Tafuta

Kongamano la Kimataifa linalonogeshwa na kauli mbiu “Wachungaji na Waamini Walei Wanaitwa Kutembea Bega kwa bega.” Kongamano la Kimataifa linalonogeshwa na kauli mbiu “Wachungaji na Waamini Walei Wanaitwa Kutembea Bega kwa bega.”   (Santiago Perez de Camino)

Kongamano la Kimataifa: Walei na Wachungaji: Uinjilishaji na Utume wa Kanisa

Walei na Wachungaji: Kuna haja ya kuanzisha mchakato wa ushirikiano na mafungano ya dhati kati ya walei na wachungaji wao katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wa Mataifa. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa waamini walei kutumia kikamilifu karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Ushiriki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, waamini walei, kama washiriki wa huduma ya Kristo Yesu kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika sana, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili.  Maana walei wenye roho halisi ya kitume, kama wale wanaume na wanawake waliokuwa wakimsaidia Mtume Paulo katika kueneza Injili (Taz. Mdo 18:18.26; Rum 16:3), wanawakirimia ndugu zao yale waliyopungukiwa, na wanaburudisha roho za wachungaji na za waamini wengine wa taifa la Mungu (Taz. 1Kor 16:17-18). Tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Vatican, kumekuwepo na uanzishwaji wa mashirika na vyama vya kitume sehemu mbalimbali za dunia na vyama hivi vimesaidia kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, malezi na majiundo makini ya maisha ya: Imani na uadilifu, Sakramenti za Kanisa pamoja na maisha ya sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; mambo muhimu yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kama kielelezo cha imani tendaji na ushiriki mkamilifu katika mchakato wa uinjilishaji na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu
Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu

Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na hiki ni kiini cha maisha ya Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani ntendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Kumbe, kwa maneno machache, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu. Mababa wa Kanisa wanasema, sasa umefika wakati wa kuyangalia ya mbeleni kwa matumaini zaidi, ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazoendelea kujitokeza miongoni mwa waamini walei ndani ya Kanisa Katoliki, ili waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, huku wakitembea bega kwa bega na wachungaji wao kama sehemu ya utekelezaji mchakato wa uinjilishaji na utume wa Kanisa.

Waamini walei washirikishe karama, mapaji na taaluma zao
Waamini walei washirikishe karama, mapaji na taaluma zao

Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, kuanzisha Alhamisi tarehe 16 hadi Jumamosi tarehe 18 Februari 2023 linaendesha Kongamano la Kimataifa linalonogeshwa na kauli mbiu “Wachungaji na Waamini Walei Wanaitwa Kutembea Bega kwa bega.” Kongamano hili linawashiriki 210 kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu 74 sehemu mbalimbali za dunia. Linahudhuriwa na waamini walei 107, maaskofu 67, mapadre 36 pamoja na wawakilishi wa mashirika na vyama vya kitume vinavyo tambuliwa na Baraza la Kipapa 29. Mwishoni mwa Kongamano hili, washiriki watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, kuna haja ya kuanzisha mchakato wa ushirikiano, mshikamano na mafungano ya dhati kati ya waamini walei na wachungaji wao katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa waamini walei kutumia kikamilifu karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao.

Ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa
Ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa

Hii ni fursa kwa waamini walei kutumia taaluma na rasilimali muda, uzoefu na mang’amuzi yao kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anataka kuona kwamba, waamini walei wanatembea bega kwa bega na wachungaji wao katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, ili kukuza na kuimarisha: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa waamini walei ndani ya Kanisa. Ni wakati wa waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutekeleza yale majukumu yanayowaangukia kitaaluma mintarafu shughuli za kichungaji. Yale majukumu yanayoweza kutekelezwa kikamilifu na waamini walei, wapewe dhamana hii, bila kuzunguka Mbuyu! Kongamano hili linajikita katika mambo makuu matatu: Msingi wa ushirikiano kati ya waamini walei na wachungaji wao katika uwajibikaji wa pamoja. Pili ni malezi na majiundo makini ya waamini walei, ili waweze kushirikiana, kushikamana na kufungamana na wachungaji wao katika maisha na utume wa Kanisa kwa kufafanua dhamana na utume wa wachungaji. Tatu ni ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei wanawajibika kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji na utume wa Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Vyama na Mashirika ya Kitume ni mashuhuda amini wa ushirikiano na mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa, hasa katika mchakato wa ujenzi wa dhamira nyofu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji.

Walei na Wachungaji
16 Februari 2023, 15:20