Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Kwa Mwaka 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 19 Agosti inaadhimisha Siku ya Wahudumu wa Masuala ya Kibinadamu Duniani iliyoridhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2009. Hawa ni wafanyakazi ambao wako mstari wa mbele kuokoa maisha ya watu wengine, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao wenyewe. Hii ni kumbukumbu endelevu ya shambulio la kigaidi lililotokea kwenye Hotel ya Canal mjini Baghdad, nchini Iraq kunako mwaka 2003 na hivyo kupelekea watu 22 kupoteza maisha, akiwemo Bwana Sergio Vieira de Mello, aliyekuwa Mkurugenzi wa huduma ya kibinadamu nchini Iraq. Kwa upande wake, Dr. Aloysius John, Katibu mkuu Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linaloundwa na Mashirika wanachama 162 amesema, Siku hi ya Kimataifa imesherehekewa na Caritas kwa kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wake wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 200 sehemu mbalimbali za dunia, kwa kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Wafanyakazi wa Caritas Internationalis wanaendelea kushikamana na kuwahudumia maskini, wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi zaidi. Ni wafanyakazi ambao daima wapo, kabla, wakati na baada ya machafuko. Wapo ili kutoa huduma za kibinadamu, lakini kubwa zaidi ni kunogesha mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu ili kujenga udugu wa kibinadamu. Ni watu wanaotoa huduma lakini pia wanaendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Caritas Internationalis inabainisha kwamba, hali inazidi kuwa tete sana kutokana na ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula duniani na utapiamlo wa kutisha, kuchechemea kwa uchumi wa Kitaifa na Kimataifa; Vita kati ya Urussi na Ukraine ni mambo yanayoendelea kuchangia hali mbaya ya maisha kwa watu wengi duniani.
Bado kuna vita inayoendelea nchini Syria, Venezuela, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na DRC bila kusahau athari za mabadiliko ya tabia nchi. Baa la njaa linatishia usalama wa watu wa Mungu Ukanda wa Pwani ya Pembe, Barani Afrika pamoja na Ukanda wa Sahel. Vitendo vyote hivi vinasigina: utu, heshima na haki msingi binadamu. Athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuwatumbukiza maskini katika umaskini zaidi. Hii ni changamoto kwa wakuu wa Jumuiya ya Kimatafa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia mama na maskini, kwa kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na athari hizi. Ni wakati wa kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho katika ngazi mbalimbali; kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inabainisha kwamba, zaidi ya wafanyakazi 460 wa misaada walishambuliwa na zaidi ya wafanyikazi wa misaada 140 waliuawa katika mashambulio haya - idadi kubwa zaidi ya vifo vya wafanyikazi wa misaada tangu 2013. Hadi kufikia Agosti 2022 wafanyakazi wa misaada 168 wamekwishambuliwa, na kusababisha vifo vya watu 44.