Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso Balozi wa Vatican Nchini Yordan
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Yordan. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso alikuwa ni Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso alizaliwa tarehe 6 Oktoba 1964. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 24 Juni 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Bolzano-Bressanone (Bozen-Brixen; Dioecesis Bauzanensis-Brixinensis) lililoko nchini Italia.
Tarehe 22 Juni 2010 akateuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, huduma iliyokoma tarehe 1 Januari 2017. Tarehe 9 Novemba 2017, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu mwambata na kumpandisha hadhi ya kuwa ni Askofu mkuu na hatimaye, tarehe 16 Desemba 2017, akawekwa wakfu kuwa ni Askofu mkuu na Kardinali Fernando Filoni. Utume huu ukafikia ukomo wake tarehe 3 Desemba 2022. Tarehe 21 Januari 2023, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Balozi mpya wa Vatican nchini Yordan.