“Sikukuu ya Mwanga” kwa waamini wa dini ya Kihindu inaadhimishwa kwa muda wa siku tano na kilele chake kwa mwaka 2022 ni tarehe 24 Oktoba 2022. “Sikukuu ya Mwanga” kwa waamini wa dini ya Kihindu inaadhimishwa kwa muda wa siku tano na kilele chake kwa mwaka 2022 ni tarehe 24 Oktoba 2022. 

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini: Sikukuu ya Mwanga 2022

Sikukuu ya Mwanga kwa Mwaka 2022: Kauli mbiu “Wakristo na Wahindu: Kukuza maisha na uwajibikaji wa pamoja.” Baraza linaonesha umuhimu wa kukuza umoja na uwajibikaji; uaminifu, mafungamano ya kijamii kwa ajili ya: utu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Pamoja na mchango wa familia katika kuwafunda watoto wao ili kukuza na kudumisha udugu na amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sikukuu ya “Deepavali” au “Diwali” “दीपावली,” yaani “Sikukuu ya Mwanga” kwa waamini wa dini ya Kihindu inaadhimishwa kwa muda wa siku tano na kilele chake kwa mwaka 2022 ni tarehe 24 Oktoba 2022. Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu “Wakristo na Wahindu: Kukuza maisha na uwajibikaji wa pamoja.” Baraza linaonesha umuhimu wa kukuza umoja na uwajibikaji; uaminifu, mafungamano ya kijamii kwa ajili ya: utu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Pamoja na mchango wa familia katika kuwafunda watoto wao ili kukuza na kudumisha udugu na amani duniani. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linasema, kukua na kupanuka kwa kinzani, migogoro na vurugu sehemu mbalimbali za dunia kwa misingi ya kidini, kitamaduni, kikabila; ni mambo ambayo yamekuwa yakichochewa na siasa za ushindani, tabia ya baadhi ya viongozi kutaka kujimwambafai katika jamii pamoja na matumizi mabaya ya njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Haya ni mambo yanayoathiri maisha ya pamoja katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu sanjari na amani ndani ya jamii. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha ushawishi na roho ya uwajibikaji kati ya watu wa Mataifa, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Wakristo na Wahindu: Kukuza maisha na uwajibikaji wa pamoja
Wakristo na Wahindu: Kukuza maisha na uwajibikaji wa pamoja

Waamini wa dini hizi mbili wajielekeze zaidi katika mchakato wa kudumisha uaminifu unaosimikwa katika urafiki na uwezo wa mtu kuishi na jirani zake kwa kuzingatia tofauti msingi, hali ya kuheshimiana na kuthaminina kama ndugu wamoja; tayari kulinda na kudumisha pia mazingira nyumba ya wote. Lengo ni kudumisha maisha bora yanayosimikwa kwenye mafungamano, ushirika na udugu. Waamini wa dini hizi mbili wanapaswa kujizatiti katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; huku utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kukazia umuhimu wa kufanya kazi. Waamini wajitahidi kujenga jamii inayosimikwa katika utu heshima na haki msingi za binadamu, na kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa, wabaki wakiwa wameungama na kushikamana kwa kuiga mifano ya watu wema waliowatangulia.

Sikukuu ya mwanga "diwali"
Sikukuu ya mwanga "diwali"

Familia zikiongozwa na mifano bora ya wazazi na wazee zina jukumu kubwa la kuwafundisha na kuwarithisha watoto na vijana maadili adhimu ya mafungamano ya kijamii. Mchango huu unapaswa kutolewa na wadau mbalimbali wenye dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanakuza na kudimisha maadili ya usikivu na uwajibikaji wa pamoja. Hii anasema Baba Mtakatifu Francisko ni ishara ya maongozi ya nyakati na njia ya upendeleo kwa ajili ya ukuaji wa udugu wa mshikamano na amani duniani. Hii ni njia yenye nguvu inayohamasisha na kutoa changamoto kwa watu wa mila, imani na dini mbalimbali kujitahidi kuyamwilisha katika maadili; udugu wa kibinadamu, umoja na mshikamamano kwa ajili ya mafao ya wengi. Waamini watambue kwamba jumuiya zao zimeegemezwa katika msingi wa imani na dini zao. Kumbe, wanapaswa kujali na kuwajibika kwa pamoja kwa ajili ustawi wa familia kubwa ya binadamu. Wakristo na Wahindu wakishirikiana na kushikamana kwa ajili ya ulinzi wa pamoja wa kazi ya uumbaji. Mapokeo, mila na desturi njema miongoni mwa Wakristo na Wahindu washikamane na kudumu katika hali ya uwajibikaji wa pamoja na mafungamano ya kijamii, ili Ulimwengu uweze kuwa ni makazi salama kwa kila mtu kuweza kuishi kwa amani na furaha.

Sikukuu ya mwanga 2022

 

 

24 October 2022, 15:34