Mkutano wa 19 wa SECAM 2022: Vyombo Vya Mawasiliano ya Jamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022, limekuwa ikiadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 huko Accra, nchini Ghana kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Umiliki wa SECAM: Usalama na Uhamiaji Barani Afrika na Visiwani. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, katika ujumbe wake amekazia ujumbe uliotolewa na Mababa wa SECAM katika Waraka wa Kampala wa Mwaka 2019 unaoongozwa na kauli mbiu “Wapate Kumjua Kristo na Kuwa na Uzima tele” (Yn 17:3; 10:10. Waraka huu pamoja na mambo mengine unakazia umuhimu wa mawasiliano Barani Afrika. Wataalam wa sayansi ya mawasiliano ya jamii wa Kikatoliki wanahimizwa kutekeleza dhamana na utume wao kwa kuzingatia usawa; kwa kutafuta na kuanzisha mahusiano na mafungamano ya Kikanisa na ya Mashirika ya Kimataifa. Mababa wa SECAM waliahidi kuboresha na kuimarisha kitengo cha mawasiliano ya jamii, kwa kutumia rasilimali zake ili kuboresha mawasiliano kwa Kanisa Barani Afrika. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa Kanisa Barani Afrika kuendelea kuwekeza katika malezi ya kitaaluma, kiufundi, kimaadili na kiutu kwa mihimili yote ya uinjilishaji, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza katika kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Malezi na majiundo makini ya wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii Barani Afrika ni muhimu sana kwa wakati huu, pengine hata kuliko nyakati za nyuma.
Ni katika muktadha huu anasema Dr. Paolo Ruffini kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Ecclesia in Africa” yaani “Kanisa Barani Afrika,” alikazia umuhimu wa ushirikiano na mafungamano kati ya wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii Barani Afrika, ili kujenga na kudumisha umoja na ushiriki wa waamini katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Ushirika huu unapaswa pia kudumishwa kati ya SECAM na Mashirika mengine ya Kimataifa, ili kuweza kusaidia mchakato wa kuwaandaa wadau wa tasnia ya mawasiliano kitaaluma, kiutu na kimaadili. Kumbe, Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, “Pan African Episcopal Conference For Social Communication, CEPACS inapaswa kutiwa moyo na kufufuliwa. Mtakatifu Yohane Paulo II alikazia kwa namna ya pekee kabisa, ushirikiano katika taaluma na ufundi kati ya vyombo vya mawasiliano ya jamiii vinavyoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki Barani Afrika. Ushirikiano huu pamoja na mambo mengine ulipania kuhakikisha kwamba, habari kutoka katika vyombo hivi zinawafikia watu wengi ndani na nje ya Bara la Afrika. Tasnia ya mawasiliano ya jamii, licha ya changamoto kubwa ya rasilimali fedha na watu, lakini inaendelea kukua na kupanuka, ikilinganishwa na wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Maaskofu Barani Afrika.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, alimteuwa Askofu Emmanuel Adetoyese Badejo wa Jimbo Katoliki Oyo, Nigeria kuwa ni kati ya wajumbe wa Barazza la Kipapa la Majawasiliano ya Jamii. Lakini, hata Mababa wa SECAM katika Waraka wa Kampala wa Mwaka 2019, unazihimiza taasisi na vyuo vikuuu vya Kikatoliki kuhakikisha kwamba, vinatoa fursa ya masomo na mafunzo ya mawasiliano ya jamii, kiutu na kitaaluma, sanjari na uundwaji wa mitala itakayosaidia kuboresha taswira ya Bara la Afrika katika ujumla wake. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, anavipongeza vituo mbalimbali vya Radio Barani Afrika vinavyoshirikiana kwa karibu sana na Radio Vatican katika lugha ya: Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kiswahili kurusha tena matangazo ya Radio Vatican katika nchi mbalimbali. Ushirikiano huu, umewawezesha watu wa Mungu Barani Afrika kuweza kufahamu yale yanayojiri kila siku kwa upande wa Kanisa la Kiulimwengu. Na kwa upande mwingine, habari za watu wa Mungu Barani Afrika zimeweza kusikika katika vyombo mbalimbali vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican.
