Tafuta

Radio Vatican ilianzishwa mwaka 1931 na Mhandisi Guglielmo Marconi na kuwekwa chini ya maombezi na ulinzi wa Malaika Gabrieli ili kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili. Radio Vatican ilianzishwa mwaka 1931 na Mhandisi Guglielmo Marconi na kuwekwa chini ya maombezi na ulinzi wa Malaika Gabrieli ili kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili. 

Miaka 30 ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican: Pongezi Kwa Utume Uliotukuka Katika Uinjilishaji!

Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma anasema, Mama Kanisa anapowapongeza na kuwashukuru wadau katika Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, anawakumbuka pia wafanyakazi wote waliojisadaka na kujitosa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya lugha ya Kiswahili. Ni wakati wa kuwekeza zaidi katika ...!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 sanjari na Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni unanogeshwa kwa kauli mbiu: “Zungumzeni Ukweli Katika Upendo”: “Veritatem facientes in caritate.” “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Efe 4:15. Katika ulimwengu mamboleo, habari imekuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha ya kila siku. Habari hizi zikiwa zimeandaliwa kwa ubora na umakini mkubwa zinawasaidia watu wa Mungu kuweza kutambua matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika jamii inayowazunguka. Huu ni mwaliko kwa kila mtu na jamii katika ujumla wake kufanya upembuzi yakinifu mintarafu tabia na mwenendo wa mtu binafsi, ndugu na jamii husika, tayari kushiriki katika mchakato wa kuunda dhamiri nyofu, mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anapatumia kuongea na waja wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa vinapaswa kusaidia malezi na makuzi ya Jumuiya za Kikristo, ili ziweze kujielekeza zaidi katika mtindo bora zaidi wa maisha, unaowajumuisha na kuwashirikisha watu wote pasi na ubaguzi au kwa kuathirika na maamuzi mbele.

Tarehe 27 Septemba 2022: Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, miaka 30.
Tarehe 27 Septemba 2022: Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, miaka 30.

Inasikitisha kuona kwamba, watu wanajikita zaidi katika tabia ya kupika majungu. Ikumbukwe kwamba, "wambea hawana bunge na wala umbea si mtaji na kama ungekuwa mtaji wangetajirika wengi”. Umbea unafunga nyoyo za Jumuiya na umoja wa Kanisa. Shetani, Ibilisi ni “mpika majungu nambari one”, anayetembea hapa na pale akipepeta mdomo kwa kuzungumza mabaya ya watu wengine, kwa sababu ni mwongo anayetaka kupandikiza mbegu ya utengano ndani ya Kanisa, kwa kuwasambaratisha ndugu ili wasijenge Jumuiya. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mawasiliano ni utume muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Wakristo wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika nyanja za mawasiliano ya jamii wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Injili. Kwa weledi wake, mwanahabari Mkristo anapaswa kutoa ushuhuda uliopyaishwa katika ulimwengu wa mawasiliano bila kuficha ukweli wala kuchakachua habari. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao ukweli wa historia ya Habari Njema ya Wokovu. Hizi ni historia zinazowajenga watu badala ya kuwaporomosha; zinawasaidia watu kugundua asili yao na nguvu zinazohitajika ili kusonga mbele. Hata katika makelele na ujumbe mwingi, bado kunahitajika historia ya binadamu inayomzungumzia binadamu mwenyewe na uzuri unaomzunguka. Ni historia inayouangalia ulimwengu sanjari na yote yanayoendelea kutendeka kwa jicho jema.

Pongezi na Shukrani kwa kazi kubwa ya Idhaa ya Kiswahili kwa Miaka 30
Pongezi na Shukrani kwa kazi kubwa ya Idhaa ya Kiswahili kwa Miaka 30

Radio Vatican ilianzishwa mwaka 1931 na Mhandisi Guglielmo Marconi na kuwekwa chini ya maombezi na ulinzi wa Malaika Gabrieli. Radio Vatican inarusha matangazo yake katika lugha 47 na kati ya lugha hizi ni Kiswahili ambacho kinaendelea kuchanja mbuga sehemu mbalimbali za dunia. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ilianzishwa rasmi tarehe 27 Septemba 1992, ndiyo maana mwaka 2022 inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, tukio ambalo limeadhimishwa kwa kishindo tarehe 29 Septemba 2022 sanjari na Sikukuu ya Malaika Wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli. Lakini itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 6 Novemba 1961, Mtakatifu Yohane XXIII alipozindua matangazo ya Radio Vatican kwa Bara la Afrika na majira ya jioni saa 11:15 matangazo kwa lugha ya Kiswahili yalirushwa kwa mara ya kwanza na yalikuwa yanaandaliwa na Shirika la Wamisionari wa Afrika, WF., kwa wakati huo. Matangazo haya kwenye miaka 1970 kutokana na sababu mbalimbali hayakuweza kuendelezwa, hadi kufikia tarehe 27 Septemba 1992.

