Tafuta

Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, “Propaganda fide” wakati ule wa mwaka 1622 Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, “Propaganda fide” wakati ule wa mwaka 1622 

Changamoto za Uinjilishaji wa Kina Nchini Tanzania! Imani Haba!

Askofu mkuu Damian Denis Dallu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kielelezo cha ukomavu wa imani. Uhaba wa imani unaojionesha pale waamini wanapokabiliana na changamoto mbalimbali katika hija ya maisha yao, kwa kutafuta miujiza ya uponyaji kutoka kwa manabii wa uwongo. Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni iliyoadhimishwa tarehe 23 Oktoba 2022 ulinogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Anasema Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, “Propaganda fide” wakati ule wa mwaka 1622. Alikuwa ni Papa Gregori wa XV tarehe 6 Januari 1622 katika Waraka wake wa Kitume wa “Inscrutabili Divinae Providentiae” akitamani kuwaunganisha Wakatoliki na Waamini wa Makanisa ya Kiprotestanti pamoja na kukoleza ari na mwamko wa uinjilishaji wa awali. Chimbuko lake ni ile hamu ya kutekeleza Agizo la Kimisionari la kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.  Mwenyeheri Pauline-Marie Jaricot (1799-1862) ndiye muasisi Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari, dhamana aliyoitekeleza kwa muda wa miaka 15 bila kuchoka! Aliteseka sana kiroho na kimwili, lakini akaimarishwa kwa Sakramenti za Kanisa sanjari na mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na sadaka ya maisha yake. Mwenyeheri Pauline-Marie Jaricot akajipambanua katika huduma kwa Mungu na jirani maskini na wagonjwa. Ari na moyo wake wa kimisionari bado unaendelea kupenya sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya misaada ya hali na mali katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Jubilei ya Miaka 400 ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu
Jubilei ya Miaka 400 ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu

Kumbe, Mwaka 2022, Mama Kanisa anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha miaka 200 ya imani na uinjilishaji sehemu mbalimbali za dunia. Mama Kanisa anawakumbuka pia mashuhuda wa imani kama vile Askofu Charles de Forbin-Janson kutoka Ufaransa aliyeanzisha Shirika la Utoto Mtakatifu ili kuhamasisha mchakato wa uinjilishaji miongoni mwa watoto wadogo. Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwa Mwenyeheri Paulo Manna, Muasisi wa Shirika la Umoja wa Kimisionari, unaopania kuchochea karama na roho ya kimisionari, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ni matamanio halali ya Baba Mtakatifu Francisko kuona Wakristo wote wakiwa ni Manabii na Mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Kwani wito wa kila Mkristo ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kiini cha mafundisho ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye aliyetumwa wa kwanza kuwa “Mmisionari” na “Shuhuda” wa Baba wa milele.

Waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania wanapaswa kusimama imara katika imani
Waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania wanapaswa kusimama imara katika imani

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuanzia tarehe 12-13 Novemba 2022, limeendesha Kongamano la Kitaifa kama sehemu ya Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu 1622-2022 sanjari na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa watoto pamoja kuendeleza mchakato wa malezi na makuzi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Kongamano hili limewashirikisha watu wa Mungu kutoka katika Majimbo 34 yanayounda Kanisa Katoliki Tanzania. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko alituma ujumbe wa pongezi na matashi mema katika maadhimisho haya. Ibada ya Misa Takatifu kilele cha Jubilei ya Miaka 400 ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu iliongozwa na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC na Mahubiri kutolewa na Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Imani haba ni chanzo cha kutafuta miujiza na uponywaji wa nguvu
Imani haba ni chanzo cha kutafuta miujiza na uponywaji wa nguvu

Askofu mkuu Damian Denis Dallu katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kielelezo cha ukomavu wa imani. Uhaba wa imani unaojionesha pale waamini wanapokabiliana na changamoto mbalimbali katika hija ya maisha yao, kwa kutafuta miujiza ya uponyaji kutoka kwa manabii wa uwongo. Amekazia umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha waamini: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ubatizo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, kuna haja ya kukazia malezi na makuzi ya mihimili ya uinjilishaji.  Askofu mkuu Damian Denis Dallu amegusia umuhimu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari kama sehemu ya mchakato wa ukombozi wa mtu mzima kiroho na kimwili kwa kujikita katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Matunda ya kazi hii ni kumbukizi ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara yaliyozinduliwa Jimbo Katoliki Bukoba tarehe 1 Oktoba 2016 na kuhimishwa Bagamoyo, Lango la Imani mwaka 2018. Pamoja na umuhimu wa kurekebisha Sheria kuhusu Taasisi za Kidini, ili kutoa nafasi kwa wamisionari kuchangia zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Dhamana na wajibu wa Kanisa la Kimisionari ni Ukombozi wa Mtu Mzima: Kiroho na Kimwili. Ametoa onyo kwa viongozi wa Kanisa na Mashirika ya Kitawa nchini Tanzania yanayoendesha huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo isigeuzwe na kuwa ni bishara, bali sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini. Kanisa litaendelea kusimama kidete katika mafundisho yake kuhusu imani, maadili na utu wema.

Kuna mafanikio makubwa ya Propaganda Fide katika kipindi cha Miaka 400
Kuna mafanikio makubwa ya Propaganda Fide katika kipindi cha Miaka 400

Naye Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Tanzania kwa ushiriki wao katika maadhimisho haya. Lakini, kwa namna ya pekee kabisa, ameupongeza Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania kwa kuonesha ushirikiano na mshikamano kati ya Ubalozi na Sekretarieti kuu ya Vatican, ambayo imeatambua na kuthamini maadhimisho haya kiasi cha Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kutuma ujumbe wa pongezi na matashi mema katika maadhimisho haya. Hiki ni kielelezo cha ushirika na umoja wa Kikanisa ulivyo imarika na unavyokusudia ustawi, maendeleo na mafao kwa Taifa la Mungu nchini Tanzania. Miaka 400 ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ni kipindi kirefu kinachoonesha mafanikio katika medani mbalimbali ya maisha ya watu wa Mungu. Huu ni mchango thabiti wa watu mbalimbali waliokwisha kufariki dunia na wale ambao bado wako hai. Ni mafanikio ambayo yanagusa undani wa mtu mzima: kiroho na kimwili katika mapambano dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi, maadui wakuu wa mchakato wa maendeleo fungamani ya mwanadamu.

Wekezeni kwenye mihimili ya uinjilishaji nchini Tanzania
Wekezeni kwenye mihimili ya uinjilishaji nchini Tanzania

Huu ni wakati wa kuanza kujiandaa kwa ajili ya Jubilei ya Miaka 1000 ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kwa kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu asitawishe na kudumisha jitihada za mchakato wa uinjilishaji kwa ajili ya mihimili yote na kwamba, kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, anakaza kusema, ni jukumu la watu wa Mungu kujenga na kuimarisha mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Waamini wajikite katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili watu wa Mungu waweze kupata furaha ya Injili na hatimaye, waweze kufika mbinguni kwa Baba wa milele. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeanza kutia nia ya ujenzi wa Makao makuu ya Baraza Jijini Dodoma alidokeza Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye tarehe 23 Novemba 2022 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Kongamano 400 Yrs
23 November 2022, 17:09