Papa amehuzunishwa na kifo cha mwanaume katika nguzo za Bernin Vatican
Na Angella Rwezaula; – Vatican
Ijumaa asubuhi tarehe 25 Novemba 2022 katika nguzo za Bernini mjini karibu na uwanja wa Mtakatifu Petro, amekutwa mwanaume mmoja hasiye na makazi amefariki dunia. Inawezekana amekufa kwa sababu ya baridi ambayo kwa siku hizi imekuwa kali na mvua hasa kwa wale ambao maisha yao na hali yao wamelazimika kukaa nje kwa kuwa hawana makazi. Ni mmoja wa maskini kati ya maskini ambao kawaida hutafuta namna ya kujikinga na bari katika siku za baridi na mvua. Kwa wapita njia hakukosa ambaye alisimama na kusali au hata kupita mwili huo ambao uliwekewa hata mshumaa kabla ya polisi kufika hapo kuutoa.
Lakini pamoja na hayo huyo mwanaume alikuwa na sura na jina. Kwa mujibu wa Msemaji wa vyombo vya habari Vatican, Dk. Matteo Bruni, akijibu maswali ya wahandishi wa habari alisema “huyo Bwana anaitwa Burkhard Scheffler, aliyezaliwa mnamo 1961 huko Ujerumani. Amekuwa akisia barabarani jijini Roma lakini akifuatiliwa na shughuli za utunzaji wa Baraza la Kipapa la Upendo. Kwa bahati mbaya, katika siku hizi za baridi na mvua, inawezekana zimeongezea udhaifu wake wa hali ya kiafya”
Kwa maana hiyo Dk. Bruni ameongeza kusema kwamba “katika sala ya Baba Mtakatifu anamkumbuka Burkhard na wale wote ambao wanalazimika kuishi bila nyumba ya kukaa jijini Roma na ulimwengu mzima na kuwaalika waamini kuungana naye”. Aidha amesema kwamba “kwa upande wa Mkuu wa Sadaka ya Kitume Kardinali Krajewski, ambaye yuko Assisi katika hija, amemkabidhi Burkhard kwa maombezi ya Mtakatifu Francis wa Assisi”.
Kwa wale ambao walikuwa wanapita njia, bila shaka hata kama walikuwa hawajuhi jina lake mara kadhaa hyo baba alikuwa anaketi kwenye nguzo akiwa ameshikilia kitabu anasoma kwa sauti ya juu kwa lugha la kijerumani. Alikuwa na vitu vichache lakini kitabu chake hakikosa kamwe mikononi mwake na karibu naye akiwa na vifuniko vya mabox. Katika hali hiyo kweli ni uwakilishi wa walio wengi sana jijini Roma ambao hawana mahali pa kulala.