Ziara ya mwakilishi wa Vatican huko Algeria ni ishara ya umakini wa zizi dogo
Na Angella Rwezaula; - Vatican
Makaribisho makubwa yalitolewa huko Algeria kwa ajili ya Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa. Askofu Mkuu huyo kwa muda wa siku mbili nchini humo wakati wa kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Algeria na Vatican, kati ya wengine aliweza kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo, ambapo tarehe 26 Oktoba alikwenda kwenye makao ya wamonaki wa Thibirine, mahali ambapo waliuawa watawa 7 wa Kitrappist mnamo 1996 na wapiganaji wa Kiislamu na kutangazwa wenyeheri mnamo 2018 huko Oran. Askofu Jean Paul Vesco, wa Jimbo Kuu Katoliki la Algeris akikamribisha uwepo wake katika Jumuiya iitwayo “Safari mpya” inayomilikiwa sasa na mosteri hiyo, alisema ni hatua ambayo monasteri hiyo ni muhimu kwa Kanisa na pia ilikuwa wakati wa kumbukumbu, wakati wa amani na uzoefu wa nguvu kwa wale wote wanaokwenda mahali hapo, kwenye monasteri hiyo na kuhisi uwepo wa watawa hapo.
Kwa askofu mkuu wa Algiers, aliyemkaribisha Katibu wa Mahusiano na Mataifa katika siku mbili zilizopita alisema ni ishara ya umakini kwa Wakatoliki walio wachache nchini. Humo na kuwapa matumaini. Siku ya Jumanne tarehe 25 Oktoba 2022 , Askofu Mkuu Gallagher alipokelewa na mkuu wa nchi, Bwana Abdelmadjid Tebboune, baada ya siku ya mazungumzo na wajumbe wa serikali na kutembelea Makumbusho ya Mashahidi, mnara uliojengwa kwa ajili ya kumbu kumbu ya wahanga wa vita vya uhuru dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa. Kwa upande wa mazungumzo ya kidini, Askofu Mkuu Gallagher pia alikutana na Sheikh Mohamed Mamoune El Kacimi El Hassini, mkuu wa msikiti mkubwa wa Algiers, anayejulikana kuwa mtu wa ridhaa na uwazi, ambapo leo hii yuko katika usukani wa msikiti mkubwa zaidi barani Afrika.
Askofu mkuu wa Algiers alizungumza juu ya kutembelea nafasi kubwa takatifu na ya Umoja. Kwa upande wake Askofu Mkuu Vesco alisema mabadilishano haya ni muhimu sana, kwani wanapenda kuwakaribisha watu katika maeneo matakatifu, watu wanapenda kwenda kwa Notre Dame d'Afrique,yaani Mama Yetu wa Afrika huko Algiers, Notre Dame Santa-Cruz yaani Mama wa Msalaba Mtakatifu huko Oran, Kanisa Kuu la Mtakatifu Augustino huko Annaba. Kushirikishana nafasi takatifu, alisema, hata bila kusema lolote tayari inaeleza mengi zaidi, labda kuhusu ukweli unaoishi katika kila mila na dini zao.
Ziara ya Askofu Mkuu Gallagher ilikuja chini ya mwezi mmoja baada ya kufungwa kwa Caritas Algeria, kama walivyoombwa na mamlaka ya umma. Kanisa Katoliki la eneo hilo liliheshimu uamuzi huo, huku likieleza wasiwasi wake, pamoja na nia yake ya kuendelea kuwasaidia watu wasiojiweza na watu wa Algeria. Kwa maana hiyo “Kuwepo huko Algiers kwa mwakilishi wa Papa na kufungwa kwa Caritas ni matukio mawili tofauti”, alisema Askofu Mkuu Jean Paul Vesco.
Hata hivyo, “ziara hii yenyewe, bila kujali kufungwa kwa huduma yetu ya Caritas, kiukweli inaangaza njia ya matumaini”. Suala hilo kwa hakika lilijadiliwa, na askofu mkuu anakiri, lakini ilitokana na ukosefu wa uelewa kutokana na ukosefu wa mawasiliano kwa pande zote mbili kuhusu Caritas maana yake ni nini katika ngazi ya kimataifa na Algeria. Huduma ya Caritas haitafunguliwa tena, lakini imehakikishiwa kwamba shughuli za upendo za kibinadamu za Kanisa zitaweza kuendelea na hii inawahakikishia ukamilifu zaidi”.