Askofu mkuu Angelo Accattino Balozi Mpya wa Vatican Nchini Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Angelo Accattino kuwa ni Balozi mpya wa Vatican nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Angelo Accattino alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Bolivia. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Angelo Accattino alizaliwa tarehe 31 Julai 1966, Jimboni Casale Monferrato, nchini Italia Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre tarehe 25 Juni 1994 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Askofu mkuu Angelo Accattino alianza utume wake katika masuala ya diplomasia ya Vatican, tarehe 1 Julai 1999.
Tangu wakati huo akatekeleza dhamana na utume wake huko Trinidad na Tobago, Colombia, Perù, Vatican na hatimaye, Marekani na Uturuki. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Septemba 2017 akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Bolivia na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu na kuwekwa wakfu kama Askofu mkuu tarehe 25 Novemba 2017. Amebahatika kutunukiwa Shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Tarehe 2 Januari 2023 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Tanzania.