Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022: Dr. Paolo Ruffini: Ushirika!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki, SIGNIS, liliundwa kunako mwaka 2001 na kutambuliwa rasmi na Vatican tarehe 24 Oktoba 2014 baada ya kuunganisha Mashirika ya OCIC, lililoanzishwa mwaka 1928 na UNDA mwaka 1945 kushughulikia masuala ya tasnia ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki katika mchakato wa kutetea, kulinda na kudumisha utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi. SIGNIS inapaswa kujielekeza zaidi katika masuala ya haki, amani na upatanisho, kama sehemu ya utume wake ulimwenguni ili kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa kweli na mwanga wa Kiinjili. SIGNIS kuanzia tarehe 15-19 Agosti 2022 huko mjini Seoul, Korea ya Kusini, linaadhimisha Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Amani katika ulimwengu wa kidigitali” linalohudhuriwa na wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mkutano unaofanyika kwa wajumbe kuhudhuria mubashara na wengine kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Korea ni nchi ambayo vyombo vya mawasiliano ya jamii vimesaidia sana katika mchakato wa uinjilishaji, dhamana iliyotekelezwa kwa kiasi kikubwa na waamini walei.
Mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa mawasiliano kwa njia ya kidigitali yameonesha ile nguvu ya kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano katika ushirika sanjari na majadiliano katika familia ya binadamu. Dhamana hii imejionesha kwa namna ya pekee kabisa wakati wa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 wakati watu wengi walipolazimika kukaa katika karantini. Ulimwengu wa kidigitali umekuwa ni chimbuko la taarifa msingi, lakini pia ulimwengu huu umesaidia familia na jumuiya za waamini kujumuika pamoja katika sala na ibada mbalimbali. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022 huko mjini Seoul, Korea ya Kusini. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anagusia masuaala ya maadili na utu wema; utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana katika ukweli na uwazi na kwamba, kusikiliza ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ulimwengu wa mawasiliano ya kidigitali na hasa mitandao ya kijamii imeibua masuala mazito mintarafu kanuni maadili na utu wema, mwaliko kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kufanya mang’amuzi ya busara, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya kweli na bora katika mahusiano ya kibinadamu. Baadhi ya tovuti zimekuwa ni kero na sumu, kwa kuchochea na kupandikiza chuki; pamoja na kusambaza habari porofu.
SIGNIS inaweza kuwasaidia hasa vijana wa kizazi kipya kukuza elimu na akili timamu na dhamiri nyofu ya kuweza kuchambua na kujifunza kutofautisha kati ya habari potofu na zile za kweli; mema na mabaya pamoja na kujikita katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, upatanisho wa kijamii na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika hotuba yake amegusia kuhusu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ujenzi wa ushirika, mawasiliano kama chombo cha huduma kinachopaswa kutumia vyema hekima na busara kwa kujikita katika ukweli na Heri za Mlimani; changamoto ya mawasiliano bora zaidi; Umuhimu wa SIGNIS katika mchakato wa mawasiliano ndani ya Kanisa yanayofumbatwa katika umoja. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya teknolojia na sayansi ya mawasiliano ya jamii katika masuala ya huduma za kitabibu na vifaa tiba pamoja na biashara za kielekroniki.
Hizi ni juhudi za binadamu katika kupambana na hali na mazungira yake, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hii ni kazi, ubunifu na usanii wa kisayansi unaobeba ndani mwake hekima ya Mungu inayowataka wanasayansi kujikita katika wongofu wa maisha ya kiroho ili vyombo hivi viweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, yaani kuwaunganisha watu katika medani mbalimbali za maisha, ili kumkomboa mwanadamu. Hapa uwajibikaji wa kijumuiya na kibinafsi unahitajika sana, ili kunogesha furaha na ushirika kati ya watu ili kuwaondolea “virusi vya upweke hasi” vinavyosigina upendo kati ya watu. Teknolojia iwapatie watu maarifa na isaidie kujenga mahusiano na mafungamano ya kidini. Lengo ni kufyakelea mbali matatizo yanayopelekea: mipasuko ya kidini, kinzani, nyanyaso, dhuluma pamoja na mifumo yote ya ubaguzi.
