Jubilei ya Miaka 50 ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Asia, FABC
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Paulo VI tarehe 27 Novemba 1970 kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa alianza Hija ya Kitume ya Siku tatu nchini Ufilippini, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu baada ya nchi hiyo kukumbwa na kimbunga kikali sana, kilichopelekea maafa ya watu na mali zao. Hii ilikuwa ni fursa kwa Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Asia kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro aliyekuwa amekuja kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo thabiti. Ni katika muktadha huu, Maaskofu Katoliki Barani Asia wakatia nia ya kuanzisha Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, ili kujenga na kudumisha umoja na ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Asia. Kumbe, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambao kwa mwaka 2022 unaadhimisha Miaka 60 tangu ulipofunguliwa rasmi tarehe 11 Oktoba 1962 na Mtakatifu Yohane wa XXIII, changamoto na mwaliko kwa watoto wa Mungu kutangaza na kushuhudia uaminifu wao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kongamano la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, huko Bangkok, kuanzia tarehe 12 Oktoba hadi 30 Oktoba 2022 limenogeshwa na kauli mbiu “Kutembea pamoja kama watu wa Asia” … na wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.” Mt 2:12.
Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, ndiye aliyemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika hitimisho la Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, huko Bangkok, nchini Thailand, Dominika 30 Oktoba 2022. Katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa watu wa Mungu Barani Asia kutembea kwa pamoja katika mchakato wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kwani hii ni sehemu ya utume wao mahususi. Mwenyezi Mungu anawaalika Wakristo Barani Asia kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; wanaodhulumiwa, kunyanyaswa na utu wao kusiginwa kwa sababu mbalimbali. Hii ni safari inayosimikwa katika huruma, upendo na uvumilivu; haki na huduma ya upendo. Kristo Yesu anasema: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yn 14:6. Kristo Yesu ni mwandani wa safari yao. Ni Emmanuel, Mungu pamoja na watu wake. Kama Kristo Kanisa Barani Asia linahamasishwa kutembea katika umoja kwa kushikamana na watu wote wa Mungu, Barani Asia.
Kwa upande wake, Kardinali Charles Maung Bo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, katika hotuba yake ya kufunga maadhimisho haya amekazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa Kanisa kuwekeza katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya, ili kupyaisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kanisa na kwa jamii, tayari kutekeleza dhamana na wajibu wao. Pili ni kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa kutambua kwamba, Bara la Asia limebarikiwa kuwa na waamini wa dini na madhehebu mbalimbali. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya watu wa Mungu Barani Asia. Hili ni Kanisa ambalo linapaswa kuwainjilisha vijana pamoja na mitandao yao kijamii, ili kuwajengea dhamiri nyofu, ili wasitumbukie na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Kanisa liwafunde vijana ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ni wakati wa kukuza na kudumisha misingi ya uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini.
Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1. Kardinali Charles Maung Bo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, anasema, Kanisa katika ukimya wake, ni chemchemi ya wokovu na matumaini kwa watu wa Mungu.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu Barani Asia linasema, Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake, kimekuwa ni kipindi muafaka cha kupyaisha maisha na utume wa Kanisa, kwa kujikita zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu. Kwa njia hii, Kanisa Barani Asia limepata mwanya wa: kusali, kusikilizana, kung’amua na kutiana shime ya kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya wa kimisionari. Kimekuwa ni kipindi cha uponyaji kutokana na madhara makubwa yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO, -19. Wajumbe wanaondoka wakiwa wamesheheni: matumaini na ujasiri wa kuendelea kutembea kwa pamoja, huku wakiwa wameshikamana, kama sehemu ya maboresho ya Bara la Asia. Hiki ni kipindi cha kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu Barani Asia kutokana na umaskini wa hali na kipato; dhuluma na nyanyaso dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa Barani Asia linapania kuendelea kuwashirikisha vijana na wanawake katika maisha na utume wake; kwa kuwa ni sauti yao makini. Kanisa linapenda kukemea misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga upendo na mshikamano wa watu wa Mungu Barani Asia; kwa kuendelea pia kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.
Ni wakati wa kusimama kidete kalinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa Barani Asia linapenda kusikiliza na kujibu changamoto zote hizi kwa kujikita katika nguvu ya upendo na huruma; haki na msamaha na kwamba, haki na msamaha ndiyo njia ambayo inapaswa kutekelezwa na Mama wa Kanisa. Utamaduni wa kusikilizana na kufanya mang’amuzi ya pamoja ndiyo njia ambayo Kanisa Barani Asia linapenda kuwekeza huko zaidi. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC., likiwa limesukumwa na tunu msingi za Kiinjili pamoja na Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, sasa wameamua kutoka kifua mbele kuwaendea wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; kuendelea kujikita katika toba, wongofu wa ndani na wa kiikolojia; kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ni wakati wa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato; biashara haramu ya binadamu, viungo vyake pamoja na mifumo yote ya ukoloni mamboleo. Ni wakati wa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa Barani Asia linahamasishwa kujenga utamaduni wa kusikilizana ili hatimaye, kwa pamoja waweze kusikiliza sauti ya Mungu, sanjari na uimarishaji wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.