Tafuta

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vaticanamehutubia katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 77 , 2022. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vaticanamehutubia katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 77 , 2022.  (2022 Getty Images)

Hotuba ya Kardinali Parolin Kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Ili kudumisha amani kuna haja kwa watu wote kuweka silaha zao chini, lakini zaidi zile silaha ya maangamizi zinazoweza kuleta maafa makubwa zaidi kwa miji na nchi mbalimbali duniani. AMANI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vatican inapenda kupembua matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika Jumuiya ya Kimataifa kwa mwanga angavu wa Injili, Mafundisho Jamii ya Kanisa; mintarafu dhamana na utume wa Kanisa kwa familia kubwa ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pasi na ubaguzi. Vatican inapania kuendeleza uhuru wa kidini na kuabudu; utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazofumbatwa kwa namna ya pekee, katika Injili ya amani na utulivu, chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Amani ya kweli inajengwa kwa njia ya majadiliano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Bado kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi. Watu wengi wameathirika sana kutoka na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Yote haya ni matukio yanayopekenya utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Hizi ni changamoto za Jumuiya ya Kimataifa zinazopaswa kuvaliwa njuga na wote, ili baadhi ya watu na Serikali wasitumie huu mwanya kama njia ya kujiimarisha katika ukoloni wa kiitikadi unaosigana na haki msingi za binadamu ambazo kimsingi zinapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Matumizi ya silaha hasa za maangamizi ni hatari kwa usalama na amani
Matumizi ya silaha hasa za maangamizi ni hatari kwa usalama na amani

Uhakika na usalama wa chakula duniani bado ni tishio kubwa hadi kufikia mwaka 2030, kwani takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya asilimia 8% ya idadi ya watu wote duniani watahitaji msaada wa chakula. Kwa muhtasari huu ni mchango uliotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 77 huko New York, Marekani, anasema, tangu mwaka 2021 idadi ya watu wanaosiginwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni zaidi ya watu milioni 828. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika mchakato wa kuondokana na vita badala ya kujiandaa kuingia vitani, kwani madhara yake ni makubwa kama inavyojionesha katika vita kati ya Urussi na Ukraine. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha, anasema, ili kuweza kuwa na amani ya kudumu, kuna haja kwa watu wote kuweka silaha zao chini, lakini zaidi zile silaha ya maangamizi. Hizi silaha za nyuklia zinazoweza kuleta maafa makubwa zaidi kwa miji na nchi mbalimbali duniani. Kwa mara nyingine Baba Mtakatifu Francisko anasema bila kupepesapepesa macho kwamba: utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema.

Silaha za nyuklia ni hatari sana kwa mafungamano ya kimataifa.
Silaha za nyuklia ni hatari sana kwa mafungamano ya kimataifa.

Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Bila ya kuzingatia na kutekeleza kwa vitendo: sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa, Ulimwengu utaendelea kutumbukia katika majanga, kutokana na ukosefu wa: usalama, amani na utulivu na kwamba, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kutoa mchango wao kama inavyopaswa, kama kielelezo cha ushirika pamoja na kuchangia gharama zinazotolewa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kudumisha amani, kulinda, utu na heshima ya binadamu. Vitendo vya kigaidi, athari za mabadiliko ya tabianchi, vita vya muda mrefu huko DRC, Sudan, Chad, Mali, Burkina Faso na Guinea vinapaswa kukomeshwa na hatimaye, kukazia mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; upatanisho, ushirikiano na mafungamano ya kijamii Kimataifa. Hali bado ni tete nchini Haiti, Nicaragua, Azerbaijan na Armenia, kumbe kuna haja ya kukazia makubaliano ya amani pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuongeza juhudi ili chanjo dhidi ya Malaria iweze kupatikana kwa watu wengi zaidi ili kupunguza vifo vya watu wengi Barani Afrika.

Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili na kiutu.
Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili na kiutu.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika huko Sharm El Sheikh nchini Misri, kuanzia tarehe 6-18 Novemba 2022 ni sehemu ya mchakato kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21. Vatican imekwisha kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia. Kuna pengo kubwa katika Ulimwengu wa kidigitali na analogia ambao kimsingi unapaswa kusimikwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu, kama chachu ya kupambana na umaskini, ili kukoleza maendeleo fungamani ya binadamu. Lakini, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa makini kwa sababu kuna baadhi ya waamini wanatumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kupandikiza misimamo mikali ya kidini na kiimani; ukoloni wa kiitikadi pamoja na kusambaza habari za kughushi ambazo kimsingi ni hatari sana. Haki jamii ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira na mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani, ili kujenga na kudumisha uchumi bora zaidi, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Huu ni wakati wa kutumia matatizo na changamoto mbalimbali ili ziweze kuwa ni fursa.

Parolin UNGA 77

 

 

 

27 September 2022, 17:29