Tafuta

Maadhimisho ya Kipindi cha kuombea kazi ya uumbaji yanasimikwa katika mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Maadhimisho ya Kipindi cha kuombea kazi ya uumbaji yanasimikwa katika mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka.  

AMECEA na Utunzaji Bora wa Mazingira: Kilele Cha Kipindi cha Mazingira 2022: Tamko!

AMECEA na Mazingira: Kanisa Katoliki kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tanzania imekuwa ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA, mwezi Julai 2022 ulionogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui yake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote ndiyo mada kuu iliyoongoza mkutano wa AMECEA kwa mwaka 2022. Kimsingi Waraka unazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki imeadhimishwa tarehe 1 Septemba 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Sikilizeni Kilio cha Kazi ya Uumbaji.” Siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015, kama sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, 2015-2016. Baba Mtakatifu aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, hawa ndio wale “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”

UTANGULIZI: Tamko hili linatolewa na Mkutano Mkuu wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Mashariki mwa Afrika uliofanyika Dar es Salaam Tanzania, uliohudhuriwa na Makardinali, Maaskofu Wakuu, Maaskofu na Wawakilishi mbalimbali kutoka nchi zote za AMECEA. Nchi hizo ni: Ethiopia, Eritrea, Kenya, Malawi, Tanzania, Uganda, Sudani, Sudani ya Kusini, Zambia na wajumbe waalikwa kutoka Djibouti, Somalia na washirika wa mabaraza hayo. Wajumbe wa Mkutano Mkuu huu walitafakari dhima kuu iliyoongozwa na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” inayozumgumzia Utunzaji wa Mazingira kama Nyumba yetu ya pamoja. Baba Mtakatifu anatumia utenzi wa Mtakatifu Francisko wa Assisi unaomsifu Mungu aliye muumbaji wa kila kiumbe (Dan 3:56-88).  Katika Waraka huo Baba Mtakatifu anakemea tabia ya mwanadamu ya kuchangia kuharibu mazingira.

Wongofu wa kiikolojia unatakiwa ili kutunza mazingira, nyumba ya wote.
Wongofu wa kiikolojia unatakiwa ili kutunza mazingira, nyumba ya wote.

Maneno ya Shukrani: Wakati wa mkutano mkuu tumetiwa moyo na maneno ya ufunguzi yaliyotolewa na Kardinali Luis Antonio Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambaye alisisitiza kwamba “tabia ya kutokujali watu wengine inaenda sambamba na tabia na mwenendo wa uharibifu wa uumbaji” na kwamba “kunapokesakana maendeleo ya mwanadamu kwa ujumla ule undugu wetu unapata mateso.” Tunatoa shukrani za dhati kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu, pia tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa ule utamaduni wa ukarimu na ushirikiano uliyopo kati ya Kanisa na serikali ambao tumeushuhudia na kuufurahia. Sisi  kama Maaskofu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Nchi za Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (AMECEA)  tunakiri kuwa licha ya taarifa ya mafanikio tuliyoshirikishana katika utekelezaji wa  ujumbe wa malengo ya Barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Laudato si;  katika ukanda huu,  wanachama wa Mabaraza ya Maaskofu wamekumbana pia na changamoto zinazohitaji mikakati mipya  ya kichungaji ili kwamba kwa dhana ya kukuza haki juu ya ikolojia  na kuzuia athari za mabadiliko ya tabia nchi, siyo tu iwe kwa maneno bali iwe ya matendo ili tuweze kusafiri kwa pamoja katika njia ya kubadilika kama inavyopendekezwa na   malengo saba ya Waraka wa Kitume ya Laudato si.

1) Hali ya mgogoro wa kiikolojia katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika: Tunakubali kwamba kuna mgogoro wa kiikolojia ambao kwa kiasi fulani unasababishwa na mwanadamu. Kwa kweli, mashindano ya kutafuta maliasili mara nyingi yamepelekea kutokea kwa mizozo na vita, vinavyofanya ‘kilio cha Mama Dunia (mazingira) na cha umaskini kuwa kikubwa zaidi. Katika kanda, mzozo wa kiikolojia sasa unathibitishwa na athari hasi za mabadiliko ya hali ya hewa ambayo ni pamoja na ukame, mafuriko na vimbunga, kati ya majanga mengine. Haya yote yanazidi kuwa tishio kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zetu na kwa mustakabali endelevu wa maisha ya watu katika ukanda huu.

