Papa Francisko tarehe 2 atasali katika Makaburi ya Vatican
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tarehe 2 Novemba 2022, siku ambayo Mama Kanisa anawakumbuka waamini waliotutangulia mbele ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa na muda wa kusali sala katika makaburi yaliyomo jijini Vatican. Sala hiyo itafanyika karibu saa 6.30, majira ya Ulaya mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu ambayo Baba Mtakatifu ataadhimisha kwenye Altare ya Kanisa Kuu la Mtakatifu petro mjini Vatican. Na wakati huo siku itakayofuata tarehe 3 Novemba 2022, Baba Mtakatifu anatarajia kufanya ziara yake ya kitume ya 39 kwenda huko Bahrain.
Mwaka 2021 Baba Mtakatifu aliongoza Misa kama hiyo katika Makaburi ya Kijeshi ya Ufaransa jijini Roma. Wakati, mnamo 2020, Papa Francisko alikuwa ameadhimisha kumbukumbu ya wafu katika Kanisa la Chuo cha Kipapa cha Teutonic cha Mtakatifu Maria, Camposanto, Vatican. Mara baada ya hapo alikwenda kusali katika Groto mbele ya makaburi ya marehemu mapapa waliomtangulia.