Papa Francisko amemtunukia Padre Mjigwa zawadi ya juu na wenzake
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baadaya ya miaka 6 tangu Mwandishi wa habari Thabita Janeth Mhella akiwa mwafrika wa kwanza kutunikiwa zawadi ya heshima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko mnamo tarehe 29 Septemba 2016, tukio kama hilo limerudiwa kwa mara nyingine tena kwa mwafrika wa pili, mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, Padre Richard Mjigwa wa Shirika la Damu Azizi, katika Siku Kuu ya Malaika wakuu Gabrieli, Michaeli na Raffaeli ambapo Malaika Gabrieli ni msimamizi wa Mawasiliano duniani. Pamoja na wafanyakazi wengine wa lugha ya nyingine na vitengo vya Baraza hilo, hata Padre Mjigwa kwa maana hiyo amepokea utambuzi huo wa zawadi ya heshima kutoka kwa Papa Francisko Alhamisi tarehe 29 Septemba 2022 kwa ajili ya huduma hii ya kuwasilisha bila kuchoka katika kueneza sauti ya Papa katika lugha ya Kiswahili katika mataifa na watu wote wanaosikiliza Radio Vatican kwa lugha ya Kiswahili.
Aliyewakabidhi zawadi hiyo kwa niaba ya Papa walikuwa na Dk. Andrea Tornielli Mhariri Mkuu wa Baraza la Mawasiliano mbele ya Dk. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano na katibu wake, ikiwa imeandikwa kwa kilatini Msalaba wa Heshima, Pro Ecclesia et Pontifice yaani kwa Kanisa na kwa Papa, ambayo kwa kawaida huwa wanapewa makleri au Walei kwa ajili ya huduma iliyotendwa kwa Kanisa na ukuu wake. Padre Mjigwa aliyezaliwa mnamo mwaka 1964 nchini Tanzania, alianza shughuli ya huduma ya uandishi wa habari kama mshirika mnamo mwaka 1994 hadi 1999 na baadaye kuanza rasmi huduma hiyo ya Lugha ya Kiswahili mnamo 2008 hadi sasa. Idhaa ya Kiingereza Afrika na Kiswahili, Radio Vatican, tunaungana kwa pamoja kwa furaha ya kumpongeza Padre Mjigwa na wengine waliotunukiwa zawadi hiyo ya heshima. Miongoni wageni, familia na ndugu jamaa na marafiki, Ubalozi wa Tanzania nchini Italia uliwakilishwa na watu wawili.
Tuzo na kibao cha Huduma ya kiswahili katika kutimiza miaka 30
Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, katika ukumbi wa Pio wa X katika jengo la makao makuu ya Mawasiliano, sherehe za utoaji wa zawadi ya heshima za Kipapa kwa baadhi ya watumishi waliojipambanua kwa kujituma na weledi katika kazi zao zilifanyika. Kibao cha ukumbusho kiliwasilishwa katika kuandhimisha miaka 30 ya kipindi cha Kiswahili, ambayo imetimia tarehe 27 Septemba. Maadhimisho ya miaka thelathini yanaashiria kurejea kwa lugha ya Kiafrika, ambayo historia yake katika kitengo cha utangazaji wa kipapa ni la zamani zaidi. Kwa njia hiyo ni siku kuu mara mbili kwa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kutimiza miaka 30 tangu kuanza tena matangazo yake ya kawaida mnamo tarehe 27 Septemba 1992. Hii ni kutokana na kwamba utangazaji wa lugha hiyo ulianza kwenye miaka ya sitini na baadhi ya Wamisionari wa Afrika (White Fathers). Kipindi cha lugha hii kwa hakika kilisikika kwa mara ya kwanza kwenye Radio Vatican mnamo tarehe 6 Novemba 1961. Papa Mtakatifu Yohane XXIII alizindua matangazo hayo ya kila siku kwa Afrika.
Tarehe 7 Julai: Ni Siku ya Kiswahili duniani
Kiswahili, ambayo ni lugha ya kibantu mwaka huu ilitambulika kama mojawapo ya lugha 10 zinazozungumzwa zaidi duniani. Katika bara la Afrika, KiSwahili, ndiyo lugha ya asili inayotumika sana. Inazungumzwa nchini Kenya, Tanzania na Uganda, na sehemu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi. Inakadiriwa kuwa kuna zaidi ya watu milioni 200 wanaosikiliza na kuzungumza KiSwahili barani Afrika na Mashariki ya Kati. Mwaka huu tarehe 7 Julai 2022, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni Ulimwenguni (UNESCO) liliadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani ambayo sasa itaadhimishwa kila mwaka. Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha kutoka nchi mbalimbali na huchukua asilimia 40% ya msamiati wake kutoka lugha ya Kiarabu. Hapo awali ilienezwa na wafanyabiashara wa Kiarabu kwenye pwani ya mashariki ya Afrika.
