Papa amemteua Mwenyekiti mpya wa Baraza la Makanisa ya Mashariki
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumatatu tarehe 21 Novemba 2022, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, Askofu Mkuu Claudio Gugerotti, ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Ravello. Hadi uteuzi huo alikuwa Balozi wa Vatican Nchini Uingereza na ambaye ataanza utume huo katikati ya mwezi Januari 2023. Atashika nafasi ya Kardinali Leonardo Sandri. Askofu Mkuu Claudio Gugerotti alizaliwa huko Verona mnamo mwaka 1955. Alijiunga katika Jumuiya ya Wachamungu wa Padre Nicola Mazza, na akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mnamo tarehe 29 Mei 1982 kwa ajili ya Jimbo la Verona. Katika masomo yake ya juu ana digrii katika lugha za mashariki na fasihi katika Chuo Kikuu cha "Ca' Foscari" cha Venezia na leseni ya liturujia katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmi,Roma (Kitengo cha Mtakatifu Giustina huko Padua) na udaktari katika sayansi za kikanisa za Nchi za Mashariki katika Taasisi ya Kipapa ya Mashariki.
Pamoja na mengine amejikita katika shughuli za ufundishaji, katika Vyuo Vikuu vya Venezia, Padua na Roma, katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriana na Taasisi ya Kipapa ya nchi za Mashariki. Mnamo Mwaka 1985 alianza huduma yake katika Baraza la Kipapa la Nchi za Mashariki. Mnamo 1997 alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Baraza hilo. Kuanzia mwaka 1990 hadi 2001 alikuwa mshauri wa Ofisi ya Maadhimisho ya Kiliturujia ya Kipapa. Baadaye kwa kuchaguliwa kuwa Askofu mkuu wa Ravello mnamo Desemba 2001, akawa Balozi wa Vatican huko nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan. Alipewa daraja la uaskofu katika mikono ya Mtakatifu Yohane Paulo II mnamo tarehe 6 Januari 2002. Mwaka 2011 akateuliwa kuwa Balozi wa Vatican, huko Belarus, mnamo mwaka 2015 nchini Ukraine na mwaka 2020 huko Uingereza.
Yeye pia ni mwandishi vitabu kama vile: Santo per gioco,yaani Mtakatifu kwa mchezo. Wasio na mwisho wa Mtakatifu Francis (Vicenza 1984); tafsiri kutoka kwa Kiarmenia, pamoja na utangulizi na maelezo ya Historia ya Sebēos (Verona 1990); Mwingiliano wa majukumu katika sherehe kama fumbo; Wazo la Nersēs Lambronac'i katika "Ufafanuzi wa sadaka" (Padova 1991); tafsiri kwa Kiarmenia, utangulizi na maelezo ya Mti wa Uzima na Gregory wa Narek (Bose 1994); Liturujia ya Kiarmenia ya kuwekwa wakfu na enzi ya Kilician. Matokeo ya ibada ya taalimungu ya umoja kati ya Makanisa (Roma 2001); Mtu mpya kiumbe wa kiliturujia (Roma 2005), pia kilitafsiriwa katika Kiromania na Kiukreni, Caucasus na mazingira (Roma 2012) na Mwonekano wa Mashariki (Bose 2012), pamoja na makala na insha mbalimbali.