Tafuta

Nembo ya Caritas Internationalis Nembo ya Caritas Internationalis 

Caritas Internationalis juu ya Usafirishaji haramu wa binadamu katika migogoro wa silaha

Usafirishaji haramu wa binadamu katika migogoro ya kisilaha na hali baada ya migogoro ni mada iliyozungumzwa pembeni kwa kikao cha 52 cha Kawaida cha Baraza la haki za Kibinadamu huko Geneva Uswiss,kilichaoandaliwa na Caritas Internationalis,Caritas Ufaransa na Shirika la Malta,kwa msaada wa COATNET.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Caritas Internationalis, Caritas Ufaransa na Shirika la Malta, kwa msaada wa COATNET, Jumatatu tarehe 27 Machi 2023 walifanya mkutano kuhusu mada ya "Usafirishaji haramu wa Binadamu katika Migogoro ya Kivita na Hali Baada ya Migogoro," kando ya  Kikao cha 52 cha Kawaida cha Baraza la Haki za Kibinadamu katika Jengo la Umoja wa Mataifa huko Geneva. Tukio hilo la majadiliano la jopo lililofadhiliwa na Utume wa Kudumu wa Costa Rica, Italia, Poland, Romania na Shirika Kuu la Malta, lilifafanua juu ya athari za migogoro ya silaha kwa haki za binadamu na juu ya hatari ya watu kwa biashara mbaya ya binadamu. Wanajopo hao pia walizungumzia juu ya haja ya ushirikiano thabiti kati ya mashirika ya kibinadamu na mashirika ya kiraia ili kusaidia vyema na kuwarekebisha waathiriwa wa usafirishaji haramu wa binadamu.

Ripoti ya UN 2022 kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu

Kama ilivyoelezwa katika Ripoti ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu (2022) kila siku katika kila nchi, wanawake, wanaume na watoto wananyonywa na kufanywa watumwa na wasafirishaji kwa njia mbalimbali. Watu maskini na walio hatarini ndio wako kwenye hatari zaidi. Katika hotuba yake ya ufunguzi wakati wa kongamano hilo, Bwana Michel Veuthey, Balozi wa Shirika  Kuu la Malta la kufuatilia na kupambana na usafirishaji haramu wa watu, alisema mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kukomesha utumwa mamboleo. Alitoa wito wa kuboreshwa kwa ushirikiano kati ya wadau wanne muhimu (serikali, biashara, vyombo vya habari na wasomi) ili kutosahau wahanga na waathirika wa biashara haramu ya binadamu.

Gamba de Potgieter: Watoto wanateseka sana 

Akizungumzia vipaumbele vya Kimataifa vya kupambana na biashara haramu ya binadamu inayotokana na migogoro ya kivita, Bi. Virginia Gamba de Potgieter, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Katibu Mkuu wa Watoto katika Migogoro ya Silaha, alisema kupitia ujumbe kwa  njia ya video kwamba juhudi za pamoja zinahitaji kupanua zaidi ya maeneo yenye migogoro ili kutambua na kufuatilia hatari na udhaifu, hasa wa watoto. “Mtoto aliyetekwa nyara anakuwa katika hatari zaidi ya kuajiriwa na kutumia aina nyingine za unyonyaji, ikiwa ni pamoja na kazi ya kulazimishwa, ndoa za kulazimishwa na unyonyaji wa kingono, na utumwa,” alisema Bi. Gamba de Potgieter. Katika Ripoti ya Mwisho ya Mwaka ya Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Kivita, watoto 3,459 walitekwa nyara (wavulana 2,399 na wasichana 1,038). Kwa ujumla, tangu ripoti ya awali, kumekuwa na ongezeko la asilimia 20 la idadi ya watoto wanaotekwa nyara, na utekaji nyara wa wasichana pekee umeongezeka kwa asilimia 40. Kwa hiyo “Takriban matukio yote ya utekaji nyara yalihusishwa na makundi yenye silaha yenye idadi kubwa zaidi kuthibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia, Bonde la Ziwa Chad, Burkina Faso na Nigeria”," aliongeza Bi. Gamba de Potgieter. 

