Shahada ya heshima kwa Kard.Ayuso kutoka chuo kikuu cha Indonesia!
Na Angella Rwezaula - Vatican
Kwa msingi wa kila ushirikiano kati ya waamini wa dini mbalimbali, kuna mzizi wa ubinadamu wetu wa pamoja. Mazungumzo hayaanzii kutoka mwanzo, hutoka msingi muhimu wa mkutano. Kadinali Miguel Ángel Ayuso Guixot Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini alisema hayo mnamo Jumatatu tarehe 13 Februari 2023 nchini Indonesia. Katika nchi yenye Waislamu wengi zaidi duniani, Kiongozi huyo alipokea tunu ya shahada ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Kiislam Negeri cha Sunan Kalijaga wilaya ya Yogyakarta, pamoja na Yahya Cholil Staquf, rais wa Nahdlatul Ulama (NU), na Sudibyo Markus, rais wa zamani wa Muhammadiyah, ambayo ni mashirika makubwa ya Kiislamu ya Sunni ya taifa la Asia.
Uwajibikaji wa dini katika kutenda pamoja kwa manufaa ya wote
Kardinali Ayuso akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa dini katika kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wote, alidokeza kwamba leo tunaishi katika jamii zenye wingi wa watu wengi, kwa bahati mbaya kwa upande mmoja zenye sifa ya migogoro inayoendelea kukua kati ya makundi ya kidini, kitaifa na kikabila na kwa upande mwingine, kutoka katika ubaguzi dhidi ya watu binafsi na watu walio katika mazingira magumu. Ulimwengu uliogawanyika, aliendelea, kwamba kwa sababu ya uchokozi unaosababishwa na tamaa ya kupata nguvu zaidi na ushawishi juu ya wengine. Kinachoongezwa kwa hili ni mzozo wa kiafya wa kimataifa unaosababishwa na janga la Uviko-19.
Kuishi pamoja kwa amani na usawa
Na katika haya yote, Kardinali aliendelea kusisitiza kuwa inatia uchungu na inatisha kuona jinsi utambulisho wa kidini unavyotumiwa, hata kisiasa, na kusababisha mgawanyiko mkubwa zaidi ndani ya jamii. Kuta zimejengwa ili kutenganisha, badala ya madaraja ya kuunganishw kwa nia ya " kuishi pamoja kwa amani na usawa. Kwa hiyo umuhimu uliosisitizwa na Kardinali Ayuso katika dini ni kuponesha majeraha ya ulimwengu dhaifu na kujenga madaraja kati ya tofauti, kama Kanisa Katoliki limekuwa likifanya kwa miaka 60 kwa kuhamasisha mienendo ya mazungumzo na ushirikiano, unaozingatia ukweli na juu ya kujitoa sadaka.
Mahusiano ya waamini wa dini mbali mbali
Kwa hiyo akiendelea Kardinali Ayuso, alidha alikumbusha jinsi ambavyo Papa Francisko amerudia mara kadhaa katika matukio mbalimbali kwamba dini hazipaswi kuwa tatizo, lakini kuwa sehemu ya kuleta ufumbuzi. Amani na mshikamano kati ya waamini unaotakiwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni kiini cha tafakari na matendo ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye tangu mwanzo wa Upapa wake ameweka msisitizo mkuu juu ya mahusiano kati ya waamini wa dini mbalimbali, huku akikazia thamani ya urafiki na heshima.
Kubadilisha mgongano wa ustaarabu kuwa mazungumzo ya ustaarabu
Hivyo msisitizo wa Kardinali Ayuso ulikuwa ni kubadilisha mgongano wa karibu wa ustaarabu kuwa mazungumzo ya ustaarabu, ambapo jumuiya zote za kidini zinaitwa kufufua mila na tamaduni halisi ili kuhusiana na kila mmoja na kushirikiana katika hali ya kuelewana na kuheshimiana. Kwa ufupi, ni suala la wajibu wa kujenga jamii pamoja, badala ya kutawala; kutetea haki za kila mtu kwa pamoja, bila ubaguzi; na kulinda kutokiukwa kwa hadhi ya mwanadamu, ili wote wafanikiwe, badala ya kupoteza nguvu za kushindana kwa maslahi fulani.