Ask.Mkuu Nwachukwu katibu mpya katika Baraza la Uinjilishaji
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Katibu mkuuwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji katika kitengo cha kwanza cha Uinjilishaji na Makanisa Mapya mahalia, Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu wa Kanisa la Acquaviva, na ambaye hadi utezi huo alikuwa ni Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na Taasisi za Maalum huko Geneva na katika Shirika la Biashara Duniani (WTO)) pamoja na Mwakilishi wa Vatican katika Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
Masomo na huduma
Alihitimu katika Maandiko Matakatifu kutoka Taasisi ya Kipapa ya Biblia na kutunukiwa shahada ya pili ya udaktari wa taalimungu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana na sheria za Kanisa za Kanoni kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas wa Akwino". Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu aliingia katika huduma ya kidiplomasia ya Vatican mnamo mwaka 1994 na kwa miaka mingi baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo cha Kipapa cha Kikanisa kunako mwaka 1992 alihudumu katika Ubalozi wa Kitume nchini Ghana, Paraguai, Algeria, baadaye katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na taasisi maalum huko Geneva.
Askofu Mkuu Nwachukwu alihudumu katika Kitengo cha Pili cha Mahusiano na Nchi na mashirika ya Kimataifa cha Sekretarieti ya Vatican na mnamo mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Mkuu wake wa Itifaki. Tarehe 12 Novemba 2012, Papa Mstaafu Benedikto XVI alimteua kuwa Balozi wa Vatican nchini Nicaragua, akirithi nafasi ya Askofu Mkuu Henryk Józef Nowacki, aliyehamishwa kuwa mkuu wa watawa nchini Sweden na Iceland; wakati huo huo alipewa hadhi ya Uaskofu mkuu na Kanisa la Acquaviva. Kufuatia na kuwekwa wakfu kwake kiaskofu, ambako kulifanyika mnamo tarehe 6 Januari 2013, kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, alianzisha shirika la Mfuko wa Fortune Aquaviva", lenye lengo la kusaidia mapadre wa Nigeria, wanaume na wanawake watawa wenye kuhitaji msaada.
Balozi wa Vatican katika nchi mbalimbali
Mnamo mwaka 2017 Papa Francisko alimteua kuwa balozi wa kitume huko Trinidad na Tobago, Antigua na Barbuda, Barbados, Dominica, Jamaica, Watakatifu Kitts na Nevis, Mtakatifu Vincent na Grenadines na Guyana pamoja na mjumbe wa kitume huko Antilles. Mnamo 2018 aliteuliwa kuwa Balozi wa Mtakatifu Lucia, Grenada na Bahamas, na baadaye Suriname na Belize. Tarehe 17 Desemba 2021 Baba Mtakatifu Francisko alimteua tena kuwa mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa na taasisi maalum huko Geneva na Shirika la Biashara Ulimwenguni na mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Shirika la Kimataifa la Uhamiaji ambpo nafasi iliyoshikiliwa hadi uteuzi wa leo hii tarehe 15 Machi 2023.