Tafuta

Kardinali Mauro Piacenza: Waamini jiandaeni kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa toba na wongofu wa ndani, kwa kutubu na kuungama dhambi zenu. Kardinali Mauro Piacenza: Waamini jiandaeni kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa toba na wongofu wa ndani, kwa kutubu na kuungama dhambi zenu. 

Wakristo Jiandaeni Kusherehekea Noeli Kwa Kufanya Toba, Wongofu na Upatanisho

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume katika barua yake kwa Mapadre waungamishaji kwa Mwaka 2022, anawataka wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wadhambi wanaokimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, ili hatimaye, waweze kukutana mubashara na Kristo Yesu anayezaliwa tena nyoyoni mwao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa katika maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, anapata mwanga wa pekee katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho, ili Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu anayezaliwa aweze kuwatakasa, kuwakomboa na kuwapyaisha, ili hatimaye, Kristo Yesu aweze kuzaliwa tena katika nyoyo za waamini wanaotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ingawa Kanisa ni takatifu, lakini daima linahitaji kutakaswa, kwa kumwangalia Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama asiye na doa “Tota Pulchra”, ambaye alibahatika kupata neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuwafungulia watu, Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kukaa kati ya waja wake kwake yeye Bikira Maria. Mama Kanisa daima anafurahia utakatifu na utukufu wa Bikira Maria asiyekuwa na doa la dhambi, ambaye daima anawaombea watoto wake, ili waweze kupata neema ya utakaso kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, kwa kujichotea neema kutoka katika chemchemi ya upendo na huruma ya Mungu yaani ubinadamu wa Mwana wa Mungu, ambaye alimwaga Damu yake Azizi katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Sakramenti ya Upatanisho iwaletee upatanisho na Mungu na jirani
Sakramenti ya Upatanisho iwaletee upatanisho na Mungu na jirani

Maungamo ya dhambi ni ushuhuda wa pekee kabisa unaowapatia waamini nafasi ya kujipatanisha na Baba wa milele pamoja na jirani zao; kwa njia ya Kristo Yesu aliyewakomboa na kuwapyaisha tena kwa neema ya Sakramenti ya Ubatizo, inayowashirikisha waamini maisha ya Kristo Yesu na hivyo kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili uliozaliwa na Bikira Maria “Verum Corpus natum de Maria Virgine.” Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, Mama Kanisa anajipatia tena watoto wapya, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, aliyezaliwa kwenye Pango la kulishia wanyama mjini Bethlehemu, ambako watu wengi wanamsubiria ili waweze kumpokea tena katika maisha yao. Mtoto Yesu aliyezaliwa Pangoni, anaendelea kutawala katika moyo wa Padre muungamishaji, akiendelea kusubiria muungamaji anayekuja kutubu ili kumwonesha ile sura ya Mwana wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume katika barua yake kwa Mapadre waungamishaji kwa Mwaka 2022, anawataka waungamishaji kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wadhambi wanaokimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, ili hatimaye, waweze kukutana mubashara na Kristo Yesu anayezaliwa tena nyoyoni mwao.

Sakramenti ya Upatanisho iwaonjeshe waamini huruma na upendo wa Mungu
Sakramenti ya Upatanisho iwaonjeshe waamini huruma na upendo wa Mungu

Mapadre waungamishaji kwa njia ya Kristo Yesu kupitia kwa Mitume wa Yesu, wamepewa dhamana na wajibu wa kuwaondolea waamini dhambi zao, ili hatimaye, waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu. Watambue kwamba, kuna waamini ambao bado ni wachanga sana katika imani. Kumbe, watambue hali yao na kuwasaidia kuonja huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na hivyo kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake anayeendelea kutenda kazi kwa njia ya Sakramenti zake. Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia kwenye Kiti cha huruma ya Mungu, ili kujiandaa barabara kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa upya katika maisha na vipaumbele vyao. Busara, hekima pamoja na umuhimu wa kusoma alama za nyakati vitumike kwa ajili ya kuwasaidia waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho, ili waamini wanaofika kutubu na kumuungamia Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ili waweze kuonja uwepo wake wa daima. Sakramenti ya Upatanisho iwe ni fursa kwa waamini kukutana mubashara na Kristo Yesu anayewasaidia waja wake kupyaisha tena imani yao.

Sakramenti ya Upatanisho: Huruma na upendo wa Mungu
Sakramenti ya Upatanisho: Huruma na upendo wa Mungu

Sakramenti ya Upatanisho inamwezesha Padre muungamishi: Kufundisha kweli za Kiinjili, Kuongoza kwa kuwapatia ushauri wa kimaadili na maisha ya kiroho na Kutakatifuza kwa kuwaondolea waamini dhambi zao. Licha ya ukame wa miito na wa Mapadre sehemu mbalimbali za dunia, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Majandokasisi katika malezi na makuzi yao wapatiwe mambo msingi kwa ajili ya maisha na utume wao wa Kipadre. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume anawatakia Mapadre waungamishaji mchoko mtakatifu, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaondolea waamini dhambi zao. Ni katika Mahakama ya Huruma ya Mungu, mwamini anaweza kupata amani ya kweli.

Ujumbe wa Toba
21 December 2022, 14:20