Papa akutana na Bi Katalin Novák,Rais wa Jamhuri ya Hungaria
Vatican News.
Papa Francisko Alhamisi 25 Agosti 2022 amekutana na Bi Katalin Novák, Rais wa Jamhuri ya Hungaria mjini Vatican ambapo mara baada ya mkutano huo amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, akisindikizana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican kwa ajili ya Masuala ya Nchi na Mashirika ya Kimataifa.
Katika Mkutano wao na Katibu wa Vatican baada ya kukumbuka ziara ya Kitume ta Papa Francisko huko Budapest wakati wa fursa ya Kongamano la 52 la Kimataifa la Ekaristi mwezi Septemba mwaka jana, wameeleza kuridhika na uhusiano mwema uliopo kati ya nchi zao mbili. Kwa maana hiyo wamezungumzia juu ya masuala ya pamoja ambayo yanatazama familia, uhamasishaji wa utamaduni wa maisha, vijana na hali halisi ya wakristo wa nchi za Mashariki. Wakiendelea na mazungumzo yao pia wamegusia vita vya Ukraine na jitihada za amani.