Rais wa Jamhuri ya Watu wa Fiji Akutana na Kuzungumza na Papa Francisko Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 1 Agosti 2022 amekutana na kuzungumza na Rais Ratu Wiliame Maivalili Katonivere wa Jamhuri ya Watu wa Fiji, ambaye baadaye amepata fursa ya kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekua ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano pamoja na Mashirika ya Kimataifa.
Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, katika mazungumzo yao ya faragha, wamegusia masuala ya Kimataifa na Kikanda, lakini kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwa sababu madhara yake kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni makubwa sana. Viongozi hawa wawili wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuthamini mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Fiji katika ujumla wao.