Holynska: Usarishaji haramu wa binadamu  huko Ukraine

Katika hali ya kutisha ya vita, wakati fulani wanaume, wanawake, na watoto wananyonywa ili waendelee kuishi. Migogoro ya vita iliyopo na inayoibuka, kama vile huko Ukraine, imesababisha maendeleo makubwa ya usafirishaji haramu wa binadamu. Bi. Natalia Holynska, Meneja wa miradi ya kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu wa Caritas Ukraine na COATNET, juu ya mada ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu Katika Muktadha wa Migogoro ya Silaha nchini Ukraine alishiriki sha kwa kina historia za kutisha za wanawake watatu wa Kiukreni ambao ni wahathirika wa unyanyasaji wa kijinsia. “Umoja wa Mataifa umethibitisha zaidi ya kesi 100 za ubakaji au unyanyasaji wa kijinsia tangu mwanzo wa vita, lakini nadhani ni 'kesi zilizothibitishwa' tu na ni ncha ya barafu, Bi Holynska alisema. Katika muktadha wa Ukraine, umri wa wahthrika ni kati ya umri wa miaka 4-82, na watoto wakiwa kundi la watu walio hatarini zaidi. Kulingana na takwimu za serikali ya Ukraine hadi sasa, watoto 464 wameuawa na zaidi ya 935 kujeruhiwa. 

Fernea: Kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu - Romania

Kwa upande wa Codruta Fernea, Rais wa Chama cha Matendo Katoliki nchini Romania, alisema shirika lake linaanzisha hatua ya kwanza kuelekea huduma ya hurumaambapo mwingiliano na waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu sio moja ya huduma bali, badala yake, ya kubadilishana wema na heshima. Alisema kuwa ugumu wa kufuatilia wahathrika na ukosefu wa takwimu rasmi juu ya idadi ya utekaji nyara inaweza kuwafanya wananchi kuamini kuwa biashara haramu haifanyiki katika mipaka ya Romania. Kuhusiana na mada ya Kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu mipakani na katika nchi jirani, Fernea alisema kuwa: “Kukosekana kwa utulivu na mkanganyiko unaosababishwa na migogoro kunawawezesha wafanyabiashara kufanya kazi kwa urahisi zaidi na kuepuka utekelezaji wa sheria. Alisema wakimbizi wako hatarini zaidi kwa usafirishaji haramu wa binadamu kutokana na ukosefu wa usaidizi wa mitandao yao ya kuaminiana kama vile familia, marafiki au watu wanaofahamiana, na changamoto za kuzunguka mazingira yasiyofahamika. Kwa ushirikiano na mashirika kama Caritas, Fernea alisema mipango ya Chama katoliki cha matendo Romania ni pamoja na kufanya  mafunzo ya kukuza ufahamu, usaidizi wa kiufundi na huduma za ujumuishaji kwa wale wanaohitaji.

Sayah: Wahamiaji na wakimbizi, Lebanon wako hatarini

Tangu Oktoba 2019, Lebanon imekumbwa na mizozo inayoingiliana kama vile mzozo mkubwa wa kiuchumi na kifedha, janga la UVIKO-19, mlipuko wa Moto  Beirut, pamoja na shida ya usalama wa chakula kutokana na vita nchini Ukraine. Kwa hiyo, kutokana na changamoto hizi, Walebanon kadhaa wamechagua kuondoka katika nchi zao na kuhamia nchi nyingine. Juu ya mada ya Wahamiaji na wakimbizi walio katika mzozo ndani ya mzozo,  Hessen Sayah, Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Caritas Lebanon na COATNET, alisema, “Wahamiaji na wakimbizi wa Lebanon walikuwa hatarini hasa kwa ukosefu wa msaada wa matibabu.” Gharama kubwa ya dawa, ukosefu wa huduma za usaidizi wa kisaikolojia na kijamii, na msongo wa mawazo wa kutoweza kulipia kodi ya nyumba kumesababisha wahamiaji kuwa katika hatari ya biashara haramu ya binadamu badala ya ahadi za chakula, nyumba na msaada wa kimatibabu zinazotolewa na wasafirishaji. Kwa mujibu wake amesisitiza kuwa: “Caritas Lebanon imejitolea kusaidia waathiriwa na waathirika kukomesha mzunguko wa vurugu kutoka kwa kujirudia hapa, na wanajifunza kuwa na matumaini,” Bi. Sayah alisema.

Mikiko Otani: Ushirikiano na kazi ya pamoja na mashirika ya UN

“Uangalifu maalum na hatua zinahitajika kwa nyanja zote za kuzuia, utambuzi, mashtaka, uokoaji na urekebishaji wa waathirika wa watoto, alisema Mikiko Otani, Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto, juu ya mada ya "Watoto katika migogoro ya kivita". Kwake yeye alisisitiza haja ya ushirikiano na kazi ya pamoja kati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa, mataifa na jumuiya ya kiraia ili kuzingatia mamlaka ya kukuza na kulinda haki zote za binadamu kwa watu wote, na kuongeza ufahamu wa suala la biashara ya binadamu, kufafanua mfumo wa kisheria, na kufanya. mapendekezo ya kuzuia, ulinzi, uokoaji na ushirikiano na upatikanaji wa haki.

28 March 2023, 16:58