Dk. Ruffini Mkutano wa sinodi unamanisha mazungumzo na kusikilizana
Hata hivyo kabla ya tukio la kuwatunikia zawadi ya Heshima, ilitanguliwa na mkutano wa wafanyakazi wote wa Baraza la kipapa la Mawasiliano wakiwa na Mwenyekiti pamoja na Katibu wake katika Ukumbi wa Makao makuu ya Baraza la Mawasiliano, wa Pio X kuhusu baadhi ya masuala yaliyojitokeza katika mikutano ya kisinodi iliyofanyika miezi iliyopita. Katika hotuba yake Mwenyiti wa Baraza la Kipapa la mawasiliano Dk. Paolo Ruffini, alirejea kuzungumza juu ya mikutano ya sinodi hiyo. Akimshukuru kila mtu kwa ukweli, kushiriki na ubunifu wa mapendekezo, Dk. Ruffini alisisitiza umuhimu wa mkutano huo, ambao unamaanisha mazungumzo na kwa hivyo kusikiliza. Alikumbusha vile vile kila mtu juu ya upekee wa vyombo vya habari vya Vatican, mahali ambapo tamaduni tofauti, lugha tofauti huishi, lakini zote zimeunganishwa na kile kinachovuka kwa kasi, akionesha uzuri wa muktadha huo. Kwa njia hiyo mwasilishaji ana jukumu la kuona mema na mazuri ambayo yanatuunganisha na ambayo sisi mara nyingi tunayachukulia kuwa ya kawaida, huku akijitahidi kuelewa makosa yaliyofanywa pamoja, bila kuficha mambo muhimu na shida ili kufikiria ya baadaye pamoja. Kwa maana hiyo, tofauti katika umoja ni sifa ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano ambapo wameunganishwa na Walei na makasisi, wanaume na wanawake, kutoka nchi mbalimbali, wenye taaluma na karama mbalimbali, wanaohusika juu ya njia tofauti za mawasiliano. Sinodi kwa maana hiyo inaweza kuchaguliwa kama mtindo wa maisha, ili kuwa jumuiya na sio tu mahali pa kazi, alihitimisha.
Misa kwa heshima ya Malaika Mkuu Gabrieli Msimamizi wa Mawasiliano
Na katika misa Takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu Maria Traspontina, Roma kuadhimisha Siku Kuu ya Watakatifu Malaika Wakuu kwa namna ya pekee kwa Malaika Gabrieli msimamizi wa Mawasiliano na vyombo vya habari ulimwenguni aliyeongoza misa ni Monsinyo Lucio Adrián Ruiz, Katibu wa Baraza hilo. Katika mahubiri yake yalilenga Malaika Mkuu/ wakuu, huduma yao na umuhimu wa utume wao. Monsiny Rusi alisema Taalimungu ya malaika ni nzuri na muhimu, kwa sababu kwa mara nyingine tena wanadhihirisha uwepo wa Mungu katika historia ya mwanadamu, sio kama kitu cha mbali, lakini karibu na hatua ya kuelewa historia na kutenda ndani yake, kama walezi na hata zaidi malaika wakuu, kama walinzi wetu watatu ni wajumbe, katika hali ngumu za maisha ya mwanadamu ili kutusaidia kutembea, kwa sababu Mungu huwa hatuachi kamwe peke yetu, hakuna vita katika historia inabaki katika upweke, bila uwepo mwororo wa Mungu. Kwa maana hiyo hivyo Monsinyo Ruiz alitaka kutafakari juu ya jukumu la waandishi wa habari na kwa ujumla zaidi wa wawasilianaji. “Sisi pia tumekabidhiwa utume huu. Katika huduma yetu ya mawasiliano, inayohusiana na huduma ya Petro, sisi pia tunapaswa kuwalinda, kuwaponya na kuwaokoa watu wa Mungu kwa kuwafanya wafikie Habari Njema na kweli, kwa sababu katika utume tuliokabidhiwa kwetu sisi lazima tuwasilishe ukweli na kutumaini kwamba wanaweza kubadilisha historia ya watu na ulimwengu”, amesema.