Toleo la IV la Kozi ya mafunzo ya mawasiliano ya vyombo vya habari: 'Mawasiliano ni utume'
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Imetangazwa toleo la 4 la Kozi ya mafunzo ya Mawasiliano ya Vyombo vya habari yenye kuongozwa na mada: Mawasiliano ni Utume, 2022-2023, lililoandandaliwa na Umoja wa Kipapa wa Kimisionari (PUM), Kitengo cha Mawasiliano cha Taasisi ya Kipapa ya Chuo Kikuu cha Santa Croce (PUSC) na Shirika la Habari za Kimisionari (Fides). Kozi hiyo inawatazama hasa wanafunzi wa Vyuo chini ya Sheria ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, ambapo inapendekeza kufunda wahudumu wa kichungaji katika mtazamo unaozingatia mawasiliano na vyombo vya habari kuwa ni fursa ya kueneza Injili, ili waweze kupata uwezo na zana za kusimulia historia, matukio, mang’amuzi na uzoefu wa kufuatilia mipaka mipya ya utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.
Kozi ya mwaka mmoja
Kozi hiyo, ambayo inachukua mwaka mmoja wa masomo, inatarajiwa kutoa ujuzi wa kinadharia na wa vitendo kuhusu mawasiliano ya vyombo vya habari mbali mbali kupitia utafiti maalum na majaribio ya lugha za video, radio, wavuti, (tovuti) upigaji picha na uandishi. Mafunzo hayo yanahusisha mbinu na ufundi wa ujifunzaji kwa ajili ya kubuni na kutengeneza bidhaa za vyombo vya habari vya kidijitali kwa njia na vielelezo vya usemi wake.
Wanaotarajiwa katika kozi hiyo
Watakao hudhuria toleo la 4 la Kozi hiyo ambayo masomo yake yatafanyika katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Santa Croce, yaani Msalaba Mtakatifu na Kituo cha Kimataifa cha Uhuishaji wa Kimissionari (CIAM), ni mapadre, watawa, waseminari, wanafunzi wa udaktari na walei waliopo katika vyuo vya kimataifa vya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, hasa kutoka bara la Afrika, Asia na Oceania(Australia) na kutoka Nyumba za Kitume Barani Amerika zote. Umoja wa Wamisionari wa Kipapa unahifadhi haki ya kugharamia, kwa hiari yake, gharama za uandikishaji na ushiriki kwa wanafunzi waliochaguliwa, wanaotoka katika makanisa yanayotegemea Baraza ka Kipapa la Uinjilishaji.
Uwasilishaji na ufunguzi 15 Oktoba 2022
Uwasilishaji na somo la ufunguzi umepangwa kufanyika tarehe 15 Oktoba 2022, katikati ya mwezi wa umisionari, huku katika kufunga, ni baada ya masaa 130 ya masomo, ambapo imepangwa mnamo mwezi Mei 2023. Waalimu wa kozi hiyo wanaundwa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Santa Croce hasa kutoka Kitivo cha Mawasiliano ya Taasisi hiyo, lakini pia na waandishi wa habari, wataalamu wa radio na televisheni, dubbing na mawasiliano ya vyombo vingi vya habari. Dirisha la kujiandikisha tayari limefunguliwa hadi tarehe 15 Septemba 2022. Kwa maelezo zaidi unaweza kumwandikia: d.sebastianelli@pusc.it