Ushirikiano, mshikamano na mafungamano haya yanapaswa kuboreshwa zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Wadau wa tasnia ya mawasiliano daima wakumbuke kwamba, “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.” Kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, Kanisa linaweza kusimama kidete kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili mintarafu hali na roho ile ya umoja na mshikamano kama ilivyokuwa katika Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, ingawa watu walikuwa wanatoka katika Mataifa na Makabila mbalimbali, lakini kila aliweza kupata ujumbe kwa lugha yake mwenyewe, matendo makuu ya Mungu na hivyo kuvunjilia mbali, mifumo ya mawasiliano inayopelekea watu wa Mungu kushindwa kupata ujumbe unaokusudiwa. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo anakazia kuhusu: Ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; umuhimu wa kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari pamoja na waamini walei kuendelea kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!
Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani pamoja na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anakaza kusema, vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuhusishwa kikamilifu katika utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ili waweze kufanya upembuzi yakinifu wa matukio mbalimbali yanayowazunguka; wajifunzee kutofautisha ukweli na uwongo; mema na mabaya.
Wajifunze pia kuthamini maisha adili na matakatifu; kufanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa; kusimama kidete kutafuta, kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; pamoja na kuendelea kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa haki, amani na maridhiano; kwa kuheshimu na kuthamini: utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, mawasiliano si huduma peke yake, bali pia ni chombo cha majadiliano katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kijamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. SECAM katika maisha na utume Barani Afrika isaidie kukuza na kudumisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, daima ikijieleza kutatua changamoto za ukosefu wa haki, amani na utulivu kati ya watu wa Mungu Barani Afrika. Yote yawe ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, ili hatimaye, familia ya watu wa Mungu Barani Afrika iweze kutakatifuzwaa.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa 19 wa SECAM, tarehe 26 Julai 2022 Rais Nana Addo Dankwa Akufo-Addo wa Ghana alikazia pamoja na mambo mengine, usalama wa raia na mali zao; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji Barani Afrika na athari zake kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ugenini. Katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 tangu nchi nyingi Barani Afrika zijipatie uhuru wake wa bendera, mapinduzi ya kijeshi, magonjwa, ujinga na umaskini, vimeendelea kutawala. Kuna vijana wengi wanaotamani maisha bora zaidi na matokeo yake wanakimbia nchi zao, lakini njiani wanakupamba na maafa, nyanyaso, ukatili na sheria kandamizi ugenini na hivyo ndoto za maisha bora zaidi, zinayeyuka na kutoweka kama umande wa asubuhi. Umaskini, vita, kinzani, migogoro, rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni kati ya mambo yanayokwamisha mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika elimu itakayoleta ukombozi wa kweli kwa watu wa Mungu Barani Afrika, kwa kuwajengea moyo wa uzalendo, juhudi, bidii na maarifa ya kazi. Watu wa Mungu Barani Afrika wajenge pia utamaduni na moyo wa uzalendo; kwa kupenda nchi na bidhaa zinazozalishwa Barani Afrika, ubora ukizingatiwa. Demokrasia, utawala bora na utawala sheria uendelezwe kukuzwa Barani Afrika kwa kuwahusisha pia vijana wa kizazi kipya, Kanisa liendelee kusimama kidete katika utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuendelea pia kujielekeza katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rais Nana Addo Dankwa Akufo-Addo wa Ghana anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwateuwa Askofu Richard Kuuia Baawobr, M. Afr. Wa Jimbo Katoliki la Wa, Ghana kuwa Kardinali na ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa SECAM, matendo makuu ya Mungu. Mwingine ni Kardinali mteule Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki la Ekwulobia nchini Nigeria bila kumsahau Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, mwenye umri wa miaka 73 na ambaye ni Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, ambaye asili yake ni Ghana.