Mt.Egidio,maskini na wakimbizi Ukraine.Kard.Parolin:mshikamano huokoa!
Na Angella Rwezaula ; - Vatican.
Takriban watu 300 maskini, wasio na makazi, wazee na, kwa mwaka huu, pia kuongezea wakimbizi wa Kiukreni ambao waliweza kula dengu na mkate wa nyama na kila mmoja akaweza kupokea zawadi ya kibinafsi walishiriki katika chakula cha mchana cha Noeli tarehe 25 Desemba 2022 kilichoandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika Basilika ya Mtakatifu Maria huko Trastevere Roma. Tukio linaloadhimisha jambo muhimu kwa pande zote yaani kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Jumuiya ilipoanzishwa mpango wa kutoa chakula cha mchana wakati wa siku kuu ya mnamo tarehe 25 Desemba 1982. Wakati huo kulikuwa na watu 47 waliokuwa wameketi kwenye meza ya Siku kuu iliyowekwa ndani ya kuta za wakristo wa kwanza katika Basilika hiyo katikati ya mtaa wa Trastevere Roma. Kwa miaka mingi, wafanyakazi wa kujitolea na waendeshaji wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio wamekuwa wakihudumia kutoa chakula cha mchana, kwa watu maskini 80,000 nchini Italia na 250,000 duniani kote, kwani tendo hilo huwa linakwenda sambamba na Jumuiya zao zilizoko duniani kote kutekeleza tendo la upendo wa kuwa karibu na wale ambao wangekuwa na upweke katika siku maalumu hiyo ya kuzaliwa kwa Bwana. Kwa maana hiyo katika Basilika hiyo Dominika ya noeli iliwaona watu wapatao 300, wameketi kwenye meza mbalimbali zilizowekwa vitambaa vyekundu vya nyota za Siku Kuu ya Kuzaliwa kwa Bwana.
Mgeni rasmi katika chakula hicho cha mchana alikuwa Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin ambaye alileta kwa wote waliohudhuria salamu na matashi mema ya Papa Francisko. Kardinali huyo alizungumzia kurudi, tena hali ya kawaida akikumbuka kuwa alihudhuria chakula cha mchana cha Jumuiya mwaka 2015. Lakini daima ni jambo nzuri sana na la kusisimua, alisema, kuona watu hawa wote pamoja kusherehekea Noeli, jambo ambalo linagusa moyo. Kardinali Parolin alionesha matamanio kwamba uzoefu huu unaweza kurudiwa na kuzidishwa, kwa sababu tunahitaji sana mshikamano na upendo katika ulimwengu wetu. Noeli inatukumbusha hili, suluhisho pekee la matatizo yetu ni kuwa makini na kuwa karibu na wengine, hasa wale wanaoteseka na kujikuta katika matatizo.
Papa anatupatia mfano huu kila siku, tunajaribu kumfuata kwa njia nyingi, lakini tunajaribu kuifanya dunia yetu kuwa bora kidogo. Karibu na Kardinali walikuwapo Anna na Pamela, mama na binti kutoka Siria na Aleppo ambapo wako nchini Italia, shukrani kwa mikondo za kibinadamu zilizoandaliwa na Jumuiya Mtakatifu Egidio pamoja na Baraza la Maaskofu Italia (CEI) na Makanisa ya Kiinjili. Kutoka kwao, ushuhuda mfupi "muhimu wa kuzaliwa kwa upya na ushirikiano ambapo kiukweli Vita ni jambo baya sana, hebu tuwe na matumaini kwamba itaisha mapema. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iliokoa maisha yetu, ndoto yetu ilikuwa kuishi kwa amani,” alisema Bi Anna.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio Bwana Marco Impagliazzo alibainisha juu ya furaha yao kuwa wanawakaribisha maelfu ya watu nchini Italia na duniani kote na kuketi nao mezani kwa sababu ni chakula cha mchana ambacho kuna anayetumikia na anayetumikiwa. Naye Meya wa mji Bwana Roberto Gualtieri, pia alizungumza na kuishukuru Jumuiya hiyo kwa mpango huu ambao, alisisitiza, kuwa unaendeleza wazo la mshikamano, ushirikishwaji, na ukarimu. Wazo msingi ambalo Roma alisema, lazima liwe daima katika moyoni mwake na kufanyiwa matendo ya dhati. Hatimaye salamu ya paroko, Padre Marco Gnavi, ambaye aliwaita baadhi ya wageni. Miongoni mwao, Armando na Iolanda, umri wa miaka 97, aliyekuwa kiukweli mkubwa wa meza, Celeste kutoka Nigeria na Jubile, ambaye alikuwa na familia yake kwa miezi kadhaa katika kambi ya wakimbizi huko Lesvos. Baada ya kumaliza salamu hizo basi chakula cha mchana kilianza. Maandalizi yote ni utamaduni wa chakula cha kiitaliano kiitwacho 'Lasagna', mkate wa nyama, dengu na vinywaji kawaida vya Siku Kuu ya Kuzaliwa kwa Bwana ambavyo ni msingi wa menyu. Kisha zilitolewa zawadi (kwa kila mtu, kama katika familia, zawadi iliyo na jina la kila mgeni), wakati wa kushirikishana na udugu.
Kwa mujibu wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inabainisha kuwa Tukio la mwaka huu pia linalenga kutangaza ujumbe wa matumaini katika wakati ulioangaziwa na mgogoro na vita nchini Ukraine. Miongoni mwa wageni, wengi walikuwa wakimbizi wa Ukraine, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wao, ambao walikimbia wakati wa kuzuka kwa vita tarehe 24 Februari mwaka huu. Chakula cha mchana katikati ya Roma sio mipango pekee ya Noeli. Mipango mingine mingi, ikiwa ni pamoja na matukio ya wafungwa, iliandaliwa kwa jina la mshikamano na ilifanyika kwa wakati mmoja katika miji mia moja ya Italia na duniani kote. Mbali na Ulaya, pia Asia, Afrika na Amerika ya Kusini. Tarehe 26 Desemba, chakula cha mchana kimeandaliwa katika gereza kubwa la Rebibbia, katika jengo jipya jijini Roma ambapo wafungwa 410 wameketi kwenye meza pamoja kula chakula cha mchana.