Kuna mgogoro wa kiikolojia Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati
Kuna mgogoro wa kiikolojia Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati

2) Udhihirisho wa wasiwasi: Tunasikitishwa sana na kasi ya misitu yetu kutoweka haraka kutokana na matumizi ya kuni, uchomaji mkaa na kwa shughuli za ujenzi wa miundombinu huku wananchi wakiwa hawafanyi jitihada za kutosha za kupanda miti. Vile vile tunajali kuhusu matokeo hasi ya uchimbaji madini na ukosefu wa mifumo bora ya usimamizi wa taka. Tunafahamu kwamba kushughulikia masuala haya kunagusa haki ya kiuchumi na usawa. Kwa hivyo, haviwezi kushughulikiwa vya kutosha bila kuzingatia ipasavyo kutoa njia mbadala kama vile kukuza matumizi ya nishati ya jua na upepo na njia zingine za kujipatia riziki. Hata hivyo, haya yote yanachangia uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa mazingira katika eneo la ukanda wetu.

3) Pongezi: Baba Mtakatifu Paulo VI mara nyingi ananukuliwa kwa kusema kwamba “Watu wa kisasa husikiliza zaidi shuhuda kuliko waalimu, na ikiwa wanasikiliza walimu, ni kwa sababu wao ni mashuhuda” (Evangelii Nuntiandi, 1975). Kwa hiyo, tunalipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP- United Nations Environment Program), serikali, majimbo, vyama vya Kikatoliki, wanaume kwa wanawake na watu wote wenye mapenzi mema ambao tayari wamechukua hatua mbalimbali za kulinda viumbe hai kama vile upandaji miti na kusafisha miji. Hata hivyo, tunasisitiza hitaji la dharura la mifano zaidi katika ukanda wetu, mifano ambayo itaangazia Maisha na juhudi za kukabiliana na kilio cha Mama Dunia (mazingira).

4) Uhamasishaji: Tunarudia wito wa kampeni kali na makini za uhamasishaji katika ngazi ya msingi ya jumuiya, ili kuongeza uelewa na kuboresha mawasiliano yetu na watu kuhusu utunzaji wa mazingira katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na ngazi ya familia.

5) Elimu: Tunasisitiza jukumu la Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa Katoliki juu ya utunzaji wa mazingira na umuhimu wa kuunganisha shughuli za elimu-ikolojia na ikolojia katika programu za elimu kwa ajili ya kuwawezesha vijana na watoto katika shule zote na nyumba za malezi za makuhani na maisha ya Wakfu. Vijana wetu lazima waelimishwe ili wawe mabalozi wa uzoefu mzuri ya ikolojia.

Mababa wa AMECEA wanakazia wongofu wa kiikolojia na elimu makini.
Mababa wa AMECEA wanakazia wongofu wa kiikolojia na elimu makini.

6) Uhamasishaji wa jamii. Tunasisitiza haja ya Kanisa Katoliki katika eneo la AMECEA kushirikiana na serikali, madhehebu mengine na jumuiya za kidini, familia, sekta binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na taasisi za maendeleo ya kijamii na watu wenye mapenzi mema kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kubadilisha mitazamo ya watu kuhusu utunzaji wa mazingira.

 7) Utetezi: Tunasisitiza ushiriki wa Mabaraza ya Maaskofu (AMECEA) katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika kuendeleza jitihada za ushawishi na utetezi ili serikali zetu ziweze kutengeneza sera na sheria za utunzaji wa mazingira, ambazo zitazuia mazoea yenye athari hasi wakifanya hivyo kwa njia ya kuhamasisha ustawi wa watu wao.

8) Mwisho: Kwa kumalizia, Sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki ukanda wa Mashariki mwa Afrika tunajizatiti kuitika kilio kwa dunia na kilio cha maskini katika kutekeleza wajibu ule wa Mungu tuliokabidhiwa.  Mungu alipenda mwanadamu ailime ardhi na kuitunza (Mw. 2:15) na kwa kutambua mwito huu mkuu ninawahimiza wahudumu wote wa uchungaji wa Kanisa Katoliki na watu wote wenye mapenzi mema kuwa walinzi wa mazingira na rasilimali asili siyo tu kwa kizazi hiki bali pia kwa kizazi kijacho ambacho kwa niaba yao tunawajibu wa kuyaendeleza mazingira.

Amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu
Amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu

MSHIKAMANO: Tunapenda kuwahakikishia ndugu zetu kaka na dada katika ukanda wetu na kwingineko waliokumbwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabia ya nchi kama vile mafuriko kwamba hawapo peke yao. Katika moyo wa sala na kujali tunasimama nao katika mahangaiko yao. Sala zetu za kuombea amani tunazielekeza kwa mabaraza wanachama walio katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na mafarakano ikiwemo Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini na jamii zote zilizo katika mafarakano katika Bara la Afrika na kokote duniani. Mwisho tunawombea wenzetu wa Kenya wanaotarajia kuingia katika uchaguzi mkuu wa tarehe 9 Agosti 2022   ili uchaguzi huo uwe huru na wa haki na amani iweze kudumu.  Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibarikia AMECEA, Mungu awabariki ninyi nyote.

AMECEA na Mazingira
02 October 2022, 14:53