maaskofu Katoliki Albania linasema, ziara hii ya kichungaji ya Askofu mkuu Paul Richard Gallagher ni kuendeleza mchakato wa kuimarisha mahusiano na mafungamamo ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili ambayo yameoneshwa kwa namna ya pekee baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II kutembelea Albania tarehe 25 Aprili 1993 na Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija yake ya kitume nchini humo tarehe 21 Septemba 2014. Katika kipindi cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Baba Mtakatifu Francisko alionesha upendo na ukaribu wa pekee kwa familia ya Mungu nchini Albania. Kanisa nchini Albania linapenda kujielekeza zaidi katika ari na mwamko wa kimisionari tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, sanjari na kuendelea kulisimika Kanisa la Kisinodi sanjari na kupembua fursa, matatizo na changamoto za maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Albania. Kristo Yesu aliwaambia Mitume wake kwamba, anawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu, hivyo, walipaswa kuwa na busara kama nyoka na wapole kama hua, kwani huko duniani, watakiona cha mtema kuni! Kutakuwa na kinzani na wengi watawachukia kwa sababu ya jina lake.

Albania na Vatican zitaka kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia
Albania na Vatican zitaka kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia

Lakini, aliwakumbusha kwamba, wale watakaovumilia hadi mwisho, hao ndio watakaookoka. Matumaini ya Kikristo ni nguvu ya mashuhuda na waungama imani. Yesu alipowachagua na kuwatuma wafuasi wake, hakuwahakikishia mafanikio ya chapuchapu kama maji kwa glasi! Kristo Yesu, aliwaonya na kuwaambia kwamba, utangazaji, ushuhuda na ujenzi wa Ufalme wa Mungu una magumu na changamoto zake kwani watachukiwa kwa sababu ya jina lake. Hili ni jambo la kushangaza sana kwani Wakristo kwa asili wanapenda, lakini daima wanachukiwa sana. Imani thabiti inashuhudiwa katika mazingira tete, kinzani na hatarishi! Hii ni kutokana na ukweli kuwa Wakristo ni watu wanaopambana na mawimbi makali ya maisha na kwamba, ulimwengu umejeruhiwa sana na uwepo wa dhambi. Hali hii inashuhudiwa kutokana na ubinafsi uliokithiri sanjari na ukosefu wa haki msingi za binadamu hasa kwa wafuasi wa Kristo, kwani wao wanajitahidi kukita maisha yao katika mantiki ya matumaini yaliyofunuliwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Kanisa nchini Albania limesimikwa katika msingi wa mashuhuda wa imani na waungama dini.

Diplomasia Vatican
18 March 2023, 16:15