Papa amemteua Mwenyekiti mpya wa Maktaba ya Kitume
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Jumanne tarehe 14 Februari 2023, Baba Mtakatifu amemteua Mwenyekiti mpya wa Maktaba ya Kitume, Vatican, Mheshimwa Padre Mauro Mantovani, S.D.B., ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Mkuu wa Kitivo cha Falsafa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesiano, jijini Roma Italia.
Wasifu wake
Padre Mantovani alizaliwa mnamo tarehe 3 Januari 1966 huko Moncalieri (Italia). Alifunga nadhiri zake za kwanza katika Jumuiya ya Wasalesiani ya Shirika la Mtakatifu Yohane Bosco mnamo 1986 na akapewa daraja la ukuhani mnamo 1994. Mnamo mwaka 2006 alipata Shahada ya Uzamivu ya Falsafa na Barua katika Chuo kikuuu cha kipapa cha Salamanca (Hispania), na mnamo mwaka 2011 akapata Shahada ya Uzamivu ya Taalimungu ya Mtakatifu Thomasi (Thomistic) katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas, Angelicum jijini Roma.
Nyadhifa nyingine
Tangu mnamo mwaka 2007 amekuwa ni Profesa Kamili katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesiano mjini Roma, ambako alishika nyadhifa zifuatazo: Mkuu wa Kitivo cha Falsafa; Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Mawasiliano ya Jamii; Makamu mkuu; Mkuu wa Chuo. Na hadi kufikia uteuzi huo alikuwa pia ni mjumbe wa Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas wa Akwino na wa Kamati ya Kisayansi ya Shirika la Vatican kwa ajili ya Tathmini na kuhamasisha Ubora wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu vya Kikanisa(AVEPRO).