Ikumbukwe kwamba. Kuna mambo ambayo kamwe hayawezi kupimwa, bali ni sehemu ya ushuhuda katika mchakato mzima wa mawasiliano ya jamii. Haya ni mambo kama vile: mahusiano na mafungamano ya kijamii; ushirika na huduma. Kumbe, kuna haja ya kujenga mfumo wa mawasiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mawasiliano yanayowaunganisha na wala si kuwatenga watu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kujikita katika kupenda kwa pamoja, kukumbatia na kusaidiana; kutambua, kukuza na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kufarijiana sanjari na kuendelea kujikita katika matumaini. Ni mwaliko kutoka katika ubinafsi na kujiunga na wengine. Kujifungia katika ubinasi ni hatari sana na madhara yake yanaweza kujionesha katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. Evangelii gaudium, 87. Wanahabari watambue kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hiki ndicho kinachowaunganisha wote hata katika tofauti zao msingi.
Dr. Paolo Ruffini, anasem, huu ni wakati kwa Mama Kanisa kujikita katika misingi ya haki, amani na usawa, kwa kutumia macho na masikio ya imani. Ili kutekeleza jukumu hili, ni wajibu wa kudumu wa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili, ili kutoa majibu muafaka kwa maswali ya watu wa kizazi hiki. Ni jambo la busara kwa tasnia ya mawasiliano ya jamii kujikita katika unafishaji wa kanuni maadili, utu wema na ukweli unaofumbatwa katika huduma. Rej. Gaudium et spes, 4. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa sehemu mbalimbali za dunia havina budi kujielekeza katika mchakato wa mafungamano, ili kushinda dhana ya woga na utengano. SIGNIS kimsingi ni mtandao mkubwa wa mawasiliano ya jamii, lakini unakosa: ubunifu, unyenyekevu na uvumilivu na uaminifu kutoka kwa Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani, huku wadau wa tasnia ya mawasiliano wakisukumwa na Heri za Mlimani, mafundisho tanzu ya Kanisa, ili kutafuta na kuambata kile kilicho kweli, chema na kizuri. Mawasiliano ya jamii, yasaidie kuboresho mafungamano kati ya watu wa Mataifa. SIGNIS haina budi kujikita katika mchakato wa maboresho ya mawasiliano yanayosimikwa katika kanuni maadili na utu wema; mawasiliano yanayovunjilia mbali upweke hasi ili kujenga ushirika miongoni mwa watu wa Mataifa.
Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii waoneshe uthubutu wa: kuwatafuta na kuwaendea watu katika maeneo na “vijiwe vyao”, ili kuganga na kuponya magonjwa na udhaifu wa upweke. Huu ni mchakato wa kuinjilisha vyombo vya mawasiliano ya jamii, kwa kutangaza na kushudia: Ushirika ambao kimsingi ndio mfumo mpya wa mawasiliano unaosimikwa katika unyenyekevu bila majivuno wala “kupandisha mabega.” Baba Mtakatifu Francisko katika nyaraka zake za Kitume zilizochapishwa hivi karibuni: Laudato si; Evangelii gaudium, Gaudete et exsulate na Querida Amazonia, anakazia umuhimu wa kusoma alama za nyakati na kutoa majibu ya matatizo, changamoto na fursa hizi kwa mwanga wa Injili. Mawasiliano yasaidie kujenga na kudumisha ushirika, ukweli na uwazi; mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Wadau wa mawasiliano wajielekeze katika kukusanya, kupanga na kujenga mitandao ya mawasiliano, ili kuwashirikisha wengine: wema, uzuri na ukweli. Dhamana hii inaweza kunogeshwa zaidi na SIGNIS katika maisha na utume wake. Isaidie mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni na yote haya yawe ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Kila mwamini anaweza kuchangia katika mchakato wa maboresho ya mawasiliano ya jamii; kwa kujikita katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Inapendeza ikiwa kama mawasiliano haya yatakuwa ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na utakaso wa mwadamu, ili hatimaye, kuvunjilia mbali upweke hasi! Dhamana hii inakwenda kinyume kabisa cha mwelekeo wa sasa katika ulimwengu mamboleo.