Kubadili mtindo wa maendeleo kabla ya kuchelewa
Andrea Tornielli
Tangu Novemba 2013, katika wosia wa Evangelii gaudium ambao unawakilisha "ramani ya njia" ya upapa, Papa Fransisko alikuwa amezungumza kuhusu uchumi "unaoua". "Leo hii, aliandika Papa, kila kitu kinaingia kwenye mchezo wa ushindani na sheria ya wenye nguvu, ambapo wenye nguvu hula wadhaifu zaidi. Kama matokeo ya hali hii, umati mkubwa wa watu hujiona wametengwa na kubaguliwa: bila kazi, bila matarajio, bila njia ya kutokea. Binadamu huchukuliwa peke yake kama bidhaa ya matumizi, ambayo inaweza kutumika na kisha kutupwa. Tulianzisha utamaduni wa ‘kutupa’ ambao hata unahamasishwa... Waliotengwa ‘hawanyonywi’ tu bali wanakataliwa, ni ‘mabaki’”. Maneno haya, ambayo yalikuwa yamefanya Papa kuwa shtaka kubwa na vilevile lisilo na msingi kwa maoni na wafafanuzi wasiojua Mafundisho Jamii ya Kanisa, bado yangali ya sasa. Na Papa Francisko amerudi kuzungumza kwa uwazi akiwa Assisi, wakati akihutubia vijana ili kuomba kwa haraka mabadiliko katika mtindo wa maendeleo, hasa kiwa tunataka kuokoa ubinadamu unaotishiwa na majanga, vita na mabadiliko ya tabianchi. Uchumi ambao umechochewa na mwelekeo wa kinabii, Papa amewaambia vijana wa ‘Uchumi wa Francisko’ kuwa "unaoneshwa leo hii katika maono mapya ya mazingira na dunia. Kuna watu wengi, makampuni na taasisi zinazofanya uongofu wa kiikolojia. Lazima tuendelee kwenye njia hiyo, na kufanya zaidi.
Hii ‘zaidi’ mnayofanya sasa na mnaiomba kila mtu. Kufanya vipodozi haitoshi, mtindo wa maendeleo lazima uwekwe kwenye mjadala. Hali halisi ni kwamba hatuwezi kungojea tu mkutano mkuu wa kimataifa utakaofuata, ambao hauwezi kusaidia kwani dunia inawaka moto leo hii, na ni leo hii kwamba lazima tubadilike, katika ngazi zote”. Kwa hivyo, hatua fulani ya kijuu juu haitoshi, manufaa ya "greenwashing" hayatoshi kwa ajili ya kuendelea kufanya kila kitu kama hapo awali. Mtindo wa maendeleo lazima uwekwe kwenye mjadala mara moja. Suala hilo la Papa ni wito ambao inapaswa uende kwenye mzizi wa tatizo na ambao haujakubaliwa vya kutosha, kueleweka na kuungwa mkono katika miaka ya hivi karibuni. Ikilinganishwa na mwaka wa 2013, hali ni ya kusikitisha zaidi, kutokana na vita vilivyozuka katikati mwa Ulaya na uchokozi wa Urussi dhidi ya Ukraine, ambayo imafanya serikali kufungia kwenye droo zao sera za ikolojia ambazo hata hivyo tayari zilikuwa hazifanyi kazi.
Papa Francisko, ambaye katika waraka wa Laudato si' ameonesha jinsi njaa, vita, uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi yalivyounganishwa, amekumbusha akiwa Assisi kwamba "kilio cha maskini na kilio cha dunia ni kilio kimoja", huku akiomba kupendelea kati ya suluhushi za kimazingira, zile ambazo "hupunguza taabu na ukosefu wa usawa". Lakini hata kama mustakabali wa ulimwengu unaonekana kwetu leo hii katika rangi mbaya kwa sababu ya tishio la nyuklia linalokuja na mbio za wazimu sawa za kuweka tena silaha, kile kinachotoka Assisi ni ujumbe wa matumaini kwamba: "kuna vijana walioazimia kujitolea na ubunifu wa uchumi mpya, kwa uchumi tofauti na zaidi wa kibinadamu, kwa ajili ya fedha mpya ambayo katikati yake haina "mungu fedha" bali binadamu". Mtindo wa maendeleo unaweza kubadilishwa tu kwa ushiriki kutoka chini, na kwa serikali zilizosadikishwa juu ya hitaji la machaguo ya mbali ili kuhakikisha mustakabali wa dunia na wale ambao wanaoishi humo.