Katibu mpya msaidizi wa Baraza la Kipapa la Ibada&Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Jumanne tarehe 31 Januari 2023, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Krzysztof Marcjanowicz kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Hadi uteuzi huo alikuwa ni Afisa wa Ofisi ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji katika kitengo cha masuala msingi ya Uinjilishaji katika ulimwengu na pia katika sehemu ya Maadhimisho ya liturujia za kipapa.
Monsinyo Krzysztof Marcjanowicz alizaliwa huko Krakow nchini Poland mnamo tarehe 24 Machi 1977. Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 8 Juni 2002 kwa ajili ya Jimbo Kuu Katoliki la Krakow. Aliendelea na masomo yake na kupata shahada ya Udaktari katika Liturujia Takatifu katika Taasisi ya Kipapa ya Mtakatifu Anselmi jijini Roma.
Na tangu mwezi Machi 2012 amekuwa afisa wa Ofisi ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji. Na ni Padre anayetoa huduma katika Kikanisa cha Kipapa na mhusika wa maadhimisho ya kiliturijia za Kipapa.