Padre Richard Mjigwa Alitunukiwa nishani ya "Pro Ecclesia et Pontefice"
Padre Richard Mjigwa Alitunukiwa nishani ya "Pro Ecclesia et Pontefice"

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican mwaka 2022 inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake rasmi. Ni katika muktadha huu, Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anasema, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ni chombo cha Kanisa kinachojihusisha kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, ambacho tarehe 27 Septemba 2022 kimeadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake. Huu ni umri wa kutosha, unapaswa kusifiwa, kutukuzwa na kuheshimiwa na kwamba, kwa hakika kazi kubwa imetendeka katika kipindi hiki cha miaka 30 na matunda yanaonekana. Injili imetangazwa na kushuhudiwa; Imani imelindwa na kuenezwa kwa lugha ya Kiswahili kinachotumiwa na watu zaidi ya milioni 200, wengi wao wakiwa ni watu wa Mungu kutoka Eneo la Maziwa makuu. Kiswahili wanasema ni “lingua franca kwa Bara la Afrika.” Askofu Michael George Mabuga Msonganzila anasema, Mama Kanisa anapowapongeza na kuwashukuru wadau katika Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, anawakumbuka pia wafanyakazi wote waliojisadaka na kujitosa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya lugha ya Kiswahili.

Kwa namna ya pekee, anakumbukwa Mama Thabita Janet Mhella na Padre Thomas Namwaga ambao walihudumu kwa muda mrefu zaidi; Padre Albadus F. Kidavuri aliyekuwa anaanda Kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu kati ya mwaka 2007-2009, RIP. Wengine ni pamoja na Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa ujana wake masomoni mjini Roma, alishiriki kuandaa vipindi vya vijana; Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki la Kondoa.Wanakumbukwa pia Askofu mstaafu Jacob Venance Koda wa Jimbo Katoliki la Same, Padre Padre Anacletus Ngenza wa Jimbo Katoliki la Kigoma. Hawa ni “vigogo” waliweka msingi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. Kuna Mapadre na watawa wengi ambao wameshiriki katika huduma ya Idhaa ya Kiswahili katika kipindi chote, wote wanakumbukwa sana kwa kushiriki katika mchakato wa uinjilishaji kwa lugha ya Kiswahili.

Radio Vatican imdechangia utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu
Radio Vatican imdechangia utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika mkutano wake wa 41 uliofanyika mjini Paris, Ufaransa, tarehe 23 Novemba 2021 uliamua kwamba, tarehe 7 Julai ya kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani. Azimio hili lilipitishwa na wanachama wote wa UNESCO bila kupingwa. Waswahili kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakafurahia sana tamko hili, kwa Umoja wa Mataifa kuamua kutoa kipaumbele cha pekee kwa Lugha ya Kiswahili. Hii ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kutoka Barani Afrika kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na kutengewa siku maalum ya kuadhimishwa Kimataifa. Kiswahili kinatambulikana kuwa ni lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Bunge la Afrika. Lakini, ikumbukwe kwamba, Kiswahili ni kati ya lugha 10 za Kimataifa zinazozungumzwa na watu wengi duniani. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila, anasema, maadhimisho haya ni fursa ya kuiombea Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican iendelee kucharuka katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, liangalie uwezekano wa kuiwezesha Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa rasilimali fedha na wat una hatimaye, lione umuhimu wa kupanua shughuli zake nje ya Vatican na Italia katika ujumla wake. Ikiwezekana iwe ni mwakilishi maalum, ili kunogesha Habari Njema ya Wokovu na kuzima dukuduku ya makundi maalum ya watu, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji yam tu mzima kiroho na kimwili. Iwe ni fursa kwa habari kutoka katika Makanisa mahalia kusikika na wengi.

Askofu Msonganzila, Kiswahili 30 Yrs
02 October 2022, 15:26