Rais wa Pwani ya Pembe Akutana na Kuzungumza na Papa Francisko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 17 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na Rais Alassane Ouattara wa Jamhuri ya Watu wa Pwani ya Pembe, “Ivory Coast” na baadaye, Rais amekutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa
Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu na mgeni wake, wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Baadaye wamezama zaidi katika masuala ya kijamii na kiuchumi, hasa katika mchakato wa umoja na upatanisho wa Kitaifa. Wamepongeza mchango unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini Pwani ya Pembe kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hususan katika sekta ya elimu na afya. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamebadilishana mawazo kuhusu masuala ya Kimataifa na Kikanda kwa kufanya rejea kuhusu jinsi hali ilivyo Magharibi mwa Afrika, Ukanda wa Sahel; Ulinzi na usalama katika eneo hili.