Tafuta

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher nchini Albania: Ujasiri, unyenyekevu na kuendelea kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher nchini Albania: Ujasiri, unyenyekevu na kuendelea kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, 

Kanisa Nchini Albania: Ujasiri, Unyenyekevu na Majadiliano!

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, akiwa nchini Albania, amewaalika Maaskofu Katoliki nchini Albania kujivika fadhila ya: Ujasiri, unyenyekevu na kuendelea kujikita katika majadiliano, ili kukabiliana na: matatizo, changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo. Familia ziwe ni vitalu vya kurithisha tunu msingi za Kikristo! Vijana wawe ni mashuhuda wa imani, maadili na utu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 20 Machi 2023 amehitimisha hija ya kichungaji nchini Albania, mwaliko uliotolewa kutoka kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini humo. Albania na Vatican, zilianza kuwa na mahusiano ya kidiplomasia kuanzia mwaka 1920, lakini uhusiano huu ulisuasua wakati wa Utawala wa Kikomunisti nchini humo na huo ukawa ni mwanzo wa madhulumu na nyanyaso dhidi ya Kanisa nchini humo. Mahusiano ya kidiplomasia yaliweza kujengwa upya tarehe 7 Septemba 1991 baada ya Utawala wa Kikomunisti kuangushwa chini. Baraza la Maaskofu Katoliki Albania linasema, ziara hii ya kichungaji ya Askofu mkuu Paul Richard Gallagher ni kuendeleza mchakato wa kuimarisha mahusiano na mafungamamo ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili ambayo yameoneshwa kwa namna ya pekee baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II kutembelea Albania tarehe 25 Aprili 1993 na Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija yake ya kitume nchini humo tarehe 21 Septemba 2014. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, akiwa nchini Albania, amewaalika Maaskofu Katoliki nchini Albania kujivika fadhila ya: Ujasiri, unyenyekevu na kuendelea kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukabiliana na: matatizo, changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo.

Maaskofu wakabiliane na changamoto kwa ujasiri na unyenyekevu
Maaskofu wakabiliane na changamoto kwa ujasiri na unyenyekevu

Imekuwa ni fursa kwa Baraza la Maaskofu nchini Albania kubainisha sera na mikakati yao ya shughuli za kichungaji, pamoja na kuendelea kushughulia matatizo na changamoto zinazojitokeza, ili kuimarisha uhusiano na mafungamano kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Albania. Maaskofu Katoliki Albania wamekazia kuhusu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kuwahusisha watu wote wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Wametia nia ya kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kama sehemu ya ujenzi wa utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Viongozi wa dini wanapaswa kuwa wadau wa kwanza katika kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na matumaini. Imekuwa ni nafasi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Albania kurejea tena katika historia na shughuli mbalimbali zinazoendeshwa na Baraza hili. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher alipata fursa pia ya kutembelea Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Bikira Maria, Mshauri wa Ajabu.” Wanafunzi watambue kwamba, Chuo kikuu ni mahali ambapo vijana wanapata mwanga wa kuweza kufukuzia mbali giza la ujinga, ili hatimaye, siku moja wanafunzi hawa wawe pia kuwa ni chumvi na mashuhuda wa nuru ya ulimwengu ambayo ni Kristo Yesu! Wanafunzi wajifunze kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha kwa kujikita katika: umoja, mshikamano, upendo na ukarimu, kwani ufanisi wao mwisho wa siku, utapimwa kwa kuzingatia nyenzo hizi. Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, waweze kupata ufunuo wa ukweli wote ambao ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kusikilizana
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kusikilizana

Wakati huo huo, waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utu wema, haki, amani, upendo, ukarimu na mshikamano, sanjari na kuzingatia kweli za Kiinjili. Familia za Kikristo ziwe ni mahali ambapo, imani, matumaini, mapendo, maadili na utu wema vinarithishwa, kama ushuhuda wa nuru ya Kristo Yesu na tunu msingi za Kiinjili. Waamini watambue kwamba, wanapokabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbalimbali watambue kwamba, Kristo Yesu yuko kati pamoja nao. Wakristo wote, lakini kwa namna ya pekee, watu wa Mungu nchini Albania wanapaswa kutangaza na kushuhudia ujasiri wa imani kama walivyofanya mashuhuda 38 wa imani nchini Albania kwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wahamasike zaidi kuwa ni mashuhuda wa imani kwa njia ya matendo adili, matakatifu na uchaji wa Mungu. Ziara hii ya kikazi nchini Albania imekuwa ni fursa ya kulishukuru na kulipongeza Kanisa mahalia kwa kuendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Albania hususan katika sekta ya elimu, afya, maendeleo pamoja na ustawi wa jamii. Mada nyingine tete zilizojadiliwa na viongozi katika mikutano yao ya faragha ni pamoja: Athari ya Vita kati ya Urusi na Ukraine, matumaini ya Albania kujiunga na Umoja wa Ulaya sanjari na umuhimu wa kujenga ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Ulaya.

Kanisa Albania
25 March 2023, 16:43