Papa akutana na Bi Čaputová,Rais wa Jamhuri ya Slovakia
Na Angella Rwezaula; – Vatican News.
Papa Francisko Jumamosi tarehe 10 Desemba 2022, amekutana na Bi Zuzana Čaputová, Rais wa jamhuri ya nchi ya Slovachia, ambapo mara baada ya mkutano huo amekutana pia na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican kwa ajili ya Mahusiano na Nchi na Mashirika ya Kimataifa. Kwa mujibu wa msemaji wa vyombo vya habari, Vatican, amebainisha kwamba katika mazungumzo yao, na Katibu wa Vatican, wameonesha uhusiano mwema uliopo sehemu zote mbele kati ya Vatican na Jamhuri ya Slovakia, na juu ya nafasi ya Kanisa katika Jamii.
Viongozi hawa mazungumzo yao, wamejadili kwa kina juu ya vita nchini Ukraine na matokeo yake kwa ngazi ya kikanda na kimataifa kwa namna ya pekee umakini kwa hali halisi ya kibinadamu, mapokezi ya wakimbizi na migogoro ya kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo kama ilivyo kawaida ya kubadilisha zawadi, Papa amemzawadia Rais medali ya Mtakatifu Martino; vitabu vya hati za kipapa; ujumbe kwa ajili ya amani kwa mwaka 2022; Hati kuhusu Udugu wa Kibinadamu, Kitabu juu ya Statio Orbis , yaani Njia ya Msalaba ya tarehe 27 Machi 2020, kilichondaliwa na LEV na kitabu chenye sentensi zinazohusu vita nchini Ukraine.
Na wakati huo huo Rais wa Slovakia Bi Zuzana Čaputová, amemzawadia Papa: Kikapu cha keki za za siku kuu ya Noeli zilizoandaliwa na watu walemavu; mti uliopambwa na mapambo ya Noeli ambao umetengenezwa na wanawake wa jumuiya moja maskini, picha moja iliyochorwa, ambayo inaonesha Mtakatifu Francis wa Assisi, kazi ya Dorota Sadovska, Kitabu cha vielelezo kwa ajili ya watoto, chenye sentesi zilizotamkwa na Baba Mtakatifu, na hatimaye kitabu kinachoonesha watu mashuhuri wa Kanisa la Slovakia kilichoandikwa na Silvo Krcmery.