Padre Federico Lombardi, SJ: Miaka 80 ya Kuzaliwa & Miaka 50 Daraja Takatifu Ya Upadre: Huduma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwa: ni wahudumu na vyombo vya ukweli, wema na uzuri, kwa kusimama kidete kutetea kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu, ili kujenga na kudumisha ushirika, upendo na mshikamano wa kidugu kati ya watu. Mawasiliano ya jamii iwe ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu, ili kuganga na kuponya madonda yanayo sababishwa na habari potofu na za kughushi, zinazodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wadau wa tasnia ya mawasiliano wanapaswa kuendeleza kipaji cha ubunifu ili kuwaondoa watu jangwani na hivyo kuanzisha mchakato wa mawasiliano mubashara unaojenga na kudumisha mahusiano na mafungamano bora zaidi ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni muda wa kujenga na kudumisha ujasiri unaofumbwatwa katika misingi ya ukarimu, udugu na mshikamano wa kibinadamu. Mtandao wa mawasiliano ya jamii hauna budi kuendelezwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na kuzingatia mahitaji ya watu mahalia. Huu ni mfumo wa kidigitali na unaozingatia ukweli, ili kuwaunganisha watu katika medani mbalimbali za maisha na kamwe si kuwatenganisha na kuwasambaratisha.Maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii hayana budi kuwa na mwelekeo wenye mafao mapana zaidi kwa watu wa Mungu. Huu ni wakati wa kujikita katika mawasiliano dhidi ya virusi vya uchoyo na ubinafsi, ili kudumisha umoja, mshikamano, ukweli na kuendeleza mchakato wa watu kukutana katika misingi ya ukweli na uwazi; upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu Mahusiano na mafungamano yamwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kujenga uchumi shirikishi, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu.
Huu ndio msingi na ndoto pana zaidi ya mawasiliano ya kijamii, Mama Kanisa anapomshukuru Mungu kwa kumwimbia utenzi wa sifa na shukrani; kwa zawadi ya miaka 80 tangu alipozaliwa Padre Federico Lombardi, SJ na miaka 50 tangu alipowekwa wakfu kuwa Padre, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni Padre ambaye katika maisha yake, amebahatika kufanya kazi na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Padre Federico Lombardi, SJ alizaliwa tarehe 29 Agosti 1942 huko Saluzzo, Italia, “akajichimbia” katika somo la hisabati na kufaulu kutunukiwa Shahada ya uzamili na hatimaye, mwaka 1972 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre sanjari na kuanza kushirikiana na Jalida la “La Civiltà Cattolica” linalomilikiwa na kuchapishwa na Wayesuit.
Kati ya mwaka 1984 hadi mwaka 1990 alichaguliwa kuwa Padre mkuu wa Kanda ya Wayesuit nchini Italia. Kati ya mwaka 1990 hadi mwaka 2016 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Vipindi Radio Vatican na baadaye akateuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa Radio Vatican. Kati yam waka 2001 hadi mwaka 2013 aliteuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV: Centro Televisivo Vaticano. Tarehe 11 Julai 2006, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa ni Msemaji mkuu wa Vatican, huduma iliyofikia ukomo wake tarehe 31 Julai 2016. Ilikuwa ni tarehe 1 Agosti 2016 Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alipo mteuwa Padre Federico Lombardi, SJ kuwa Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger – Benedetto XVI, ulioanzishwa kunako mwaka 2010. Mfuko huu unapania kwa namna ya pekee kusaidia juhudi za Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mfuko ambao unajikita katika kumwilisha Injili ya upendo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kumi na wawili kila mwaka kupata nafasi za masomo kutoka ndani na nje ya Italia. Mfuko wa Joseph Ratzinger unasaidia pia kugharimia makongamano ya kitamaduni na kisayansi kadiri ya katiba ya mfuko huu kwani unatambua kwamba, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni mahali muafaka pa kukuza na kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.
Mfuko huu pia unatoa tuzo kwa wasomi waliojipambanua katika huduma kwa ajili ya kushuhudia na kueneza Injili ya Kristo kwa watu wa mataifa, ili kweli Injili iweze kuingia na kugusa mila, desturi na tamaduni za watu dhamana inayoweza kutekelezwa kwa dhati kabisa kwa njia ya weledi wa kitaaluma, kisayansi na kielimu. Padre Federico Lombardi, SJ katika mahoniano maalum na Vatican News anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii hususan vijana wa kizazi kipya kuifanya kazi ya uandishi wa habari kuwa ni sehemu ya wito wa maisha yao na wala si tu kama taaluma inayowapatia chakula chao cha kila siku. Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wote aliomtendea katika maisha yake; amekutana na vizingiti, lakini kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu akaweza kuvivuka na hivyo kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Katika maisha na utume wake kama mwandishi wa habari za Kanisa, amejifunza umuhimu wa kumwilisha imani katika matendo, ili hata habari zinazotolewa ziwe ni kwa ajili ya huduma inayozingatia: Ukweli, wema na uzuri, kwa kusimama kidete kutetea kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu, ili kujenga na kudumisha ushirika, upendo na mshikamano wa kidugu kati ya watu. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ushuhuda na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu ni sehemu ya amana, vinasaba na utume wa Mama Kanisa ulimwenguni. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii, kwa njia ya utume wao, wanapaswa kunogesha ujenzi wa daraja la mawasiliano kati ya Mungu na binadamu.
Tasaufi ya Mtakatifu Inyasi, imemsaidia sana katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni tasaufi inayomwonesha Mungu akiwa anatenda kazi ndani ya waja wake, jambo la msingi ni kutambua na kukiri uwepo wake wa daima. Padre Federico Lombardi, SJ anakiri kwamba, sehemu kubwa ya maisha yake, amekuwa karibu sana na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Baba Mtakatifu Francisko, mahusiano na mafungamano yake pamoja nao ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu. Hii ni huduma kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Na kwa hakika anamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumwita na kumwezesha kutekeleza utume huu ndani ya Kanisa. Mawasiliano ya jamii, yawasaidie watu kufahamu na kuambata ukweli; kutangaza na kushuhudia mazuri yanayopatikana katika maisha ya watu na wala si kujikita tu katika habari za “udaku na kashfa” kwani hizi hazitakosekana katika maisha ya mwanadamu. Waandishi wa habari wajitahidi kutambua uzuri, ukuu na utakatifu wa kazi na utume wao kwa watu wa Mungu na wala wasimezwe na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini zaidi, wajitahidi kujenga jamii inayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Padre Federico Lombardi, SJ anahitimisha mahojiano maalum na Vatican News kwa kusema, hata wazee katika uzee wao, wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni watu wanaokazia amana na tunu msingi za maisha katika tasnia ya mawasiliano, badala ya waandishi wa habari kujitafuta wenyewe. Mambo msingi kama vile: ukweli, wema na uzuri yaendelee kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na kama chemchemi ya matumaini.